-Kuendeshwa na wakufunzi wa Man U
-Kushirikisha nchi 12
-Tanzania kuwakilishwa na wachezaji 19

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania leo imetangaza kufanyika kwa kliniki ya soka ya Kimataifa ya Manchester United hapa Dar es Salaam kuanzania 23 -27 Aprili mwaka huu.

Kliniki hiyo ambayo itafanyika kwenye uwanja wa Azama FC (Chamazi Complex Stadium), ina nia ya kuwaendeleza vijana waliofanya vizuri kwenye michuano ya mwaka jana ya kimataifa ambayo ilifanyika Lagos, Nigeria na kushirikisha nchi 12 ambapo timu ya Tanzania ya wasichana iliibuka mabingwa.

Hii ni mara ya pili kwa kliniki kama hiyo kufanyika hapa nchini kufuatia kliniki kama hii liyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa 2011. Kliniki nyingine ilifanyika Nairobi 2012 na Tanzania iliwakilishwa na wavulana watatu na wasichana watatu.

Kama ilivyokuwa kwenye kliniki zilizopita, kliniki ya mwaka huu itaendeshwa na makocha kutoka shule za soka za Klabu ya Manchester United na wanatarajiwa kutoa mafunzo ya awali ya mpira wa miguu kama vile kupiga pasi, kukimbia na mpira, kupiga mashoot, nidhamu na nyingine nyingi.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice Singano alisema kliniki hiyo ni sehemu ya mpango kapambe wa Airtel kusaka na kuendeleza vipaji vya soka hapa Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.
IMG_0793
Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania Beatrice Singano akiongea na waandishi wa Habari wakati wa kutangaza Kliniki ya Kimataifa ya mpira wa soka ya Manchester United ambayo itafanyika Jijini Dar es Salaam April 23-27 chini ya wakufunzi kutoka Klabu ya Manchester United. Kulia ni Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Tanzania Public Relations Officer Jane Matinde. 

 ‘Airtel inajivunia kuwekeza kwenye soka ambayo ina uwezo wa kuileta jamii pamoja kupitia hamasa ya mashabiki na yenye uwezo wa kuwafanya wachezaji kupata elimu pamoja na ajira’, anasema Singano.

Aliongeza kuwa Airtel inajivunia programu ya Airtel Rising Stars kwa kuleta furaha na hamasa kubwa miongoni mwa vijana wa Tanzania na pande nyingine za Bara la Afrika hivyo kuifanya kampuni ya Airtel kuhamasika kuendelea kuwekeza kwenye soka.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Celestine Mwesigwa ameishukuru kampuni ya Airtel kwa mpango huu makini wenye nia ya kutafuta na kuendeleza vipaji chipukizi vya soka Tanzania.

 ‘Ninaamini ya kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na vipaji vingi vya soka. Tunachohitaji ni uwezo wa kifungi na raslimali za kutuwezesha kusonga mbele na ndio maana tunawashukuru Airtel kwa kujitokeza kutuunga mkono kupitia programu hii ya vijana’, Anasema katibu wa TFF.

Washiriki wa kliniki hii watatoka nchi za Kenya, Uganda, Malawi, Chad, Burkina Fasso, Sierra Leon, Sheli sheli, Congo Brazzaville, Nigeria, Zambia na wenyeji Tanzania ambao watawakilishwa na wachezaji 19.

Airtel Rising Stars ni programu inayojumuisha Africa nzima ili kutoa nafasi kwa wanasoka chipukizi chini ya umri wa miaka 17 kuonyesha uwezo wao mbele ya mawakala wa soka, makocha na kupata fursa ya kujiendeleza zaidi. Mpango huu unawalenga wavulana na wasichana Barani Afrika.