Sunday, August 17, 2014

KIGOGO CCM AKATALIWA NA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU

Na Allan Ntana,Tabora

WAJUMBE zaidi ya 130 wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi
Tabora mjini wamemkataa Katibu wa Chama hicho wilaya ya Tabora mjini
Bakar Luasa kwa madai ya kukigawa na kukichafua.

Hatua hiyo ilifikiwa Agosti 12 mwaka huu baada ya wajumbe hao
kuamua kutoka nje ya ukumbi wa Ali Hassan Mwinyi kwa madai ya kutokuwa
na imani na Katibu huyo wa CCM wilaya.

Chanzo cha taarifa toka kwa wajumbe wa halmashuri kuu ya CCM ndani ya
kikao hicho ambao hawakutaka majina yatajwe walisema kufuatia hali
hiyo kikao kiliahirishwa na kufanyika tena mwezi Agosti 13 mwaka huu.

Wajumbe hao walisema baada ya kuingia ukumbini walitoka
nje na kuongea kwa nyakati tofauti wakidai hawamtaki Katibu wao Bakar
Luasa kwa madai kuwa hawana imani naye na anakigawa chama.

“Huyu Katibu wetu ana kama miezi sita au saba hivi na toka amehamia hapa Tabora
lakini tokea afike amekuwa akikivuruga chama kwa migogoro
isiyoisha…….kwa kujifanya yeye anajua ilani na taratibu za chama kila
kukicha anagombana na Mwenyekiti wake”, waliongeza.

Walisema Mwenyekiti wa CCM Tabora mjini Abrahman Nkonkota aligombea
vipindi viwili na
akashinda kwa kura nyingi hivyo kama Mwenyekiti wetu ana tatizo wapo zaidi
ya Makatibu wanne ambao wamepita hatukuona wanakwaruzana naye.

Walisema Katibu huyo wana taarifa anapokea fedha kila mwisho wa mwezi
ili aendeleze fujo na kugawa chama kwa maslahi yake na kamwe
hawataweza fanya kazi na Katibu Bakar Luasa kutokana na kuendeleza
majungu na fitina.

Walisema alipeleka taarifa Makao Makuu ya chama kuwa hakuna
watendaji, sasa wanachama na wajumbe ambao hawamtaki tunatamka wazi
kuwa tunatoka nje ya ukumbi, hatumtaki.
 
Mwandishi wet alimtafuta Katibu wa CCM Bakar Luasa kuhusiana na madai
hayo ambapo alisema yeye hana tatizo, mwenye tatizo ni Mwenyekiti wake
kwani ndiye anaratibu hayo.

“Mimi nafikiri kila kitu kiko wazi kama mimi ni tatizo kwani katibu
mkuu wa CCM Abdurahaman Kinana alikuja akaelezwa na makamu
mwenyekiti wa CCM Philip Mangula naye alielezwa tunasubiri maamuzi ya
kamati kuu ya CCM” alisema.

Alisema kwa kuwa kamati kuu inataka kuchukua maamuzi dhidi yangu na
Mwenyekiti, sina cha kueleza zaidi tusubiri.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora mjini Abdulrahaman Moshi Nkonkota
alijibu kuwa tuhuma hizo si za kweli yeye hana matatizo kwani kila kitu kiko
wazi,..... mimi siwezi kushawishi wajumbe zaidi ya 140 wamkatae Katibu wangu
ili iweje, aliongeza.

Alisema, ukweli ni kwamba anagawa chama,  hapa ofisini haelewani na
watendaji, wanachama na mimi mwenyewe kwani hataki kufanya kazi na mimi.

MAJAJI WA SHINDANO LA TANZANIA MOVIE TALENT (TMT) WAKIFUATILIA FILAMU FUPI ILIYOCHEZWA NA BAADHI YA WASHIRIKI WA SHINDANO HILO

Majaji wa Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) wakifuatilia Filamu fupi iliyochezwa na baadhi ya washiriki wa Shindano la Tanzania Movie talents (TMT) wakati ilipokua ikionyeshwa kwenye runinga kubwa katika Ukumbi wa Makumbusho. Kutoka Kulia ni Single Mtambalike au Rich Rich katikati ni Vyonne Cherry au Monalisa na Kushoto ni Jaji Mkuu wa Shindano hilo Roy Sarungi.
 Mahosti wa Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) Joti na Lulu wakiwajibika katika Jukwaa la Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa wakati shindano hilo lilipokuwa likiendelea alhamisi iliyopita.
 Mmoja kati ya Washindi kutoka Kanda ya Pwani, Mkoa wa Dar Es Salaam katika Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) Shiraz Ngassa (wa Kwanza Kushoto) akiongea na Msanii Joti mara baada ya Kuaga rasmi shindano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa siku ya alhamisi.
 Fredy Kiluswa ambae pia alikuwa mmoja kati ya Washindi watano kutoka Kanda ya Pwani katika Hatua ya kuwatafuta washindi wa Kanda akitoa maneno ya Shukrani mara baada ya kuaga shindano hilo kutokana na uchache wa kura alizopata.
 Baadhi ya washiriki wa kundi la Kwanza wakiwa mbele ya Majaji wa Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) mara baada ya Filamu yao fupi kuonyeshwa.
Mwinshehe Mohamed ambae alikua mmoja kati ya Washindi wa Tatu kutoka Kanda ya Kati mkoa wa Dodoma akitoa pongezi na Maneno ya Shukrani kwa Timu nzima ya TMT mara baada ya kuaga shindano alhamisi katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
 Baadhi ya washiriki wa Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) waliofanikiwa kuingia hatua ya Fainali ambapo mshindi wa Shindano hilo linalotarajiwa kufikia Tamati Mnamo mwisho wa Mwezi wa Nane kwa Mshindi Kukabidhiwa Kitita Cha Shilingi Milioni hamsini za Kitanzani.Picha Zote na Josephat Lukaza - Proin Promotions ltd

Na Josephat Lukaza - Proin Promotions Limited - Dar Es Salaam.
Hatimaye Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) limefikia hatua ya Mwisho kabisa mara baada ya washiriki kumi bora kupatikana katika Show ya Mchujo iliyofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa siku ya Alhamisi.

Show hiyo ya Mwisho katika katika Hatua ya mchujo ilifanyika siku ya Alhamisi na kupelekea Washiriki watatu kutoka Kanda Mbili za Tanzania yaani Kanda ya Kati na Kanda ya Pwani kuondolewa katika Kinyanganyiro hiko na Kupelekea Shindano hilo kubaki na washiriki 10 tu ambao wameingia hatua ya fainali ambapo mshindi mmoja ataondoka na kitita cha Shilingi Milioni 50 za kitanzania katika Fainali Kubwa inayotarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mlimani City siku ya Tarehe 30 Mwezi huu wa Nane.

Washiriki waliondolewa katika Kinyanganyiro Hiko ni Mwinshehe Mohamed ambae alikuwa mmoja kati ya Washindi watatu kutoka Kanda ya Kati ambapo anafanya Idadi ya washiriki wawili kutoka Kanda ya Kati kuondolewa na Kuifanya Kanda ya Kati kuwakilishwa na Mshindi Mmoja katika Fainali hiyo.

 Wengine waliotoka ni Shiraz Ngassa na Fredy Kiluswa ambao wote ni Washindi kutoka kanda ya Pwani Mkoa wa Dar Es Salaam. Kanda ya Pwani walichukuliwa washindi watano huku Shiraz na Fredy wakitimiza idadi ya Washiriki wanne kuondolewa katika kinyanganyiro hiko kwa Kanda ya Pwani, Tishi Abdallah ndie Mshindi mmoja kati ya washindi watano kutoka kanda ya Pwani ambae anaiwakilisha Kanda ya Pwani katika Fainali kubwa ya Shindao la Kwanza na la Kipekee kufanyika Afrika Mashariki na Kati la Tanzania Movie Talents (TMT).

Mpaka Sasa Ni Kanda Moja tu ambayo washindi wake wote watatu ndio wanaiwakilisha Kanda hiyo katika Fainali kubwa itakayofanyika Mwishoni Mwa Mwezi wa Nane katika Ukumbi wa Mlimani city ambapo mshindi mmoja ataondoka na Kitita Cha Shilingi Milioni 50 za Kitanzania huku washindi wote kumi waliofanikiwa kuingia Katika hatua ya Fainali watakuwa chini ya Kampuni ya Proin Promotions limited ambapo watacheza filamu ya pamoja na Hatimaye kuanza kunufaika na Mauzo ya Filamu hiyo inayotarajiwa kutoka Hivi Karibu.

Vipindi vya Shindano hili la Tanzania Movie Talents (TMT) vitaendelea kurushwa katika Kituo cha Runinga cha ITV siku ya Jumamosi Saa 4 Usiku huku marudio yake yakiwa siku ya Jumapili Saa 10 Jioni na Siku ya Jumatano saa 5 usiku.

Ili Kuendelea kumuwezesha Mshiriki wako kuibuka mshindi wa Shindano la Tanzania Movie Talents (TMT) kwa Mwaka 2014 unachotakiwa ni kuendelea kumpigia kura kwa wingi kadri uwezavyo kwa Kuandika Ujumbe Mfupi wa Maneno (SMS) Neno TMT acha nafasi ikifuatiwa na namba ya Mshiriki halafu tuma kwenda 15678. Mfano TMT 00 halafu tuma kwenda 15678 au unaweza kupiga kura pia kupitia Ukurasa wetu wa Facebook kwa kufungua kiunganishi hiki https://www.facebook.com/tztmt/app_316963748468949

CHADEMA YAKUBALI KUSHIRIKIANA NA ACT-KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma

CHAMA  cha  Demokrasia  na  Maendeleo (Chadema) mkoani hapa,kimekubali kushirikiana na vyama vya upinzani kikiwemo chama kipya cha ACT  kwa lengo la kukiondoa madarakani  chama Tawala ambacho ni chachu ya kudumaza huduma za jamii zishio vijijini.
 
Kauli hiyo ni moja ya harakati ya uongozi mpya wa chama hicho kukiri mabadiliko ya mfumo wa vyama vya upinzani  vinahitaji dhati ya mshikamano,uwazi,uwajibikaji  na utoaji wa elimu sahihi ya uraia kwa tija ya umma kubaini uhalisia wa mambo hatimaye kukiondoa chama tawala madarakani 2015.
 
Mwenyekiti wa chadema Mkoa huo  Ally Kisala alisema kukaidi kuviunga mkono vyama vipya ni moja ya mapungufu ya vyama kutokukubali alama za nyakati  ambazo huchangia baadhi ya viongozi wa vyama husika kutumia muda mwingi  kuponda uongozi wa chama kingine ambapo wote wana nia ya kushika dola kwa mujibu wa katiba zao.
 
Kisala alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya mwanga center kigoma ujiji,uliokuwa ukitambulisha safu ya uongozi mpya wa chadema na kuelezea wananchi uhai wa chama mkoani hapo na  lengo la  vyama vya upinzani ni kukiondoa ccm kwenye mfumo wa utawala wa miaka kenda usiorasimisha mabadiliko ya  utawala mpya kwa kushindwa  kuwajibikaji kwa viongozi wazembe.
 
“hatunahaja  ya kulumbana,tunataka tuungane ili kukitoa ccm katika madaraka,waliotoka chadema tufanye kazi pamoja ya kuelimisha umma,ili wakati wa uchaguzi mkuu vyama vya upinzani tushike majimbo yote na si kubomoana wenyewe” alianisha Kisala.
 
Katibu wa Chadema wa hapa Shaban Madede aliwataka wakazi wa hapo watumie fursa kwa kuchukua  fomu za  chama hicho kwa  kuomba  nafasi ya kada mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya kitongozi hadi taifa kwa maslai ya kukijenga chama ili kufanikisha ndoto za kuingia ikulu mwakani.
 
Mkurugenzi  wa  Mipango Taifa  Benson  Kigaila alisema chadema taifa  inathamini nguvu za wakazi wa kigoma kwa kujitolea mali na jasho lao katika kukiimarisha chama tangu kuanzishwa kwake ndio maana inatoa nafasi nyingi  kwa wazawa wa hapo kwenye safu ya uongozi taifa na kuwasihi wanachama wazingatie maadili na falsafa ya katiba yao.
 
Pia ,imependekeza kuwa suala la kujadili rasimu ya katiba ifutwe kwa sasa ili fedha mtambukwa zisaidie huhudumia  jamii na kushawishi wananchi ifikapo 2015 wakipe kura chadema ili ishike dola na rasimu ya katiba ifanyike katika mfumo wa utawala wao.
 
Jamboleo liliwahoji  Katibu mwenezi  wilaya ACT wa hapa Anzoluni Kibela    na Katibu wa NRA Taifa Hamis Kiswaga ni kweli wapo tayari kushirikiana kukiondoa madarakani ccm 2015 na kuacha kudoboana majukwaani  kwa nyakati tofauti walisema  ni ndoto  kwa vyama hivyo ,kutokana na sera,itikadi ,utashi na ubinafsi uliopo miongoni mwa  viongozi wa vyama vilivyopo.
 
Walisema baadhi ya viongozi katika vyama wanautashi binafsi na kushawishi jambo Fulani kwa wakati maalum na linapokuja suala la umoja,mshikamano wa kusimika mgombea mmoja katika kiti cha urais ili kukiondoa ccm madarakani huibuka hisia za utashi na  ubinafsi kwa kusalitiana hatimaye ccm inaendelea kuhodhi madaraka  na kushauri wasafiane nia na uwazi wa malengo ili kutimiza hilo.
 
Kwa upande wa Katibu mwenezi CCM wa hapa Kalembe Masudi alisema vyama vya upinzani hawana dhati ya umoja,mshikamano ,kutokana na kushindwa kuwa  na uwazi wa uwajibikaji kwa wanachama wake kwa mujibu wa katiba zao na kudai  ccm itaendela kutawala kutokana na vyama hivyo kuwa na umoja wa mashaka kwa kutawaliwa na ubinafsi na si tija kwa wananchi.

Thursday, August 14, 2014

RAIS KIKWETE AFUNGUA MKUTANO WA KWANZA WA DIASPORA JIJINI DAR ES SALAAM LEO

di1
di3
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua tovuti rasmi ya Diaspora wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Diaspora katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo Agosti 14, 2014.
Pamoja naye ni Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda, Mwenyekiti wa Taasisi ya Diaspora Bw. Emmanuel Mwachullah (wa pili kulia), Mwana-Diaspora Dennis Londa (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Diaspora Bi. Rose Jairo

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA TAA YAKABIDHI MADAWATI 100 SHULE YA MSINGI YOMBO

3a
6a
Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya Ndege Tanzania TAA Bw. Suleiman Suleiman akimkabidhi Abdallah Ali Mmoja wa wanafunzi hao ambaye ni kiranja huku Mwalimu Mkuu Bi. Christina Kasyupa akishuhudia wa pili kutoka kushoto ni Celina Dismas Dada wa shule.
7a
Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya Ndege Tanzania TAA Bw. Suleiman Suleiman ,Abdallah Ali Mmoja wa wanafunzi hao ambaye ni kiranja na Celina Dismas Dada wa shule wakiwa wamekaa kwenye dawati mara baada ya makabidhiano huku uongozi wa shule hiyo ukishuhudia tukio hilo.
a1
Kwaya ya shule hiyo ikitoa burudani
a4
Wanafuzi wakicheza ngoma.
…………………………………………………………………………………
Dotto Mwaibale
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imetoa msaada wa madawati 100 kwa Shule ya Msingi ya Yombo iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam   ili kukabiliana na changangamo ya madawati shuleni hapo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi madawati hayo Dar es Salaam leo asubuhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Suleimkan Said Suleiman alisema msaada huo ni utekelezaji wa ahadi ya TAA kwa shule hiyo walioitoa mwaka jana.

“Kazi hii tunayoifanya ni kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa na kudumisha ujirani mwema  uliopo kati ya shule yenu na Kiwanja cha chetu cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA)” alisema Suleiman.

Alisema mwaja jana TAA ilitoa ahadi kwa shule hiyo ya kuwapa sh.milioni 10 ili ziwezekusaidia kupunguza tatizo la madawati ahadi ambayo wameitimiza jana kwa kutoa madawati hayo yenye thamani ya sh.milioni 10.

Suleiman alisema  msaada huo utakuwa kwa kamati ya shule hiyo na kuongeza jitihada za kuboresha zaidiufaulu kwa shule hiyo na wanafunzi kuhudhuria shuleni bila ya kukosa kwa faaida yao na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Suleiman alitumia fursa hiyo kuuomba uongozi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi hao kuyatunza madawati ili yaweze kusaidia na vizazi vingine.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Christina Kasyupa aliishukuru TAA kwa msaada huo kwa shule hiyo na kuwa wameupata kwa wakati muafaka kutokana na changamoto waliyokuwa nayo ya ukosefu wa madawati.

Shule ya Msingi ya Yombo ilianzishwa mwaka 1962 na imefanikiwa kufaulisha wanafunzi kwa asilimia 85 kwenda sekondari mwaka2013 na kupata cheti cha ugaguzi daraja A  na sasa ipo katika Mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu.

MH. LOWASSA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA BALOZI WA JAPAN NCHINI

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akisalimiana na Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada wakati alipo mtembelea ofisini kwake Jijini Dar es Salaam na kufanya nae mazungumzo.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada ofisini kwake,Mwenge jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada akifafanua jambo wakati wa Mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa ofisini kwake,Mwenge jijini Dar es Salaam leo.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa (kushoto) akimtambulisha Mbunge wa viti maalum CCM mkoa wa Arusha, Mh. Namelock Sokoine kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada pamoja na Ujumbe wake alioambatana nao.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akielezea jambo kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada na ujumbe wake alioambatana nao wakati wa kikao chao kilichofanyika leo ofisini kwake Mwenge,jijini Dar es saalam.Kulia ni Mbunge wa viti maalum CCM mkoa wa Arusha, Mh. Namelock Sokoine.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa (kushoto) na Mbunge wa viti maalum CCM mkoa wa Arusha, Mh. Namelock Sokoine (kulia) wakimsikiliza Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada (wa pili kushoto) wakati alipokuwa akifafanua jambo kuhusiana na namna Ubalozi huo utakavyoweza kufanisha Mradi wa Ujenzi wa Shule na Hospitali katika Wilaya ya Monduli.Wa pili kulia ni Katibu wa Balozi wa Japan,Bw. Sato Firgt.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akijadiliana jambo na Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada mara baada ya kufanya nae mazungumzo ofisini kwake Mwenge,Jijini Dar es salaam leo.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiagana na Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada

KIGOMA WAANZISHA BENKI MAALUM YA MATOFALI,NI AGIZO LA RAIS KIKWETE


Na Magreth Magosso,Kigoma
 
IMEELEZWA kuwa,Mkoa wa kigoma umefanikiwa kutimiza agizo la Rais Jakaya Kikwete juu ya kuanzishwa kwa Benki maalum ya matofali kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali katika sekta ya elimu,Afya na Ulinzi kwa lengo la kuboresha huduma hizo.
 
Tamko hilo limefanikiwa kwa asilimia 65 ya nguvu kazi ya wananchi wa wilaya sita ya Kigoma,Kakonko,Buhigwe,Uvinza,Kasulu na Kibondo kwa kuweza kuwa na matanuri ya matofali yapatayo 70 sawa na matofali  milioni tatu,ambapo ifikapo mwishoni mwa mwka huu watakuwa na matofali milioni 5 .
 
Wakizungumza kwa nyakati Tofauti baadhi ya wakazi wa mkoa huo Tumain Fredrick na Juma Hassan  walisema wanachi wapo tayari kutoa nguvu,akili na mali zao katika shuguli za maendeleo ya taifa lao kwa maslai ya kizazi cha leo na siku za usoni kwa kufuata taratibu husika na kuwaasa  viongozi wasimamie kwa dhati ili kufanikisha malengo mtambukwa.
 
 Kwa upande wa mwanafunzi wa shule ya sekondari Manyovu  Juma Nyamgenda alisema ujenzi wa maabara ukifanikiwa katika shule zote itasaidia ufaulu wa masomo michepuo  ya sayansi ambapo  watajifunza kwa vitendo , pia uwepo wa mabweni  ni usalama kwa kutokubughudhiwa na kazi za majumbani na  mimba kwa  wanafunzi wa kike na  kuisihi serikali na jamii watimize  ili  ndoto zao zitimie.
 
Akizindua matanuri hayo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Lt.mstaafu Issa Machibya alisema mradi huo ni moja ya kupunguza changamoto mbalimbali katika jamii husika,hususani ujenzi wa maabara,mabweni,nyumba za watumishi idara ya ulinzi,wauguzi na walimu.
 
 
Machibya aliongeza kwa kubainisha kuwa,viongozi wakishirikiana na wananchi katika agizo hilo ni moja ya kuokoa wanafunzi na matokeoa mabovu ya mtihani wa taifa sanjari na mimba za utotoni kwa wasichana wanaosoma shule za kutwa ambapo ujenzi wa mabweni ni tija kwao kuondokana na vishawishi vya uraiani.
 
 
Aidha  Mpango wa Benki ya Tofali umefikia awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza ulikuwa ni mandalizi ya ufyatuaji wa matofali ambapo juzi ulizinduliwa rasmi na mkuu wa mkoa huo katika kijiji cha Mwayaya wilaya ya buhigwe ambapo kupitia wilaya zake sita wamefanikisha agizo la Jakaya Kikwete kwa maslai ya umma  na kuongeza ufanisi wa huduma kwa jamii husika.

MKUTANO WA UJIRANI MWEMA KATI YA BURUNDI NA TANZANIA WAFANYIKA KIGOMA,WAZUNGUMZIA MAHUSIANO YA KIULINZI,UCHUMI NA BIASHARA


 Na Jacob Ruvilo-Kigoma
VIONGOZI wa serikali za mikoa ya mpakani mwa Burundi na Tanzania wasema mahusiano mema ya nchi hizo kiulinzi uchumi na biashara ni moja ya  nguzo muhimu kulinda amani na utulivu baina yq nchi hizo

hayo yamesemwa na wakuu wa mikoa ya Luyigi nchini Burundi na Kigoma nchini Tanzania wakati wa  mkutano maalumu wa ujirani mwema unaofanyika Alhamisi hii katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kigoma Tanzania


Mkuu wa mkoa wa Luyigi nchini Burundi ambaye ni mkuu wa msafara huo Bw Nshimilimana Siriyako ameshauri Tanzania kuboresha miundombinu ya Reli ya kati na barabara kwakuwa Burundi inategemea bandari za Dar na kigoma kibiashara.

aidha mkuu wa mkoa wa kigoma luten kanali mstaafu Issa Machibya amesisitiza umuhimu wa nchi hizi kuboresha ulinzi wa mipaka kupunguza uwezekano wa mwingiliano wa waharifu na wahamiaji Haramu ambao mara zote wamekuwa wahusika wakuu wa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha kali za kivita

Hata hivyo mwakilishi wa Burundi katika ujumbe huo wa kamati ya ulinzi na usalama kwa mikoa hiyo Bw Nshimirimmana  ameipongeza Tanzania nakuhimiza kuendeleza  oparesheni ondoa wahamiaji haramu nakwamba  ilifanya wakimbizi haramu kurejea nchini kwao na salsa wanajenga nchi yao kimaendeleo.

AFARIKI BAADA YA KUTIBIWA NA DAKTARI FEKI SINGIDA


DSC00179111

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela.

Na Nathaniel Limu
MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Iyumbu tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,Jubulu Mahende,amefariki dunia muda mfupi baada ya kupewa matibabu na mtu anayedaiwa kuwa ni daktari feki.

Imedaiwa kuwa Jubulu aliyekuwa akisumbuliwa na kifua, kiuno na mgongo alizidishiwa dawa kitendo kilichopelekea hali yake kuwa mbaya zaidi.

Daktari huyo ambaye amekiri hana cheti cha aina yo yote kutoka vyuo vya afya,Prospa Simson,baada ya kubaini hali ya mteja wake inakuwa mbaya,alimpa chupa tisa za maji,ili kuokoa maisha yake,lakini hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda.Pia alipatiwa vidonge sita ambavyo hata hivyo havijafahamika vilikuwa vinatibu maradhi gani.

Imedaiwa kuwa baada ya muda mfupi,Jubulu alipoteza maisha yake katika sebule ya nyumba ya mganga feki, Simson.

Kaimu  mganga mkuu wa wilaya ya Ikungi, Dk.Philip Kitundu alisema tukio hilo lilitokea Agosti 10 mwaka huu saa nne asubuhi kwenye vyumba maalumu vilivyotengwa na Simson kwa ajili ya kutolea huduma mbali mbali za matibabu.

“Tulipata taarifa ya tukio na agosti11mwaka  huu, tulienda kukagua duka la dawa ambalo lilisadikika lilitibu Jubulu ambaye alifia pale pale dukani”alifafanua.

Akifafanua zaidi,alisema walipolikagua duka hilo,waligundua kuwa Simon hakuwa na leseni kutoka TFDA ya kumruhusu kufanya biashara ya kuuza dawa kwa ajili ya binadamu.Pia yeye mwenyewe Simon,alikiri kuwa hakuwa na cheti  cha chuo chochote alichosomea utaalamu huo.

“Hata tulipopekuwa pekua dukani tulikuta madawa ambayo hayaruhusiwi kabisa kwenye maduka ya dawa muhimu,tulikuta madawa ya sindano,madawa ya vidonda,alikuwa anafunga vidonda,analaza,anatoa huduma za kujifungua kwa akina mama wajawazito”alisema Dk.Kitundu.

Aliongeza kwamba katika ukaguzi huo walikuta pia dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi. Tukio hilo la watu kupoteza maisha yao ni la tatu kutokea kwa watu waliopatiwa matibabu katika duka hilo isipokuwa matukio mawili yalitokea nje ya duka hilo.

 Kwa upande wake daktari huyo bandia,Dk.Prospa Simson licha ya kukiri kumpokea mgonjwa huyo akiwa na hali mbaya na kwamba baada ya kuchukua historia yake aligundua kuwa alikuwa akisumbuliwa na kifua na kwamba kabla ya kupelekwa kwake, alianza matibabau kwa waganga wa tiba asilia.

Kwa upande wake mtoto wa marehemu, Jilala Jibulu, alisema siku ya tukio asubuhi alikwenda kumsalimia baba yake na kumkuta akiwa na hali mbaya na ndipo alipoamua kumpeleka kwenye duka hilo la madawa,na muda mfupi alifariki akipatiwa matibabu.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,SACP Geofrey Kamwela,amekiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kwa sasa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama muuza duka hilo la madawa, ndiye alikuwa akimtibu au alienda dukani hapo kununua dawa alizoandikiwa na daktari mwingine.

MABWENI YA SHULE YA SEKONDARI YA MIVUMONI ILIOPO KWENYE MSIKITI WA MTAMBANI KINONDONI YATEKETEA KWA MOTO

DSCF8468
Moto Mkubwa ukiendelea kuwaka katika eneo la juu la Jengo la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Mivumoni (Mivumoni Islamic Seminary) iliyopo ndani ya Msikiti wa Mtambani,Kinondoni B Jijini Dar es Salaam jana.
Eneo hilo ambalo lilikuwa likitumika kama Mabweni ya Wanafunzi wa Shule hiyo,Maabara na Ofisi za Walimu limeteketea kabisa kiasi kwamba hakuna kitu chochote kilichoweza kuokolewa.
Jitihada za kuuzima moto huo zimekuwa zikiendelea hadi hivi sasa,huku sehemu ya Waumini wa Kiislam wakijitokeza kwa wingi kusaidia juhudi hizo za kuuzima moto huo zilizokuwa zikiendesha na Kampuni ya Kuzima moto ya Ultimate,japo baadae gari hilo liliisha maji,hali iliyowapelekea Waumini hao kulijaza maji gari hilo kwa kurumia ndoo huku kazi ya Uzimaji moto huo ikiendelea.
Chanzo cha Moto huo,inadaiwa ni hitilafu ya Umeme iliyokuwepo kwenye Bweli la Wasichana Wanafunzi wa Shule hiyo.Hakuna mtu yeyote aliepoteza maisha wala kujeruhiwa katika tukio hilo.Picha zote na Othman Michuzi.Kwa hisani ya  http://issamichuzi.blogspot.com/
DSCF8475
 Moto mkubwa ukiendelea kuwaka kwenye eneo hilo.
DSCF8481
 Ulinzi mkali wa Polisi ulitawala katika eneo la Msikiti huo wa Mtambani kuhakikisha Usalama unakuwepo kwenye eneo hilo.
DSCF8497
 Baadhi ya Waumini wa Kiislam wakishirikiana kusombelea maji ili kuuzima moto huo. 
DSCF8736
Gari la Zima Moto mali ya Kampuni ya Ultimate Security likijazwa maji kwa ndoo ili kuendelea na zoezi la uzimaji w amoto huo. 
DSCF8746
  Likafika na gari hili kwa ajili ya kusaidia kuzima moto huo.

LHRC WASIKITISHA NA KITENDO CHA KUKATWA MKONO MLEMAVU WA NGOZI - KALIUWA

Mtoto mlemavu wa ngozi albino Pendo Sengerema(14)mkazi wa Kijiji cha Usinge wilayani Kaliuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo akiwa anapatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa kwa kukatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana ambao walivamia nyumbani kwao na kumkata mkono na hatimaye kutoweka nao kusikojulikana,Hali ya Pendo hivi sasa inaendelea vizuri. 
Maafisa kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC,Bw.Mkuta Masoli anayeshughulikia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na Wakili Bw.Regnald Martin ambao walifika kumpa pole mlemavu huyo Pendo aliyenusurika kuuawa baada ya kukatwa mkono.

Na Mwandishi wetu-Urambo.
Mtoto Pendo Sengerema(14)mkazi wa Kijiji cha Usinge wilayani Kaliuwa ambaye kwasasa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo akipatiwa matibabu kufuatia kujeruhiwa kwa kukatwa mkono na watu  wasiojulikana na kisha kutoweka nao.

Pendo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Usinge hali yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibau katika hospitali ya wilaya ya Urambo.

Akizungumzia tukio hilo kwa kutumia lugha ya kabila la Wasukuma,Pendo ambaye kwasasa yupo katika uangalizi mkali wa Jeshi la Polisi katika Wodi maalumu alisema watu watatu ambaye mmoja tayari amemfahamu walifika nyumbani kwao majira ya saa tatu usiku na kubisha hodi ambapo waliingia ndani na kumuangusha chini kisha kumkata mkono na kuondoka nao mbio.

"Sisi tulikuwa ndani tunakula chakula na mama,walipoingia tu mmoja akaniangusha chini mwingine akanikata na upanga huku akinikataza kupiga kelele,...alinikata mara mbili tu akauchukua mkono wangu akakimbia,mimi nilikuwa nimekaa chini ninawaangali tu bila kupiga kelele"alisema Pendo 

Kwamujibu wa Pendo watu hao baada ya kutekeleza unyama huo walikimbia ndipo wakaanza kupiga mayowe kwa lengo la kuomba msaada.

"Mama yangu ni kipofu hakuona walivyonikata isipokuwa alikuwa akisikia wakati wananiambia nisipige kelele ingawa nilikuwa nasikia maumivu makali sana"aliendelea kueleza huku akiweka wazi kuwa katika watu aliowaona mmoja alimtambua kabisa.

Maafisa  wawili kutoka Kituo cha Sheria na haki za binadamu LHRC Bw.Mkuta Masoli anayehudumu  dawati linaloshughulikia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na Wakili wa Kituo hicho Mwanasheria Reginald Martin walifika katika hospitali ya wilaya ya Urambo kumjulia hali mtoto huyo Pendo na kupata maelezo yake kuhusu mkasa huo.

Katika tamko la LHRC lililotolewa na Bw.Masoli alieleza kuwa LHRC imelaani vikali unyama huo na kuviomba vyombo vya dola kushirikiana katika kukabiliana na wimbi la mauaji ya Walemavu wa ngozi albino ambayo yameanza kujitokeza tena kwa siku za hivi karibuni.

"Kitendo hiki ni cha kinyama ni vema tushirikiane katika kukomesha ukatili wa aina hii ni wazi kwamba Walemavu wa ngozi ni binadamu wa kawaida  na wanahaki kama walivyowengine,taifa linaingia katika kashfa ya ukiukwaji wa haki za binadamu"alisema Masoli huku akiitaka jamii kuvisaidia vyombo vya dola katika kuwafichua wanaofanya uharamia huo kwa imani za kishirikina 

Hata hivyo bado jamii mkoani Tabora inahitaji elimu kuhusu haki za binadamu kutokana na ukweli kwamba matukio ya mauaji yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara yakiwemo ya watu wenye ulemavu wa ngozi albino huku jamii ya vikongwe nayo ikiendelea kuwa katika mazingira hatarishi ya kuuawa kwa imani hizo za kishirikina. 

Wednesday, August 13, 2014

KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA NCHINI AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA KAMPUNI YA EQUATOR AUTOMECH LEO JIJINI DAR ES SALAAM

image
image_1
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Equator Automech, Robert Ndege(wa kwanza kushoto) akielezea namna Kampuni yake itakavyoshrikiana na Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Magereza katika miradi mbalimbali ya Uzalishaji ikiwemo ya Kilimo(katikati) ni Mkurugenzi Mshauri wa Kampuni hiyo, Ahmed Bakari akifuatilia mazungumzo hayo.
photo
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakifuatilia mazungumzo ya namna Kampuni ya Equator Automech itakavyoshrikiana na Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Magereza katika miradi yake ya Kilimo. Mazungumzo hayo yamefanyika leo Agosti 13, 2014 Jijini Dar es Salaam(wa kwanza kulia) ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa pili kulia) ni Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza, Gaston Sanga(katikati) ni Mkuu wa Kitengo cha Kilimo na Mifugo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mlasani Kimaro(wa kwanza kushoto) ni Mthibiti wa Fedha wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Gideon Nkana(wa pili kushoto) ni Mwanasheria wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Issack Kangura(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza).

WANAFUNZI WATUMIA MIFUKO YA RAMBO KUJISAIDIA-KIGOMA

 
Na Magreth Magosso,Kigoma


WANAFUNZI wa  Shule ya Msingi Airport  iliyopo wilaya ya Kigoma   Manispaa  ya Kigoma Ujiji, wanadaiwa kutumia mifuko ya Rambo kujisaidia haja zao ,baada ya kukosa choo  zaidi ya miaka miwili,  ili  hali  uongozi husika  wanalifumbia  macho changamoto hiyo.


Pia shule hiyo  inakabiliwa na adha ya ukosefu wa maji sambamba na madawati 600 ,ili kukidhi hitaji la wanafunzi wapatao 1408 pamoja na  vyumba vya madarasa ,ambapo kila darasa lina wanafunzi  173, hali inayochangia uelewa finyu kwa wanafunzi husika.


Jamboleo lilipiga hodi katika shule hiyo,baada ya kubaini Diwani wa kata ya Mwanga mjini Moses  Bilantanye Kuahidi kupeleka  Mifuko ya Rambo shuleni hapo,ili kuokoa jahazi la vifo kwa wahanga hao kutokana na choo chao kutitia.


shule ilitaka kufungwa kitambo lakini wamezibaziba  tundu mbili tu tena kwa shida ,wanafunzi hutumia sasa mimi napeleka mifuko  wiki ijayo ,ili wajisaidie humo,” alianisha Bilantanye.


Kwa upande wa Mwalimu Mkuu Yustus Fundi alipohojiwa  mifuko ya Rambo kutumika  kwa wanafunzi hao ili kujisitiri na maumbile  ya mwili alisema ni kweli hali inayochangiwa na ubovu wa matundu saba ya choo  sambamba na ukosefu wa maji.


Alisema aliyekuwa mkurugenzi wa awali Alfred  Luanda na ofisa elimu Shomari Bane walifika katika shule hiyo na kutaka ujenzi ufanyike ndani ya wiki moja kuokoa janga hilo, kabla ya utekelezaji  walihamishwa  mkoani hapo.


Mratibu  elimu kata ya husika  Edes  Ibrahim  na  kaimu mwalimu mkuu Deogratius Rulakuze  kwa nyakati tofauti walisema Novemba,23,2012 walipeleka barua kwa wakuu wa idara na hakuna jipya zaidi ya kila mwanafunzi anajua njia ya kujisitiri kwa namna yake.


Walisema  walijaribu kuomba msada kwa BayPort na  mkuu wa uwanja wa ndege mkoani hapo lakini jitihada za kuwapatia  hitaji hilo hakuna  zaidi ya ahadi ya maneno .


Aidha Mtandao huu umeshuhudia baadhi ya wanafunzi Matilda Zephine na Neema Samweli wakinyata kwa tahadhari kuingia katika choo hicho ambacho wakati wowote kitazama chini kutokana na shimo kubwa lililotoboa  tundu za choo hicho.


Walipoulizwa sababu ya kunyata wakati wa kuingia chooni walidai wanaogopa kutumbukiwa na kukiri hali hiyo inashawishi baadhi kuwa watoro hasa wakishikwa na haja wakienda nyumbani nadra kurudi darasani kuendelea na vipindi vingine.


Akijibia hilo  Mwenyekiti  kamati ya uchumi  afya na elimu  manispaa hiyo Moshi Said  alisema  changamoto ya vyoo katika shule za manispaa kigoma ujiji ni makubwa hivyo  katika kikao cha Octoba mwaka huu 2014  watatenga   bajeti ya  kujenga matundu ya vyoo 200 kwenye shule  zote zenye changamoto hiyo .

Tuesday, August 12, 2014

BBC YAZINDUA STUDIO ZAKE NCHINI,KIPINDI CHA AMKA NA BBC KURUKA MOJA KWA MOJA KUTOKA JIJINI DAR-ES-SALAAM


Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu,Bi. Nikki Clarke akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,katika Jengo lao lililopo Mikocheni.Kushoto ni Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh (wa tatu kulia) akiwapatia maelekezo Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Dkt. Salim Ahmed Salim na Mwenyekiti wa CUF,Prof. Ibrahim Lipumba ya namna Idhaa hiyo inavyoandaa vipindi yake na inavyopeleka hewani wakati wa hafla ya Uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC,jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu,Bi. Nikki Clarke akibadilishana mawazo na aliewahi kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Tiddo Mhando wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,Hassan Mhelela (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo pamoja na kuitambulisha timu yake.
Baadhi ya Wageni waalikwa wakiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wakuu wa BBC waliokuwepo kwenye hafla hiyo,jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa zamani wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Tiddo Mhando (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC,Bw. Ali Saleh pamoja na Mtangazaji Sussani Mongi.
Taswira za Studio za BBC jijini Dar.
Chumba cha Habari cha BBC jijini Dar.
Wadau Salim Kikeke na Nicolas wakipitia habari kabla ya kuipeleka hewani.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
BBC Idhaa ya Ulimwengu, imezindua ofisi zake jijini Dar es Salaam. Ofisi za Dar es Salaam zina studio ambazo zinatumika kuandaa matangazo maarufu ya redio ya asubuhi, Amka na BBC, na pia kuendesha tovuti ya bbcswahili.com.
 
Katika kuadhimisha uzinduzi huo, vipindi vingine viwili vya BBC Idhaa ya Kiswahili, Dira ya Dunia ya redio na ya TV vitaandaliwa kutoka Dar es Salaam katika siku hiyo ya Jumatatu Agosti 11.
 
Ufunguzi wa ofisi za Dar es Salaam ni matokeo ya mikakati ya BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuhamisha uandaaji wa vipindi vya redio na tovuti kutoka London kwenda Afrika Mashariki.
 
Ofisi mpya ina vifaa vya kisasa vinavyoweza kutayarisha vipindi vya redio, TV na huduma za habari kwa njia ya simu za mkononi. Amka na BBC, kipindi cha nusu saa ambacho hutangazwa Jumatatu hadi Ijumaa humulika matukio na taarifa zitakazojiri katika siku, sasa kitaandaliwa Dar es Salaam na watayarishaji na watangazaji 15.
 
Ofisi mpya pia zina watayarishaji wanaoandaa taarifa mbalimbali za kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya vipindi vya TV vya Focus on Africa na Dira ya Dunia. Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu Nikki Clarke amesema:
 
 “Uzinduzi wa ofisi zetu za Dar es Salaam ni hatua kubwa katika safari yetu iliyoanza muda mrefu kidogo, katika kuwapa wanachotaka wasikilizaji katika nchi zinazozungumza Kiswahili, na ambao husikiliza BBC wanapotaka kupata taarifa wanazoziamini na zenye uhakika. Takriban watu milioni 12.4 – ambao ni kama nusu ya idadi ya watu wazima nchini Tanzania, husikiliza matangazo ya redio ya BBC kila wiki.
 
Na sasa moja ya kipindi maarufu cha BBC, Amka na BBC, kimekuja karibu zaidi na wasikilizaji.” Ofisi ya Dar es Salaam, ina studio mbili za redio ambazo zinaweza kutumika na hadi watu sita kwa wakati mmoja, na hivyo ni muafaka kabisa kwa kipindi kichangamfu cha Amka na BBC kwa ajili ya mijadala na mahojiano ya kuvutia.
 
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh anasema : “Ofisi mpya zinatoa nafasi bora kabisa kwa watayarishaji wa BBC nchini Tanzania kuimarisha ukusanyaji wa habari na kutoa taarifa kutoka katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
 
Amka na BBC itakuwa na uwezo mkubwa zaidi kutoa taarifa na habari mchanganyiko, za Afrika Mashariki na pia za dunia, pamoja na mahojiano ya moja kwa moja na watu mbalimbali, lakini pia makala na habari za kijamii.” Idhaa ya Kiswahili ya BBC imekuwa kitovu cha hatua ya BBC Idhaa ya Ulimwengu ya kuimarisha kuwepo kwake katika sekta ya habari barani Afrika.
 
Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Nairobi mwaka 1998, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilikuwa shirika la kwanza la habari la kimataifa kuwa na kituo cha uandaaji habari barani Afrika. Mwaka 2006 Amka na BBC ilihamishwa kutoka London kwenda Nairobi, na BBC Idhaa ya Ulimwengu, kwa mara nyingine tena ikawa shirika la kwanza la kimataifa la habari kuandaa na kutangaza vipindi kutoka barani Afrika. 
 
Katika hatua ya kuhamisha utayarisaji wa vipindi na taarifa za kwenye tovuti, kipindi maarufu cha jioni cha redio, Dira ya Dunia sasa kinatayarishwa Nairobi. Mwisho// Kwa taarifa zaidi wasiliana na afisa wa idara ya mawasiliano ya BBC Idhaa ya Ulimwengu – Lala Najafova, lala.najafova@bbc.co.uk.
 
Kwa wahariri: BBC Idhaa ya Ulimwengu ni shirika la utangazaji la kimataifa lenye idhaa nyingi za lugha mbalimbali zinazotoa huduma ya matangazo ya redio, TV, kwenye mtandao wa internet na pia simu za mkononi. BBC Idhaa ya Ulimwengu hutumia njia mbalimbali kuwafikia wasikilizaji wake wapatao milioni 191 duniani kote. BBC huwafikia watu milioni 265 duniani kote kila wiki kwa huduma zake kutoka BBC Idhaa ya Ulimwengu, BBC News TV na bbc.com.