Sheikh Sharifff Mikidadi akiwa ameshika nyama hiyo akimuonesha mwandishi wetu huko nyumbani kwake Magomeni jijini Dar-es-Salaam. |
Na Mwandishi wetu maalum.
Siku chache baada ya tukio la kugundulika kwa nyama ya ng'ombe iliyoandikwa kwa maandishi ya lugha ya kiarabu jina la Mwenyezimungu yaani ALLAH huko nyumbani kwao Sheikh Shariff Mikidadi eneo la kata ya Kiloleni Tabora mjini, tukio la aina hiyo limejitokeza tena huko nyumbani kwake eneo la Magomeni jijini Dar-es-Salaam na kusababisha mshangao mkubwa kwa watu walioshuhudia.
Kutokea kwa kipande hicho cha nyama ambacho kilitokana na nyama ambayo ilikwenda kununuliwa kwenye moja ya maduka ya nyama eneo la Magomeni kwa ajili ya kitoweo nyumbani kwa Sheikh Shariff,,maswali mengi yameendelea kujitokeza na kukosa majibu hata kufikia hatua kwa wengine kumwachia Mungu.
Maelezo ya awali yaliyotolewa na mmoja wa kaka wa Sheikh Shariff anayefahamika kwa jina la Abdillah Mikidadi alithibitisha kuwa mara baada ya nyama hiyo kufikishwa nyumbani kwa Sheikh Shariff taratibu za mapishi ziliendelea na baada ya kuiva kipande kimoja kilionekana kikiwa kimeandikwa maandishi hayo ya kiarabu kwa maana ya ALLAH.
Alisema watu mbalimbali wakiwemo baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu wamefika nyumbani kwa Sheikh Shariff kushuhudia kipande cha nyama hiyo na huku wengine wakizidi kukumbwa na mshangao.
MAELEZO YA SHEIKH SHARIFF MWENYEWE.
Alipohojiwa kuhusu kuwepo kwa tukio hilo ambalo pia limejitokeza katika familia yake tena kwa mara ya pili mfululizo,Sheikh Shariff Mikidadi ambaye pia ni kijana mwenye historia kubwa kutokana na kuzaliwa kwake katika mazingira ya miujiza,alisema kuwepo kwa nyama hiyo ni tukio linalodhihirisha uwepo wa Mwenyezimungu na kwamba hakuna haja ya kuleta fikra potofu juu ya hilo.
Sheikh Shariff aliendelea kusema kuwa jambo la msingi kwa waumini wa dini ya kiislamu ni kuimarisha imani zao kwa kufanya ibada ipasavyo na kumtukuza Mola wao na si vinginevyo.
''Mimi binafsi katika hili naamini kuwa ALLAH anadhihirisha uwepo wake kwetu sisi na kwamba kuna haja kwa waislamu kushikamana katika dini yao na kwamwe tusifarikiane na kusababisha madhara kwetu sisi kama waislamu pia hata na kwa wenzetu wa dini nyingine na hata wale wasiokuwa na dini''alisema Sheikh Shariff
Aidha katika siku za hivi karibuni tukio la kugundulika kwa nyama ya aina hiyo lilijitokeza nyumbani kwao Sheikh Shariff huko kata ya Kiloleni Tabora mjini ambapo tukio hilo liliripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari na kushangaza idadi kubwa ya watu.
No comments:
Post a Comment