Pages

KAPIPI TV

Showing posts with label ELIMU. Show all posts
Showing posts with label ELIMU. Show all posts

Monday, January 23, 2012

WANAFUNZI WA KIKE WAFAIDIKA MBOLA

WANAFUNZI WA KIKE WAFAIDIKA MBOLA
 WAFADHILIWA MASOMO KWA ZAIDI YA SHILINGI MIL.46
 Wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule mbalimbali zilizopo kwenye eneo la mradi wa vijiji vya Milenia Mbola,wanafunzi hawa kwasasa  masomo yao wanafadhiliwa na Mradi  huo.Picha ya kwanza wanafunzi wakiwa na mkuu  wa  wilaya ya Uyui Bw.Stanley Kolimba,viongozi wa mradi na diwani wa kata ya Ilolangulu.


 Wanafunzi wa kidato cha pili  Shule ya Sekondari ya Lolangulu wanaofadhiliwa na Mradi wa Milenia Mbola,pichani  wakiwa na mkuu  wa wilaya ya  Uyui  Bw.Stanley Kolimba pamoja na viongozi wa  mradi.
 Mkuu  wa  wilaya  ya  Uyui  Bw.Stanley Kolimba akizungumza  wakati wa uzinduzi wa  Program ya Ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike kwa Shule  za sekondari zilizopo eneo la Mradi  wa Milenia Mbola. 

 Mratibu wa vijiji  vya  Milenia Mbola Dr.Gerson Nyadzi akitambulisha  wanafunzi wa kike waliochaguliwa kufadhiliwa na mradi katika program ya kuwasaidia wanafunzi.hao kuwaendeleza kielimu.
 Mtafiti  wa masuala  ya  kisayansi  Mradi wa vijiji vya Milenia Afrika na  Mkurugenzi  Taasisi ya  afya  Chuo  kikuu  cha  Columbia  Marekani,Prof.Cherly Palm akipanda mti nje ya jengo la Maendeleo ya jamii lililopo Ilolangulu wilayani Uyui.

Jumla  ya  wanafunzi  wasichana  wapatao  26 waliofaulu mtihani  wa  darasa  la  saba  kujiunga  na masomo  ya  kidato  cha  kwanza  mwaka  huu  katika  shule  mbalimbali  zilizopo  eneo  la  mradi  wa Milenia  Mbola  wamepata  ufadhili  wa  masomo  kwa  gharama  ya zaidi ya  shilingi  mil.46.

Mpango  huo  ambao  umelenga  kuwawezesha  wanafunzi  wasichana  ambao  unaratibiwa  na  Mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola  MVP,umezinduliwa  rasmi  wiki  hii  katika  kata  ya  Ilolangulu  wilayani  Uyui  mkoani  Tabora.

Akizungumza  katika  hafla  fupi  ya  uzinduzi  wa  Mpango  huo  unaotajwa  kama  Girls connect to Learn,mratibu  na  mtafiti  wa  masuala  ya  kisayansi  wa  mradi  wa  Milenia  Mbola  Dr.Gerson  Nyadzi  alisema  katika  mpango  huo  unaofadhiliwa  na  watu  kutoka  mataifa  mbalimbali  ulimwenguni  kwa  mwaka  huu  kwa  wanafunzi  hao  wa  kike  26  kila  mmoja  atagharamiwa  kuwezeshwa  masomo  yake  kwa  kiasi  cha  shilingi  862,000/=

Aidha  alifafanua  kiwango  hicho  cha  fedha  pamoja  na  kuangalia  gharama  za  malipo  ya  ada  na  vifaa  vya  shule  lakini  kwa  mwaka  huu  umeenda  mbali  zaidi  kwa  wanafunzi  hao  kupatiwa  fedha  taslimu  shilingi  laki  moja  kwa  wale  ambao  wanaishi  katika  familia  zenye  uwezo  mdogo,posho  ya  sh.20,000 na  kupatiwa  baiskeli  kama  njia  ya  kumwezesha  mwanafunzi  kufika   shuleni.

Dr.Nyadzi  sambamba  na  hilo aliweka  bayana  kuwa  mpango  huo  pia  umeendelea  kuwawezesha  wanafunzi  waliopata  ufadhili  kwa  mwaka  jana  ambao  kwasasa  wapo  kidato  cha  pili  ambapo  kila  mwanafunzi  amepata ufadhili  wa kiasi  cha shilingi  490,000.

Akizindua  mpango  huo  wa  Girls connect to Learn,mkuu  wa  wilaya  ya  Uyui  Bw.Stanley  Kolimba  ameupongeza  Mradi  wa  MVP  kwa  kuanzisha  mpango  huo  ambao  utakidhi  mahitaji  ya  serikali  katika  kuwawezesha  wanafunzi  kielimu  huku  akibainisha  changamoto  inayoikabili  wilaya  hiyo  ya  kuwa  na idadi  kubwa  ya  wanafunzi  wakike  ambao  wanakosa  elimu  kutokana  na  matatizo  mengi  yakiwemo  ya  kutokuwa  na  uwezo  wa  kifedha  kwa  baadhi  ya  wazazi.

Bw.Kolimba  alitumia  fursa  hiyo  kuwataka  wazazi  na  walezi  wa  wanafunzi  hao waliohudhuria  katika  hafla  hiyo  fupi  kuunga  mkono  juhudi  za  wafadhili  na  kuhakikisha  wanawapa  malezi  bora  watoto  wao  ikiwa  ni  pamoja  na  kuwapatia  muda  wa  kusoma  badala  ya  kutumia  muda  mwingi  kuwatumikisha  kazi  za  nyumbani  hasa  kilimo.   

Kwa  upande  wake  Mkurugenzi  na  mtafiti  wa  kisayansi  wa  Mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Afrika  kutoka  Chuo  kikuu  cha  Columbia  cha  nchini  Marekani  ambaye  pia  ni  mmoja  kati  ya  wafadhili  wa  mpango  huo  Prof.Cherly  Palm,alisema  jamii  inapaswa  kuwekeza  kwa  kuwasaidia  wanafunzi  hasa  wakike  kwakuwa  kufanya  hivyo  ni  moja  ya  njia  itakayosaidia  kuikomboa  jamii  kuanzia  ngazi  ya  familia.

Alisema  familia  yake  kwa  kutambua  umuhimu  wa  kumsaidia  mwanafunzi  wa  kike  imeamua  kuchangia  katika  mpango  huo  ikiwa  ni  jitihada  za  kumpunguzia  unyonge  wa  umasikini  mwanafunzi  wa  kike.

Aidha  kwa  mujibu  wa  Mradi  wa  Milenia  Mbola   mpango  wa  kuwafadhili  wanafunzi  wanaofanya  vizuri  shuleni  umepangwa  kuwa  endelevu  kwa  kila  mwaka.                      

Friday, November 18, 2011

TABLE FOR TWO VIJIJI VYA MILENIA MBOLA


WATEMBELEA  SHULE  ZA  MSINGI
MRADI  WA  VIJIJI VYA  MILENIA  MBOLA 
Wafanyakazi  wa  Mradi wa  Vijiji  vya  Milenia  Mbola  na  wafadhili  wa  TABLE  FOR  TWO wakiwa  nje  ya ofisi  ya  MVP. 
TABLE  FOR  TWO watembelea  baadhi  ya  wakulima  wa kijiji  cha  Inonelwa kuangalia  mafanikio  katika  sekta  ya  kilimo.
 Wanafunzi  Shule  ya  Msingi  Ilolangulu wakinawa  mikono  na  kuosha  vyombo  kwa  ajili  ya  kuchukua  chakula  cha  mchana  kinachotolewa  shuleni  hapo.
TABLE  FOR  TWO.Alex Talpaert akisaidia  zoezi  la  ugawaji  chakula  cha  mchana  shule  ya  msingi  Ilolangulu wakati  walipotembelea shule  zilizopo eneo  la  mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola.
  TABLE  FOR  TWO.Tomoko Kobayashi akipata  chakula  cha  mchana  na  wanafunzi  wa  Shule  ya  Ilolangulu.
TABLE  FOR TWO.Aya Miyaguchi akipata  ugali  maharage na  mmoja  wa  wanafunzi  wa  darasa  la  pili.

Wananchi  wakipata  huduma  ya maji  safi  katika  moja  ya  visima  vilivyochimbwa  na  mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola  katika  kijiji  cha  Inonelwa.




TABLE  FOR  TWO  KUTEMBELEA  MRADI  WA  MILENIA  MBOLA.

TABORA.

Baadhi   ya  wafadhili  wa  Shirika  la kimataifa  la  Table  For  Two  linalojumuisha  wadau  kutoka  nchi  za  Japan,Marekani  na  China  wametembelea  mradi  wa  vijiji  vya  Millenia  Mbola  kuangalia  maendeleo  ya  mpango  wa  chakula  kwa  shule  za  msingi  zipatazo  kumi  na  saba  zilizopo  eneo  la  mradi  huo.

Wakiwa  katika  ziara  ya  siku  mbili  wafadhili  hao  ambao  lengo  lao  kubwa  lilikuwa  ni  kuangalia  mpango  huo  wa  chakula  kwa  shule  za  msingi,  katika   hatua  za  awali  walitembelea  Shule  za msingi  za  Ilolangulu,Madaha  na  Mbola  zilizopo  eneo  la  mradi  wa  vijiji  vya  Milenia.

Katika  Shule  ya  msingi  Ilolangulu  wafadhili  hao  ambao  watatu  wanatokea  nchini  Japan,mmoja  Marekani  na  mwingine  nchini  China  walifika  katika  shule  hiyo  majira  ya  saa  sita  hadi  saa  saba  mchana  muda  ambao  wanafunzi  walikuwa  wakiandaliwa  kupata  chakula  cha  mchana  na  hivyo  kupata  fursa  ya  kushudia  zoezi  la  zima  la  chakula  cha  mchana  kwa  wanafunzi  hao.

Akizungumza  na  kutolea  ufafanuzi  kwa  wafadhili  hao,mwalimu  mkuu  wa  shule  ya  Ilolangulu  Bi.Hawa  Mwamba  alisema  kwa  kiasi  kikubwa  mpango  huo  wa  chakula  shuleni  umesaidia  kwa  kiasi  kikubwa  na  hasa  kuongeza  mahudhurio  kwa  wanafunzi  kutoka  aslimia  45  hadi  asilimia  97.

Aliongeza  kwa  kusema  kuwa  hatua  hiyo  pia  imesaidia  usikivu  kwa  wanafunzi  wawapo  darasani  na  hata  kufikia  pia  matokeo  mazuri  kwa  ufaulu  kwa   wanafunzi  wa   darasa  la  saba  ikilinganishwa  na  hali  halisi  kabla  ya  kuanzishwa  kwa  mpango  huo  wa  chakula  shuleni.

Mwalimu  Hawa  aliwaeleza  wafadhili  hao  kuwa  mpango  huo  ni  wazo  lililotolewa  na  Mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola  katika  kufikia  Malengo  manane  ya  Milenia  na  hivyo  Mradi  umekuwa  ukichangia  na  huku  wazazi  pia  wakitakiwa  kuchangia  mpango  huo  wa  lishe  kwa  wanafunzi.

Hata  hivyo  wafadhili  hao  wakiongozwa  na  Bi.Tomoko  Kobayashi  kutoka  nchini  Japani,walionesha  kuridhishwa  kwao  na  utaratibu  wa  mpango  huo  ingawa  umekuwa  ukikabiliwa  na  changamoto  ya  upungufu  wa  vyombo  vya  kupikia,mishahara  kwa  ajili  ya  wapishi  na  sehemu  maalumu  ya  kulishia  chakula  hicho  kwa  wanafunzi.

Kwa  upande  wake  mratibu  wa  mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola  Dr.Gerson  Nyadzi  alisema  mpango  huo  wa  chakula  shuleni  ni moja  kati  ya hatua  za   kuboresha    elimu  katika  kutekeleza  malengo  manane  ya  millenia  kwa  kushirikisha  wakazi  wakiwemo  wazazi  wa  wanafunzi  kuchangia  gunia  moja  la  mahindi  unapofika  msimu  wa  mavuno  kwa  kila  mwaka.

Aidha  Dr.Nyadzi  akifafanua  zaidi  aliwaeleza  wafadhili  hao  kuwa  mradi  mbali  na  masuala  ya  elimu  pia  mafanikio  makubwa  yamejidhihirisha  kwenye  sekta  za  kilimo,afya  na  maji.

Kwa upande  wa  sekta  ya  afya  aliweka  bayana  kuwa  kiwango  cha  magojwa  ya  Malaria  kwa  wakazi  wa  vijiji  vya  millennia  Mbola  kimepungua  kwa  kiasi  kikubwa  hali  aliyodai  kuwa  imetokana  na  ugawaji  wa  vyandarua  vyenye  dawa  sambamba  na  elimu  juu  ya  matumizi  ya  vyandarua  hivyo.

Dr.Nyadzi  pia  alisema  vifo  vya  kinamama  wajawazito  na  watoto  chini  ya  umri  wa  miaka  mitano  vimepungua  kutokana  na  elimu  ya  kuwahimiza  kuhudhuria  katika  zahanati  zilizojengwa  na  mradi  huo   na  pengine  wajawazito  kujifungulia  hospitalini  huku  mradi  ukiwa  umeweka  gari  kwa  ajili  ya  wagonjwa  wanaohitajika  kupelekwa  hospitali  ya  mkoa   wa  Tabora.

Aidha  kwa  upande  wa  kilimo  Dr.Nyadzi  alizungumzia  mafanikio  yaliyopatikana  ni  pamoja  na  wakulima  kuongeza  mavuno  kutoka  wastani  wa  gunia  tano  za  mahindi  kwa  hekari  moja  ya  shamba   hadi  kufikia  mavuno  ya  magunia   35  kwa  hekari  moja  hali  iliyotokana  na  kuwapatia  pembejeo  na  elimu  ya  kilimo  cha  kisasa  na  chenye  kuleta  tija  kwa  mkulima.

Kuhusu  suala  la  maji  Dr.Nyadzi  alisema  mpango  wa  Mradi  ni  kuchimba  visima  na  kuwasogezea  karibu  wananchi  huduma  hiyo  ya  maji  jambo  ambalo  limekwisha  fanyika  karibu  maeneo  yote  ya  vijiji  vipatavyo  17  vinavyofadhiliwa  na   mradi  huo.
               

Wednesday, November 9, 2011

MGOMO CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA TABORA WAMALIZIKA

MGOMO  CHUO  CHA  UTUMISHI  WA  UMMA  TABORA WAMALIZIKA.
''MKURUGENZI  MKUU  AUNDA  TUME  KUCHUNGUZA  KAULI  ZA  WALIMU WA CHUO HICHO'' 
Wanachuo chuo  cha  Utumishi  wa  Umma  wakati  walipokuwa na  mgomo  wa kutoingia  darasani kushinikisha Uongozi  wa  Chuo  hicho kusikiliza  madai  yao.
Uongozi  wa  chuo  cha  utumishi  wa  umma.
Walimu  Chuo  cha  Utumishi  wa  Umma  tawi  la  Tabora  wakipata  elimu  zaidi  kuhusu  sheria  mpya  inayohusiana  na  vyuo  nchini  kusajiliwa  NACTE.
Wanachuo  Chuo  cha  Utumishi  wa  Umma  tawi  la  Tabora wakiendelea  na  masomo  baada  ya  kumalizika  kwa  mgomo.


Mkurugenzi  mkuu  Chuo  cha  Utumishi  wa  Umma  nchini  Bw.Said  Nassor  ameunda  tume  huru  kuchunguza  kauli  ya  baadhi  ya  walimu  walizozitoa  na  kusababisha  mgomo  kwa   wanachuo  wakati  wakidai  kueleweshwa  mabadiliko  ya   mfumo  juu  ya   utolewaji  wa  kozi  mbalimbali  kwa  ngazi  za  diploma.


Bw.Saidi  Nassor  amelazimika  kuunda  tume  hiyo kuchunguza baadhi  ya  kauli  za  viongozi ambazo  alidai  kuwa  zimekuwa  ni  sehemu  ya kuwachanganya wanachuo  na  kuona  kana  kwamba  chuo  hakina  nia  nzuri  na  wanachuo  hao.

Akifafanua  zaidi  Bw.Nassor alisema  chuo  tangu  kusajiliwa  kwake  na  Nacte  kwa  ajili  ya  kuboresha  mafunzo  tayari  kimelazimika  kufuata  taratibu  za  baraza  hilo  ikiwa  ni  pamoja  na  mfumo  wa  utoaji   wa  vyeti  kwa  kozi  mbali na  hasa  za  ngazi  ya  Diploma.

Aidha amesema  kufuatia  hali  hiyo  madai  ya  wanachuo yaliyokuwa  yakidai  kupatiwa  cheti cha Diploma  ya  miaka  miwili  ni  kinyume  na  utaratibu  wa  Nacte ambapo kwa  utaratibu wa baraza  hilo mwanachuo  anayetaka  kujiunga  na  chuo hicho akiwa  na  elimu  ya  kidato  cha  nne  atasoma  kozi  ya  utunzaji  kumbukumbu  na katibu muhtasi  Diploma  kwa  muda  wa  miaka  mitatu  wakati  wale  wa  elimu  ya  kidato  cha  sita  watasoma  kozi  hizo  kwa  Diploma  ya  miaka  miwili.

Hata  hivyo amekiri  kuwepo  kwa  madhaifu katika chuo  hicho  ambapo  baadhi  ya  walimu  wamejigeuza  kuwa  wasemaji  wakuu  hali  iliyosababisha  kuwayumbisha  wanachuo  waliokuwa  wakihitaji  ufafanuzi  wa  taratibu  hizo  na  hivyo  kujikuta  wakianzisha  mgomo wa  kutoingia  darasani.

''Hatuwezi  kulivumilia  hilo kwa hiyo  ndio  maana  tumeunda  tume  huru  na  ikibainika  kuhusika  kwa  mwalimu  yeyote  atalazimika  atoe  ufafanuzi kwa  maandishi  na  kisha  taratibu  za  kinidhamu  katika  utumishi  zitafuata''alisema  mkurugenzi  huyo.

Aidha  kwa  mujibu  wa  mkurugenzi  huyo  amesema  tume  hiyo  ya  watu  wanne  kutoka  nje  ya chuo  hicho imepewa  muda  wa  siku saba  kukamilisha  uchunguzi  na  baada  ya  matokeo  hatua za  kinidhamu  zitachukuliwa  ili  kuendelea  kulinda  heshima  ya  chuo  hicho  kilicho  chini  ya  ofisi  ya  Rais  menejimenti  ya  utumishi  wa  Umma.    


Katika  hatua  hiyohiyo  wanachuo  wameendelea  na masomo  na  kushiriki  shughuli  za  chuo  kama  kawaida.