Pages

KAPIPI TV

Monday, January 23, 2012

WANAFUNZI WA KIKE WAFAIDIKA MBOLA

WANAFUNZI WA KIKE WAFAIDIKA MBOLA
 WAFADHILIWA MASOMO KWA ZAIDI YA SHILINGI MIL.46
 Wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule mbalimbali zilizopo kwenye eneo la mradi wa vijiji vya Milenia Mbola,wanafunzi hawa kwasasa  masomo yao wanafadhiliwa na Mradi  huo.Picha ya kwanza wanafunzi wakiwa na mkuu  wa  wilaya ya Uyui Bw.Stanley Kolimba,viongozi wa mradi na diwani wa kata ya Ilolangulu.


 Wanafunzi wa kidato cha pili  Shule ya Sekondari ya Lolangulu wanaofadhiliwa na Mradi wa Milenia Mbola,pichani  wakiwa na mkuu  wa wilaya ya  Uyui  Bw.Stanley Kolimba pamoja na viongozi wa  mradi.
 Mkuu  wa  wilaya  ya  Uyui  Bw.Stanley Kolimba akizungumza  wakati wa uzinduzi wa  Program ya Ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike kwa Shule  za sekondari zilizopo eneo la Mradi  wa Milenia Mbola. 

 Mratibu wa vijiji  vya  Milenia Mbola Dr.Gerson Nyadzi akitambulisha  wanafunzi wa kike waliochaguliwa kufadhiliwa na mradi katika program ya kuwasaidia wanafunzi.hao kuwaendeleza kielimu.
 Mtafiti  wa masuala  ya  kisayansi  Mradi wa vijiji vya Milenia Afrika na  Mkurugenzi  Taasisi ya  afya  Chuo  kikuu  cha  Columbia  Marekani,Prof.Cherly Palm akipanda mti nje ya jengo la Maendeleo ya jamii lililopo Ilolangulu wilayani Uyui.

Jumla  ya  wanafunzi  wasichana  wapatao  26 waliofaulu mtihani  wa  darasa  la  saba  kujiunga  na masomo  ya  kidato  cha  kwanza  mwaka  huu  katika  shule  mbalimbali  zilizopo  eneo  la  mradi  wa Milenia  Mbola  wamepata  ufadhili  wa  masomo  kwa  gharama  ya zaidi ya  shilingi  mil.46.

Mpango  huo  ambao  umelenga  kuwawezesha  wanafunzi  wasichana  ambao  unaratibiwa  na  Mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Mbola  MVP,umezinduliwa  rasmi  wiki  hii  katika  kata  ya  Ilolangulu  wilayani  Uyui  mkoani  Tabora.

Akizungumza  katika  hafla  fupi  ya  uzinduzi  wa  Mpango  huo  unaotajwa  kama  Girls connect to Learn,mratibu  na  mtafiti  wa  masuala  ya  kisayansi  wa  mradi  wa  Milenia  Mbola  Dr.Gerson  Nyadzi  alisema  katika  mpango  huo  unaofadhiliwa  na  watu  kutoka  mataifa  mbalimbali  ulimwenguni  kwa  mwaka  huu  kwa  wanafunzi  hao  wa  kike  26  kila  mmoja  atagharamiwa  kuwezeshwa  masomo  yake  kwa  kiasi  cha  shilingi  862,000/=

Aidha  alifafanua  kiwango  hicho  cha  fedha  pamoja  na  kuangalia  gharama  za  malipo  ya  ada  na  vifaa  vya  shule  lakini  kwa  mwaka  huu  umeenda  mbali  zaidi  kwa  wanafunzi  hao  kupatiwa  fedha  taslimu  shilingi  laki  moja  kwa  wale  ambao  wanaishi  katika  familia  zenye  uwezo  mdogo,posho  ya  sh.20,000 na  kupatiwa  baiskeli  kama  njia  ya  kumwezesha  mwanafunzi  kufika   shuleni.

Dr.Nyadzi  sambamba  na  hilo aliweka  bayana  kuwa  mpango  huo  pia  umeendelea  kuwawezesha  wanafunzi  waliopata  ufadhili  kwa  mwaka  jana  ambao  kwasasa  wapo  kidato  cha  pili  ambapo  kila  mwanafunzi  amepata ufadhili  wa kiasi  cha shilingi  490,000.

Akizindua  mpango  huo  wa  Girls connect to Learn,mkuu  wa  wilaya  ya  Uyui  Bw.Stanley  Kolimba  ameupongeza  Mradi  wa  MVP  kwa  kuanzisha  mpango  huo  ambao  utakidhi  mahitaji  ya  serikali  katika  kuwawezesha  wanafunzi  kielimu  huku  akibainisha  changamoto  inayoikabili  wilaya  hiyo  ya  kuwa  na idadi  kubwa  ya  wanafunzi  wakike  ambao  wanakosa  elimu  kutokana  na  matatizo  mengi  yakiwemo  ya  kutokuwa  na  uwezo  wa  kifedha  kwa  baadhi  ya  wazazi.

Bw.Kolimba  alitumia  fursa  hiyo  kuwataka  wazazi  na  walezi  wa  wanafunzi  hao waliohudhuria  katika  hafla  hiyo  fupi  kuunga  mkono  juhudi  za  wafadhili  na  kuhakikisha  wanawapa  malezi  bora  watoto  wao  ikiwa  ni  pamoja  na  kuwapatia  muda  wa  kusoma  badala  ya  kutumia  muda  mwingi  kuwatumikisha  kazi  za  nyumbani  hasa  kilimo.   

Kwa  upande  wake  Mkurugenzi  na  mtafiti  wa  kisayansi  wa  Mradi  wa  vijiji  vya  Milenia  Afrika  kutoka  Chuo  kikuu  cha  Columbia  cha  nchini  Marekani  ambaye  pia  ni  mmoja  kati  ya  wafadhili  wa  mpango  huo  Prof.Cherly  Palm,alisema  jamii  inapaswa  kuwekeza  kwa  kuwasaidia  wanafunzi  hasa  wakike  kwakuwa  kufanya  hivyo  ni  moja  ya  njia  itakayosaidia  kuikomboa  jamii  kuanzia  ngazi  ya  familia.

Alisema  familia  yake  kwa  kutambua  umuhimu  wa  kumsaidia  mwanafunzi  wa  kike  imeamua  kuchangia  katika  mpango  huo  ikiwa  ni  jitihada  za  kumpunguzia  unyonge  wa  umasikini  mwanafunzi  wa  kike.

Aidha  kwa  mujibu  wa  Mradi  wa  Milenia  Mbola   mpango  wa  kuwafadhili  wanafunzi  wanaofanya  vizuri  shuleni  umepangwa  kuwa  endelevu  kwa  kila  mwaka.                      

No comments: