Pages

KAPIPI TV

Monday, November 3, 2014

MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WALAANI VURUGU WAKATI WA MDAHALO

Kwa Niaba ya Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu.

Kutokana na kitendo cha kudhalilisha  kilichofanywa na kundi la watu wachache wanaodaiwa kuwa na maslahi ya chama  kwa ajili ya kuvuruga  mdahalo wa kujadili katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika ukumbi wa Ubungo Plaza tarehe 2/11/2014.  
 
Mtandao unakemea vikali kitendo hicho kilicho watia hatarini watetezi wa haki za binadamu, wahandishi wa habari  pamoja na wahudhuriaji wengine kwani kililenga kuvunja amani ya eneo lile. Vurugu hizo zingeweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali endapo kundi kubwa la wananchi waliohudhuria mdahalo huo wangeamua kupambana na hilo genge la wahuni lilotumwa na kundi fulani la wanasiasa kuharibu mdahalo huo.

Sisi kama Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu, kwa pamoja tusimame kukemea uvunjifu huu wa Ibara za 18,20 na 26  za katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kuzuia uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kushirikiana na wengine na pia wavamizi hao wameshindwa kutekeleza wajibu wa kutii sheria za nchi. Hivyo basi kwa makosa hayo tunaisihi serikali kutolifumbia  swala hili macho na ihakikishe watuhumiwa wanafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Tukumbuke ya kuwa, waliofanyiwa vurugu siku ya jana ni watetezi wa Haki za Binadamu na hivyo sisi kama wanamtandao tunatakiwa kukemea kilichotendeka ili kuhakikisha sauti yetu inasikika kwa pamoja katika kukemea uvunjifu wa haki za binadamu nchini.

Ili kuhakikisha uhuru a maoni unaheshimiwa, mtandao umeanzisha Hashtag ya kutumia kwenye mitandao ya kijamii ya #UhuruwaMaoniKatibaMpya hivyobasi, kwa watumiaji wa mtandao wa Twitter, Instagram na Facebook  tunaomba mtumie hashtag hii kwa wingi kukemea yaliyotokea jana na pia kuwaelimisha wananchi kuwa wana Uhuru wa kuchangia maoni katika katiba mpya.

Pia kuambatana na hiyo hashtag, mtandao unatoa changamoto kwa wanachama wake kupiga picha huku wamebeba makaratasi au mabango yanayolaani vitendo vya jana huku bango moja wapo likiwa limeandikwa #UhuruwaMaoniKatibaMpya. kama ilivyo kwenye picha iliyoambatanishwa.

Kwa wale wa Dar-es-Salaam, Mtandao unapenda kuwakumbusha kutokukosa mkutano wa Viongozi Wakuu  wa Azaki tarehe 4 November 2014 kuanzia saa 4 kamili asubuhi kweye ukumbi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kutoa tamko la kulaani vitendo  hivi ambavyo vinaashiria kuwanyima wananchi haki ya kutoa maoni na kupata taarifa kinyume na Ibara ya 18 na 21 (2) ya katiba ya Tanzania.

Mariagoreth Charles,

Afisa Mawasiliano

No comments: