Pages

KAPIPI TV

Tuesday, July 22, 2014

MAUAJI YA VIKONGWE YASHIKA KASI MLELE- KATAVI

???????????????????????????????
(Picha zote na Kibada Kibada –Mlele Katavi)

Na Kibada Kibada –Mlele Katavi.
Wimbi la mauaji kwa watu wenye umri kuanzia  miaka 60 na kuendelea  Wilayani Mlele Mkoani Katavi linaonekana kushika kasi na kutishia hali ya ulinzi na usalama kama hatua za makusudi hazitachukuliwa.

Hii ni kwa Mujibu wa Taarifa ya Hali ya ulinzi na Usalama Wilayani humo  iliyotolewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya hiyo , Zabron Ibeganisa kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Madiwani uliokuwa ukipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizotekelezwa kwa kipindi cha mwaka  wa 2013/2014.

Mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai alieleza kuwa changamoto zitokanazo na matukio ya mauaji ni kubwa katika wilaya hiyo  na watu wanaolengwa na mauaji hayo ni wale wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea ambapo kwa sehemu kubwa mauaji hufanyika nyakati za usiku kwa kuwavamia walengwa kwenye makazi yao.

Alisema katika matukio 24 yaliyotokea, watu 24 kwa kipindi cha januari hadi juni mwaka 2014   wameuwawa na waliolengwa hasa ni watu wa umri huo.

Alisema kuwa wauaji hao hutumia silaha zenye makali kama panga,shoka, na sime kuwakata waliowalenga na kisha kutoweka bila kuchukua kitu chochote.

Mauaji haya yanafanana sana na jinsi yanavyotokea katika mikoa ya Shinyanga kwa kuwaua vikongwe kwa imani kwamba ni wachawi.

Aidha akifafanua zaidi alieleza kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita kuanzia mwezi januari hadi juni 2014 ,  yametokea mauaji 24 na watu 24 wameuwawa  ambapo kati ya mauaji hayo watuhumiwa sita walikamatwa.

Akibainisha hali ya uhalifu katika wilaya hiyo alieleza kuwa matukio mbalimbali ya makosa madogo ya kuwania mali yalikuwa 107 makosa makubwa dhidi ya binadamu kwa mauaji yalikuwa 24, kubaka 23,kulawiti mawili ,makosa madogo dhidi ya Binadamu yalikuwa 194, makosa madogo dhidi ya uvunjwaji wa maadili yalikuwa 108,  ajali zilizosababisha vifo ni mbili,ajali zilizosababisha majeruhi zilikuwa 39, ajali za kawada 17, makosa mengine 844.

Makosa makubwa dhidi ya maadili ya jamii kama kupatikana na bangi yalikuwa manane, kupatikana na pombe ya moshi 8, makosa ya kupatikana na nyara za serikali yalikuwa matatu na kupatikana na silaha moja
Ipo changamoto kutokana na ugumu uliopo wa kuwatambua wauaji ,hata hivyo jeshi la polisi linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo na kuwaasa  wana jamii  kuendeleza  ule utaratibu wa  daftari la wakazi kwa kuwaorodhesha wakazi kwenye maeneo kwa kuwa ni muhimu na litasaidia kuwatambau wageni wanaoingia kwenye maeneo na iwapo watakuwa na nia mbaya watabainika.

No comments: