Pages

KAPIPI TV

Thursday, July 24, 2014

"KILA MTU ANA HAKI YA KUGOMBEA UBUNGE,KAMA ULIWAJIBIKA VIZURI KWA WANANCHI WATAKUCHAGUA TENA"-MH.MUNDE

Na Mwandishi wetu.
"Hakuna mtu mwenye haki miliki ya Ubunge,kwani hiyo ni dhamana tu tuliyopewa na wananchi,lakini kwanini ifikie hatua ya watu kuhitilafiana na kugombana pasipo sababu za msingi"hii ni kauli ya Mbunge wa vitimaalumu  mkoa wa Tabora Mheshimiwa Munde Tambwe wakati akizungumza na mtandao huu.

Wakati huu kabla  ya kuelekea kwenye mchakato wa kura za maoni  kwa Chama cha Mapinduzi kumekuwa na hali ya kupigana vikumbo kwa baadhi ya makada wa Chama hicho hatua ambayo imebadili kabisa ukurasa wa maisha ya kawaida ya kibinadamu na kujenga sura mpya ya siasa za chuki kwa mtu mmoja kumchafua mwingine au kikundi cha watu fulani kumchafua mtu mmoja jambo ambalo linadhihirisha watu wamesahau kabisa majukumu yao na kugeuza kuwa ni ajenda muhimu ya katika maisha.

Jambo hili limemsukuma Mbunge wa vitimaalum Mheshimiwa Munde Tambwe na kuona kuwa watu wanakoelekea siko ambako CCM inataka kutekeleza malengo yake katika kuwahudumia wananchi ambao kimsingi ndio wamekiweka madarakani chama hicho.

"Ninavyofikiri mimi kwa muda huu sisi kama wanaccm ni vema tushirikiane,tujenge mshikamano katika kutekeleza Ilani ya Chama chetu badala ya kukaa tunajengeana chuki zisizo na msingi,yaani huyu kamsema yule na yule kamsema huyu,hii haitusaidii kabisa itatufanya tushindwe kujibu maswali ya msingi ya wananchi watakapo tuuliza nini tumefanya tangu tuwe madarakani"alisema Mheshimiwa Munde

"Ubunge si haki miliki ya mtu,kwani yeyote anahaki ya kugombea muda ukifika lakini kwasasa tunatakiwa kuwasaidia wananchi,wewe kama umewajibika ipasavyo kwa wananchi, wenyewe watakuchagua hata kama ni vipindi vitatu,lakini kama umepewa dhamana ya kuwa mbunge halafu unashindwa kutekeleza majukumu yako huna sababu ya kugombana na watu,wananchi wenyewe wataamua na wewe utavuna ulichopanda"msisitizo wa ziada wenye lengo la kujenga.

Kwa kauli hii ni vema pia watu waliopewa dhamana au ridhaa na wananchi ya kushika wadhifa walionao wapate fursa ya kujipima,je,wanayo nafasi tena ya kujitosa wakati wa kura za maoni utakapowadia?au ndio kuanzisha chuki na vurugu kwa kila mtu mwenye uwezo wa kifedha unayemuona amevaa sare ya Chama na kutoa misaada kwa watu  unamhisi anataka kuchukua nafasi yako?

"Hakuna mtu anakatazwa kushirikiana na wengine katika kufanya kazi za chama ni vema tukafuata taratibu na kanuni za chama chetu na muda ukifika refarii atapuliza kipenga kila mmoja wetu ataona kama anauwezo wa kuomba nafasi anayoitaka kuliko kuanza kujipitisha huku na kule na kujinadi,binafsi sitofanya hivyo isipokuwa nawaombeni makada wenzangu tushirikiane kutekeleza Ilani ya chama chetu ili wenzetu wa vyama vya upinzani wakose la kuhoji"alisema Mheshimiwa Munde

"Chama cha Mapinduzi kina utaratibu mzuri sana katika kuwapata viongozi wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge ni dhahiri kwamba mtu akifuata taratibu na kanuni za chama chetu atakuwa na haki ya kuwania nafasi anayoitaka na si kweli kwamba kutumia fedha kwa maana ya kuwahonga wapigakura inaweza ikawa sababu ya kuchaguliwa hilo si kweli"alisema huku akitahadharisha wanachama hasa makada ni vema wakashirikiana katika kutekeleza majukumu ya chama katika kutimiza ahadi zilizotolewa na viongozi wakati wa kuomba ridhaa kwa wananchi uchaguzi wa mwaka 2010.

"KWA PAMOJA TUSHIRIKIANE KUUJENGA MKOA WETU,VIONGOZI TUWASAIDIE  WATU WAONDOKANE NA UMASIKINI WA KIPATO,CCM DAIMA"      
  

No comments: