Pages

KAPIPI TV

Monday, June 23, 2014

SHUGHULI ZA WANANCHI CHANZO CHA KUTOWEKA KWA ZIWA KUSARE -ARUSHA


Na  Magreth Magosso, Kigoma.


UHARIBIFU wa mazingira unaofanywa na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi ya Taifa ya Arusha , imeelezwa kuwa ni chanzo  cha kupoteza kwa  baadhi ya vivutio katika hifadhi hiyo na hivyo kusababisha kuzorotesha  utalii wa ndani na nje ya nchi.

                                                            

Akifafanua hilo kwa waandishi wa habari  kutoka Mkoa wa kigoma ambao walitembelea hifadhi hiyo hivi karibuni, Afisa utalii Samweli Sakinoi alisema changamoto ya uharibifu wa mazingira limechangia kutoweka kwa ziwa Kusare ambalo   ni sehemu ya kivutio cha utalii.


Alisema hali hiyo imechangiwa na shughuli mbalimbali za binadamu zinazo endelea katika maeneo hayo ,ambapo ni chachu ya kina cha maji kupungua, kutokana na kujaa kwa tope,  sambamba na wanyama kupoteza maisha kutokana na sumu za madawa yanayotumiwa katika shughuli za kilimo.


“  mbolea zenye kemikali  kali zinaathiri Ekolojia ya aina ya wanyama hasa wakinywa maji yalilitoka kwenye mashamba husika hupata madhara ikiwa ni pamoja na kuwapotezea uhai wao’’alisema Sakinoi.


Mkuu wa idara ya ujirani mwema Pendaeli Shafuri alisema jitihada mbalimbali zimetumika kuhakikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wanashiriki kikamilifu kutunza mazingira licha ya kuwepo kwa changamoto ya mipaka, ambapo bado zinafanyiwa kazi na idara husika.


Alisema elimu wanayotowa kwa jamii husika, imesaidia kutambua umuhimu wa hifadhi  na ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali hasa miradi ya maendeleo  ni pamoja na ujenzi wa mradi wa shule, nyumba za walimu, miundombinu ya maji pamoja na kuchangia katika shughuli za kijamii.


Shafuri alisema  wananchi wamenufaika kupata ajira  ndogondogo kwa vijiji 88 vinavyozunguka hifadhi huku vijiji 21 kati ya hivyo vipo karibu sana na hifadhi jambo ambalo ni changamoto  ya wananchi kutumia fursa hiyo kusogeza mipaka hatimaye kuingia ndani ya hifadhi husika.


“ wananchi wengine hupoteza maisha  kwa kushambuliwa na wanyama wakali pamoja na kuliwa mazao yao na kupelekea uhasama baina yetu ingawa hali hii inachangiwa na ongezeko la jamii husika” alisema Shafuri.


Baadhi ya wakazi wa vijiji husika Michael Palanju na Ally Abdallah walisema hifadhi hiyo imekuwa msaada katika uchangiaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ajira kwa vijana hali inayohamasisha jamii  kuienzi hifadhi iwe endelevu na yenye tija siku za usoni.


Aidha waliitaka serikali iboreshe miundombinu ya Barabara zinazo elekea katika hifadhi hiyo, ili kuongeza ubora na viwango vya hifadhi jambo ambalo litachangia utalii kuongezeka kwa kasi kubwa na kuongezeka  kwa pato la Taifa.

No comments: