Pages

KAPIPI TV

Monday, June 23, 2014

"WAISLAMU TABORA KUMBURUZA MAHAKAMANI SHEIKH MKUU WA TANZANIA"

Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi,baadhi ya waislamu Tabora kwa kushirikiana na viongozi wa Msikiti mkuu wa Ijumaa Tabora mjini wamekusudia kumfikisha mahakamani Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Simba kufuatia mgogoro uliopo baina ya viongozi wa msikiti huo na baraza kuu la Waislam Tanzania Bakwata ambao umesababisha mgawanyiko wa waislamu wa mkoani Tabora.

Taarifa zilizotufikia zimeeleza kuwa tayari taratibu za mahakamani zimekwishafanyika katika kufungua mashtaka dhidi ya kiongozi huyo mkubwa wa dini ya kiislamu hapa nchini na kwamba wakati wowote kuanzia sasa atafikishwa katika mahakama kuu kanda ya Tabora kukabiliana na shitaka lake ambalo inadaiwa limemuunganisha yeye(Mufti),Bakwata na Katibu mkuu wa Bakwata.

Aidha ikumbukwe kwamba katika siku za hivi karibuni Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Simba aliwasimamisha madaraka viongozi wa msikiti mkuu wa ijumaa na kumvua wadhifa wake Sheikh wa mkoa wa Tabora Shaaban Salum jambo ambalo lilipingwa na idadi kubwa ya waumini wa dini ya kiislamu na hivyo kusababisha   kuwa chanzo cha vurugu katika msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni Tabora mjini.

Katika muendelezo wa mgawanyiko na mgogoro huo wa waislamu Tabora mjini ambao ukielezwa kuwa ni wa kwanza kutokea ndani ya miaka zaidi ya 80 iliyopita ambapo Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Simba alimteua Sheikh Ibrahim Mavumbi kuwa Sheikh wa mkoa katika kipindi cha miezi Sita hadi hapo uchaguzi utakapofanyika hatua ambayo pia iliendelea kuleta mzozo  mkubwa hata kufikia hatua kwa baadhi ya waumini kupinga kuongoza ibada kwa Sheikh mteule katika msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni na hivyo kusababisha aliyekuwa Sheikh mkuu Shaaban Salumu kukamatwa na Polisi na hatimaye kufikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora akituhumiwa kwa kosa la kutaka kuleta fujo eneo la kuongozea Ibada msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni akiwa na wafuasi wengine watano.

Hata hivyo hali hii bado imeendelea kuzua mashaka makubwa kutokana na kuwepo kwa tetesi kwamba wapo baadhi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa wamesimama nyuma ya pazia la Mgogoro huo unaoendelea kuwagawa waislamu ingawa hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyejipambanua kuwa anashiriki katika vuguvugu la sakata hilo la waislamu lililoingia katika sura mpya ya mgongano wa maslahi binafsi kwa baadhi ya kikundi cha watu.  

No comments: