Pages

KAPIPI TV

Monday, June 23, 2014

MIKOA 11 NCHINI YANUFAIKA NA HUDUMA ZA AFYA ZITOLEWAZO NA EGPAF

Na Allan Ntana, Tabora

MIKOA 11 hapa nchini imeanza kunufaika na huduma mbalimbali za afya
zinazotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Elizabeth Glaser
Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) Tanzania lenye makao yake makuu
jijini Washington nchini Marekani.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili Mratibu wa Mawasiliano wa
EGPAF Mercy Nyanda alisema tokea kuanzishwa kwake hapa nchini mwaka
2003 shirika hilo limefanikiwa kupanua wigo wa huduma za afya katika
mikoa ipatayo 11.

Alitaja mikoa ambayo imenufaika na huduma za shirika hilo kuwa ni
Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara, Tabora, Simiyu, Geita, Shinyanga,
Mwanza, Zanzibar na Pwani.

Alisema shirika hilo linalofadhiliwa na ‘Watu wa Marekani’ kupitia
mashirika ya CDC na USAID linatoa huduma za afya katika nyanja
mbalimbali ikiwemo huduma ya afya ya uzazi kwa mama na mtoto na kuzuia
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto (PMTCT),
huduma inayotolewa katika mikoa yote.

Huduma nyingine zinazotolewa ni upimaji wa maambukizi ya VVU bure,
utoaji dawa na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU, huduma kwa watoto
wachanga wanaoishi na VVU (EID), utoaji huduma za maabara, huduma za
wagonjwa majumbani na huduma shirikishi ya tiba ya ukimwi na Kifua
kikuu.

Alitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na kuwezesha na kuendesha
mafunzo mbalimbali ya afya kwa watoa huduma walioko katika vituo
mbalimbali vya kutolea huduma za afya katika mikoa hiyo ili kuboresha
huduma hizo.

Nyanda alibainisha kuwa EGPAF kwa msaada wa watu wa Marekani
inaisaidia serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa
jamii katika maeneo mbalimbali ikiwemo ununuzi wa dawa, mashine za
kupimia, kuboresha mazingira ya maabara na vituo vya afya na kutoa
elimu mbalimbali katika fani ya maabara.

‘Ili kufanikisha malengo yake katika mikoa hiyo EGPAF inashirikiana
kwa karibu zaidi na hamashauri za wilaya katika mikoa husika katika
kutekeleza ufanisi wa miradi yake inayohusiana na afya ikiwemo VVU na
UKIMWI’, aliongeza.

Takwimu zinaonyesha kwamba tangu kuanzishwa kwake hapa nchini hadi
mwaka jana 2013 EGPAF imewezesha akina mama zaidi ya mil 2.6 kupima
afya zao na kupewa ushauri nasaha ambapo kati yao 78,400  alikutwa na
maambukizi ya VVU na 67,118 walipewa kinga ya kuzuia maambukizi kwa
watoto wachanga.

Aidha EGPAF imewezesha uandikishaji wa watu wenye VVU 149,184 katika
vituo vya tiba wakiwemo watoto 13,814 walio chini ya umri miaka 15,
kati ya hao 149,184 walioanzishiwa dawa ni 84,000 wakiwemo watoto
8,300 chini ya miaka 15.

Akitoa wito kwa jamii Nyanda alishauri watu kujenga tabia ya kupima
afya zao ili kubaini kama wana VVU na ikibainika waanze kupatiwa
ushauri wa afya zao na wale ambao tayari wana VVU alishauri waende
vituo vya afya wapatiwe dawa za ARV’s, sambamba na hilo aliiasa jamii
kutowabagua wanaoishi na VVU.

No comments: