Msemaji
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab Katimba akizungumza na
waandishi wa habari jana, kuhusu mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
mchakato wa Katiba. Kulia ni Wajumbe, Shaban Ibrahim na Suleiman
Abdallah. Picha na Rafael Lubava.
Na Peter Elias, Mwananchi
“Nchi
hii haithamini mchango wa wataalamu, tumeona Tume ilivyofanya kazi
nzuri, leo hii wanatukanwa hadharani, nawashangaa sana viongozi wa nchi
hii,”.
Dar es Salaam. Jumuiya
na Taasisi za Kiislamu Tanzania imeungana na maaskofu mbalimbali
kuwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa kwa mujibu wa sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia,
taasisi hiyo imemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi
kutokana na kauli waliyodai ya kichochezi, aliyoitoa katika Kanisa la
Methodist, Jimbo la Dodoma kuwa ukipitishwa muundo wa serikali tatu,
jeshi litachukua nchi kwa sababu itashindwa kuwalipa mishahara.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi hizo, Sheikh
Rajab Katimba alilaani kauli kuhusu jeshi na kuwa makanisa yote
yatafungwa na nchi itakosa amani kutokana na kupitisha muundo huo wa
serikali.
Sheikh
Katimba alisema Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
imetokana na utafiti na uchambuzi wa maoni ya wananchi wa Tanzania Bara
na Visiwani ili kuboresha Muungano kutatua kero zilizodumu kwa miaka 50
sasa.
Msimamo
Jumuiya
hiyo iliweka wazi msimamo wake wa kutaka serikali tatu na kutaka maoni
ya makundi mbalimbali ndani ya Bunge la Katiba kuheshimiwa.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ramadhan Sanze pia alisema si ustaarabu kwa kundi moja kuhodhi mchakato kwa masilahi binafsi.
Alisema
kukosoa maoni ya waasisi wa Taifa si dhambi kwa sababu wao hawakuwa
Mungu kwamba hawakosei, badala yake alipendekeza watu waachwe wazungumze
kwa utashi wa matakwa yao juu ya kile kilichowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Nchi
hii haithamini mchango wa wataalamu, tumeona Tume ilivyofanya kazi
nzuri, leo hii wanatukanwa hadharani, nawashangaa sana viongozi wa nchi
hii,” alisema.
Sheikh
Sanze alisema miiko na misingi waliyoiweka waasisi wa Taifa inavunjwa
na viongozi wenyewe ambao leo wanasema waasisi wanatukanwa kwa kuwa
wamependekeza serikali tatu badala ya mbili walizounda waasisi.
“Kulikuwa
na utaratibu wa kubadilishana awamu za uongozi katika Serikali ya
Muungano, awamu hii rais akitoka Tanzania Bara, ijayo atatoka Zanzibar;
hii ndiyo misingi waliyoiweka waasisi, mbona leo haifuatwi? Huu ni
unafiki...” alifafanua Sheikh Sanze.
Jumuiya
hiyo imewataka wananchi wote kuendelea na mshikamano katika kutengeneza
Katiba Mpya yenye maridhiano na itakayoondoa kero zilizodumu kwa zaidi
ya miaka 50.
Kuhusu Lukuvi
Sheikh
Katimba alisema iwapo Lukuvi alikuwa anasisitiza suala la amani, basi
angezungumzia ulipuaji wa mabomu unaotokea Arusha, tena kanisani, jambo
ambalo hakugusia kabisa badala yake alikuwa akieneza propaganda za kuwa
serikali mbili ndizo bora zaidi.
“Kama
Lukuvi ana utafiti alioufanya, kwa nini asiutoe na kuwaeleza
Watanzania? Kulikuwa na haja gani ya kutumia mabilioni ya pesa za
wananchi kwa jambo ambalo Lukuvi na chama chake walishakuwa na mpango
wao?” alihoji Sheikh Katimba. Jumuiya hiyo imepinga kauli nyingine ya
Lukuvi kuwa Wazanzibari wanataka serikali yao ili wajitangaze kuwa nchi
ya Kiislamu.
“Waislamu wameiita kauli hiyo kuwa ni ya kichochezi yenye lengo la kuwagawa kwa misingi ya kidini,” alisema.
Alisema
Taasisi ya Uamsho ambayo Lukuvi aliituhumu kuwa na msimamo mkali, ni
taasisi halali iliyosajiliwa na Serikali katika kuendesha shughuli zake.
Alisema mpaka sasa Uamsho imeshinda baadhi ya kesi zilizokuwa
zinawakabili viongozi wao na nyingine bado zinaendelea mahakamani.
Alihoji
kuwa kama Lukuvi alikuwa na ushahidi wa kutosha kwa nini hakuupeleka
mahakamani kuthibitisha kuwa kikundi hichi ni tishio kwa amani ya nchi
kutokana na misimamo yake mikali.
Jumuiya hiyo imeitaka Serikali kukanusha kwa uwazi na kuwaomba radhi Waislamu na wananchi kwa jumla juu ya kauli ya Lukuvi.
“Tunamtaka
Waziri Lukuvi ajiuzulu nafasi zake za uongozi kwa sababu anazitumia
vibaya kuchochea chuki. Tunashangaa mpaka sasa Serikali haijachukua
hatua yoyote, Rais amwajibishe,” alisema kiongozi huyo. CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment