Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia jana aliongoza
mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Moshi
Chang'a yaliyofanyika katika makaburi ya Mtwivila, Kihesa Iringa.
Akizungumza
katika mazishi hayo, Ghasia alisema Chang'a alikuwa mchapakazi na kuwa
hata yalipofanyika mabadiliko ya maeneo ya kazi kutoka wilaya moja
kwenda nyingine, hakuwahi kulalamika tofauti na ma-DC wengine.
Alitoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa wilaya aliyokuwa akiiongoza kwa kuondokewa na mchapakazi huyo.
Ghasia
aliwataka wananchi wakati wote kuwa tayari kwa kifo na kutenda mema kwa
watu wote bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini, kama alivyokuwa
Chang'a.
Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema DC Chang'a alikufa kutokana na
shinikizo la damu na kisukari, na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili tangu Machi 29, mwaka huu.
Alisema wakati wa uhai wake, marehemu Chang'a alikuwa mcheshi na mchapakazi kwa jamii anayoitumikia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Chang'a ndiye aliyechangia yeye kupata wadhifa huo alionao.
Spika
Makinda alisema alipata ubunge wa Njombe Kusini mwaka 1995 katika
uchaguzi wenye ushindani mkali na wa kwanza wa vyama vingi kwa msaada
mkubwa kutoka kwa Chang'a, wakati huo akiwa Katibu wa CCM Wilaya ya
Njombe.
Alisema
Chang'a alifanikisha masuala mengi ambayo yaliwashinda watu wengi,
ikiwamo kutuliza vuguvugu la kisiasa na kuwasikiliza watu wote bila
kujali itikadi za kisiasa na kidini.
Alisema
licha ya kushinda kwenye uchaguzi huo katika ushindani mkali wa
NCCR-Mageuzi, baadaye ilifunguliwa kesi ambayo ilidumu kwa miaka minne
na mmoja wa waliosaidia kushinda kesi hiyo ni Chang'a.
Alisema ni vyema kuiga mfano wa utendaji wa kiongozi huyo hasa kwa kuweka mbele masilahi ya Taifa.
Meneja wa
Wakala wa Misitu Kanda ya Kusini, Bruno Mallya alisema enzi za uhai
wake, marehemu alihimiza wananchi kutunza mazingira.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment