Hawa ni wahamiaji wa haramu waliokamatwa usiku wa kuamkia leo mkoani Iringa
Hapa wakipata chakula kwani walikuwa kwenye hali mbaya kwa kukosa chakula
Hili ni gari ambalo lilikuwa likiwasafirisha kutoka jijini Tanga
Kamanda wa
polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi alizungumza na waandishi wa
habari kuhusiana na kukamatwa kwa wahamiaji hao.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
JESHI la Polisi mkoani Iringa limewakamata wahamiaji haramu 46 kutoka Ethiopia wakiwa njiani kuelekea Afrika Kusini.Akizungumza na wanahabari mjini humo, Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, ACP Ramadhani Mungi, amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 9:50 alfajiri ya leo katika eneo la Sheli ya zamani kwenye kitongoji cha Geza Ulole, Kijiji cha Ruaha Mbuyuni, Tarafa ya Mahenge wilayani Kilolo.
Kamanda Mungi amesema askari polisi wakiwa kwenye doria waliwakamata wahamiaji hao haramu 46 kutoka Ethiopia wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T342AJU aina ya Canter likiendeshwa na Mbega Ally (37), kabila Mbondei na mkazi wa Tanga wakiwa wanaelekea Afrika Kusini. Dereva wa gari hilo amekamatwa.
"Tumefanikiwa kuwakamata wahamiaji hawa haramu baada ya kupata taarifa za kiitelijensia, hii inaonyesha namna gani tulivyojipanga kuhakikisha tunawadhibiti wahalifu wote wakiwemo wahamiaji haramu," alisema Mungi.
Mungi alisema kwamba, wahamiaji hao waliwekwa katikati ya matenga (maboksi) ya kubebea nyanya ambayo yalikuwa tu.
Wahamiaji hao haramu walikuwa wamepakiwa kwenye Canter hiyo inayomilikiwa na Bw. Zuberi Kitojo mkazi wa Tanga, ambapo wahusika walidai kwamba walikuwa wamepakia nyanya.
Mmoja wa wahamiaji hao haramu, Shiraom Tadeu (20), amesema kwamba wamekimbia vita Ethiopia na kwamba walikuwa wanaelekea Malawi kwenye makambi ya wakimbizi.
"Tumetumia siku 21 porini tukikwepa vyombo vya usalama. Tumepitia Kenya na hatimaye kuingia Tanzania, kule hali ni mbaya sana," alisema Tadeu na kuongeza kwamba wameshindwa kuomba hifadhi ya ukimbizi Kenya kwa sababu hali ya amani ni tete, lakini kwa hapa Tanzania hakuna kambi hata moja ya wakimbizi," alisema.
Tadeu, ambaye anaongea Kiswahili kidogo, alisema kaka yake pia yuko kwenye kambi hizo za wakimbizi nchini Malawi na ndiye amekuwa akiwasiliana naye tangu wanatoka Ethiopia.
No comments:
Post a Comment