Pages

KAPIPI TV

Friday, October 18, 2013

WABUNGE WA MAJIMBO TABORA WAFANYIWA TATHIMINI,MMOJA APATA ASILIMIA 20,KASHINDWA KUTEKELEZA AHADI ZAKE

Na  Mwandishi wetu maalumu.

Kama  ilivyokawaida  yangu,ndugu zangu  nilikuwa kimya muda mrefu hii  ni kwasababu  ya  kufuatilia huko  majimboni hawa waheshimiwa tuliowachagua kutuwakilisha mjengoni nini  wanachokifanya na wanawasidia vipi wananchi katika kuleta maendeleo  kama  walivyoahidi.

Kiukweli wapo ambao bila kusema uongo wamekuwa karibu zaidi na wananchi na kujua namna gani wanatoa michango yao kuleta mabadiliko ya kimaendeleo ingawa si kwa kiwango walichoahidi, na hii  imetokana  na ukweli kwamba  ni  binadamu hajakamilika,si vibaya...tunawasamehe,tunasameheana.

Wakati  nafuatilia  suala  hili  ambalo lilikuwa  likinikera  zaidi  kwa  kuwa  kila nilipokuwa nikikutana na  mwananchi ambaye ndiye kimsingi ni mpiga kura alikuwa akilalamikia mheshimiwa na Jimboni kwake kwa kushindwa kutekeleza hiki mara kile ilimradi tu inaonesha ni jinsi gani kero za maendeleo  zinavyoshindwa kutekelezeka kama ilivyoahidiwa wakati wa kuomba kura.

Kwa wabunge baadhi  kama nilivyosema  hapo  awali angalau  wamefanya kile walichoweza kukifanya na hivyo kupunguza malalamiko kwa wapiga kura wao,si vibaya kuliko kukosa kabisa....Wapo wengine kilichowasaidia zaidi  hata kama hawatekelezi kwa asilimia mia moja,lakini ukaribu wao kwa wananchi ndio msingi bora wa mafanikio yao hata kama watajaribu kurudi tena kwa wananchi na kuomba ridhaa  ya  kuchaguliwa kushika nyadhifa hizo.

Wapo  waheshimiwa wengine huwafikia wapiga kura na  kuwa  karibu  nao  kama  jamii  moja,hushiriki pia  masuala  mbalimbali  kama  kawaida ingawa  wanaonesha mguu  nje,mguu  ndani,wanajenga  mahusianao mazuri  na  wananchi  wakati  wote.

Kwa maeneo  ya  majimbo mengine  ya  hapa  mkoani  Tabora  imenishangaza  sana  kuona  mheshimiwa  akiingia  na  kutoka  jimbo  mwake hatuliii kana  kwamba  kakalia  kiti  cha  moto,...anawachekea  wananchi  kwa  kuwadhihaki,hana ukweli  hata  mmoja,ana weweseka  kuona  labda  nafasi  yake  huenda  akaikosa  kipindi  kijacho  na kumhisia kila mtu  kuwa huenda  atampokonya  nafasi  hiyo  aliyonayo.

Hili likanifanya nianzishe mazungumzo na  baadhi ya  wananchi  kwa  kila  jimbo  la  mkoa  wa  Tabora,kwakweli  niliyoyakuta ndugu zangu sio siri chama kilichopo madarakani kwa maana  ya  CCM kitakuwa na wakati  mgumu sana katika uchaguzi mkuu  wa 2015 ingawa kwa upande wa upinzani sioni kama watakuwa wanalifahamu hilo.

Ukitazama huduma nyingi za kijamii hazieleweki,usimamizi mbovu fedha za umma,maendeleo hayalingani na hali halisi....Kero kubwa kwa walimu,mapunjo yasiyoeleweka,hakuna mtu wa kuwasemea na hata kama akitokea kuwasemea hafuatilii zaidi ya  kuingia mjengoni na kupiga usingizi akishtuka kazi yake kubwa ni  kukubali NDIYOOOO  AU  SIYOOOOO bila kujali kaulizwa nini.     

Angalau  baadhi ya majimbo  hasa  ya  wale  ambao  wamekalia viti hivyo  kwa muda mrefu hawana  matatizo na wapiga kura wao,na sio kama nathibitisha kuwa wametekeleza ipasavyo ahadi zao  lakini niseme kuwa Waheshimiwa hao wanajua kula  na Kipofu!

Naomba nisiwachukulie muda wenu kuhusu hili,licha ya kuwa tathmini niliyoifanya mimi binafsi nimeamua kuiweka pembeni kuhusu alama kwa kiwango cha asilimia nilizowapatia waheshimiwa hawa, lakini naomba niwaeleze zile nilizozichungulia kwenye fomu za tathimini za kuwapima wabunge wa CCM katika majimbo saba ya mkoa wa Tabora.

Amini usiamini,wanachama wenzangu wa CCM wakaamua  kuniibia siri kuwa, CCM makao  makuu  wameleta fomu huku majimboni ambazo zitajazwa kuwatathimini wabunge mambo waliyoyafanya na endapo kama uchaguzi utaitishwa ghafla je watakuwa na nafasi gani,na ni vipi chama wabunge wameweza kukijengea imani kwa wananchi waliowachagua,....Lakini  zaidi  ya  yote huu  umeonekana kuwa ni mfumo mzuri utakaosaidia wabunge kuondoa usingizi mzito walionao.

Nilivyochungulia kwa mara ya kwanza nikakutana na matokeo ya tathimini za Jimbo la Bukene,nikasema si vibaya sana imekaa vizuri....Nikaendelea jimbo la Igalula,mhmmmm!!!..jamani acha tu......Nikafunua Jimbo la Nzega  kama vile ilikuwa nusu kwa nusu.

Nikazidi kupata shauku Jimbo la Urambo mashariki,angalau iko sawa....Jimbo la Urambo magharibi zikawa dalili za matumaini kiasi.....Mungu wangu nikazipitia za Sikonge nafuu  na  ahueni kabisa ikawepo...Karatasi iliyofuata jamani nikachungulia Tabora Kaskazini,ikawa ni za kipekee kuliko maeneo mengine.....Igunga nikaangalia nikasema huyu kwa kuwa alikuwa kwenye matatizo muda mrefu inawezekana kupata hizi asilimia alizopata.

Nilipotaka kukata tamaa kuendelea kuangalia tena karatasi hizo nikagundua kuwa bado kuna mapungufu kama nisingeangalia kwa Jimbo la Tabora mjini ambako nilifunua na kufunika nikajisikia usingizi umenibana ghafla na kuamua kumpatia yule mwanaCCM mwenzangu zile kopi za  karatasi za tathimini ambazo zinatarajiwa kupelekwa makao makuu kwa ajili ya kuzipitia upya na hatimaye kuwapa mrejesho wabunge kwa kile walichokipanda tangu kuchaguliwa kwao.

Kwa ujumla ndugu zangu angalau wapo baadhi  ya wabunge wamepata zaidi ya asilimia 50,lakini mbunge mmoja kati ya wabunge 8 wa mkoa wa Tabora amepata asilimia 19.87 kwa ujumla katika tathimini aliyofanyiwa jimboni kwake ambazo kwa Jimbo lake zililazimika kufanyika kwenye Kata badala ya kamati ya siasa ya wilaya kama inavyotakiwa.  

Kibaya zaidi tathimini iliyofanywa kwa mbunge huyo baadhi ya Kata alipata asilimia moja na Kata nyingine ni asilimia 0.01 ikimaanisha kuwa hakubaliki kabisa.

Ndugu zangu naomba niishie hapa nasubiri atakachokisema Mwenyekiti wetu wa Taifa Dr.Jakaya Mrisho Kikwete wakati matokeo ya tathimini hizo kwa nchi nzima zitakapofikishwa mezani kwake na kutoa majibu.

Ahsanteni sana.
         

 
              

No comments: