Na Mwandishi wetu, Tabora
VITENDO vya uharibifu wa mazingira katika manispaa ya Tabora
vimeendelea kuongezeka siku hadi siku katika maeneo mbalimbali ndani
ya manispaa hiyo hali inayotishia kuharibika kwa mandhari na mwonekano
mzima wa mazingira ya mji huo mkongwe.
Maeneo mengi yanayozunguka manispaa ya Tabora yamejaa mashimo makubwa
yanayosababishwa na uchimbaji wa mchanga kwa ajili ya kuuza na
shughuli zingine kama vile ufyatuaji matofali na ujenzi wa matanuru
ya kuchomea matofali hayo hali inayoashiria uharibifu mkubwa wa
mazingira katika manispaa hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Tabora Alfred Luanda alibainisha
hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari ambapo alieleza
kuwa amedhamiria kulisimamia kidete kwa sababu uharibifu wa mazingira
mahali popote pale unaharibu mandhari ya mji na unachangia kwa kiasi
kikubwa uchafuzi wa mazingira.
Alisema uchimbaji huo wa mchanga, mawe na udongo wa kufyatulia tofali
za kuchoma unafanywa kiholela pasipo mpangilio wowote na karibu
maeneo mengi yanayozunguka manispaa ya Tabora hususani maeneo ya
Mawiti, Kizigo, Malolo na mengineyo yameharibiwa vibaya na bado watu
wanaendelea kuchimba.
Aidha alisema wameanza kuchukua hatua kadhaa za kukomesha vitendo
hivyo ikiwemo kusambaza taarifa mbalimbali za matangazo ya kupiga
marufuku uchimbaji huo katika mitaa mbalimbali ya mji huo lakini
baadhi ya watu hawasikii, badala yake shughuli hizo zinaendelea
kufanyika kama kawaida japo kwa kujificha.
Ndugu waandishi, napenda kuwataarifu kuwa mimi na watendaji wenzangu
tumechoshwa na vitendo hivi vinavyoharibu mandhari ya mji wetu,
tumedhamiria kukomesha uharibifu huu na katika kufanikisha hili
tumepanga kuendelea na oparesheni ya kuwakamata na kuwatoza faini
sambamba na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, alisema.
Aidha alitoa wito kwa wenyeviti wa vitongoji , serikali za mitaa,
watendaji wa kata, madiwani na wakazi wote wa manispaa hiyo
kushirikiana na watendaji wa manispaa hiyo ili kuhakikisha vitendo
vyote vya uharibifu wa mazingira vinavyofanyika katika maeneo yao
vinadhibitiwa na kukomeshwa kabisa sambamba na kuchukua hatua za
kisheria kwa wote watakao kaidi.
No comments:
Post a Comment