Pages

KAPIPI TV

Friday, October 18, 2013

JAMII YAASWA KUJENGA TABIA YA KUNAWA MIKONO KWA SABUNI

Na Allan Ntana, Uyui

WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi
na sabuni ili kujiepusha na magonjwa ya kuhara ambayo huenezwa
kutokana na kushika kinyesi au uchafu wowote wenye vijidudu.

Ili kudhibiti maambukizi hayo ya magonjwa ya kuhara wananchi
wanatakiwa kutambua nyakati muhimu za kunawa mikono kwa maji na sabuni
ambazo ni kila watokapo chooni, kabla na baada ya kula, wanapooga na
kila wanapotawaza watoto.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Said
Ntahondi katika maadhimisho ya ‘Siku ya Unawaji Mikono Duniani’
iliyofanyika jana katika tarafa ya Ilolangulu wilaya ya Uyui mkoani
Tabora chini ya uratibu wa mradi wa Millenia Village Mbola.

Alisema magonjwa ya kuhara, homa ya matumbo, kipindupindu na mengineyo
yanaweza kuepukwa na jamii kwa kujijengea utamaduni wa kujali afya zao
hasa kwa katika suala la usafi wa mikono, kabla ya kula kitu chochote
kile tunapaswa kunawa kwanza ili kuondoa vijidudu vyote katika mikono
yetu.

‘Natoa wito kwa wazazi wote, hakikisheni kabla ya kula kaya nzima
inawe mikono kwa maji safi na sabuni ndipo muanze kula na kama sabuni
hamna tumieni maji na majivu kunawa vinginevyo mtakula vijidudu’
alisema

Awali Dr. Jaiving Kazitanga, Mratibu wa Afya katika vijiji vya mradi
wa Millenia Mbola, alisema lengo la kampeni hii kuongeza uelewa wa
jamii juu ya umuhimu wa kunawa mikono kwa maji na sabuni kama njia
sahihi ya kupunguza uenezi wa magonjwa ya kuhara.

Alisema vijidudu vya magonjwa ya kuhara hutoka kwa muathirika kwenda
kwa mwingine ambaye ni mzima kwa njia mbalimbali kama kushika mikono,
kula bila kunawa, kula matunda pasipo kuoshwa, kunywa maji
yaliyochafuliwa kwa kinyesi cha binadamu na mwisho vijidudu hivi
huingia mwilini kupitia mdomoni mwetu na hewa.

Aliongeza kuwa tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kwamba uhamasishaji
wa unawaji wa mikono na sabuni kwa watoto hupunguza utoro mashuleni
kwa mfano katika nchi za Misri, Uchina na Kolombia utoro kwa watoto wa
shule ulipungua kwa asilimia 20 hadi 50 baada ya wanafunzi kuanza
tabia ya kunawa mikono na sabuni hivyo kujiepusha na magonjwa.

Aidha alisema ‘Siku ya Unawaji Mikono Duniani’ ni siku ya kuhamasisha
na kuchochea mamilioni ya watu duniani kunawa mikono yao kwa maji
yanayotiririka na sabuni na siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 15
Octoba, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni SAIDIA
WATOTO KUFIKISHA MIAKA 5 NA KUENDELEA.

No comments: