AFISA
mtendaji ya kata ya Kitunda, wilayani Sikonge, mkoani Tabora, Julius Ndege, amenusurika
kuuawa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi baada ya kumkosakosa kwa kumfyatulia
risasi kuelekea kwenye gari yake.
Akielezea mkasa
huo, afisa mtendaji huyo, alisema makasa huo ulimtokea wiki hii, siku ya
jumatatu ya tarehe 25 machi, majira ya saa nane mchana, wakati akitokea Kitunda
kuja Sikonge mjini akiwa na familia yake.
Ndege alisema
akiwa na gari yake yenye namba za usajili T 189 BAG aina ya RAV 4, alipofika eneo linalojulikana
kama “mtaji wa masikini” ghafla aliona watu watatu wenye makoti makubwa
walioficha nyuso zao na sura za bandia wakitokea msituni kuelekea eneo la
barabara.
Alisema mmoja
kati yao alikuwa na silaha aina ya SMG, mmoja akiwa na jiwe kubwa na mwingine
akiwa hana kitu chochote walijitokeza barabarani ghafla na yule mwenye silaha
akachuchumaa chini na kuanza kufyatua risasi mbili mfululilizo akilenga tairi
za gari, huku mwingine akiwa anasukuma jiwe kubwa kufunga barabara.
Kufuatia hali
hiyo mtendaji alisema alijifanya kama anasimama na wao walipozubaa alikanyaga
mafuta na kufanikiwa kuwatoroka, lakini wakati amefanikiwa kuwatoroka majambazi
hao walifyatua risasi nyingine ambayo ilikwenda kuharibu rejeta ambayo ilianza
kuvuja maji.
Ndege alisema
alijikongoja na kufanikiwa kufika katika kijiji cha Mabangwe ambapo aliomba
msaada wa maji kwa wananchi na kuweka kwenye rejeta, kisha akafanikiwa kutoa
taarifa kituo cha polisi wilaya ya Sikonge kwa njia ya simu.
Aidha mtendaji
huyo alisema kwenye gari yake alikuwa na mkewe aitwaye Vailet Jumanne, mtendaji
wa kijiji cha Mwenge Shaban Swed, motto wake Janet Julius mwenye umri wa mwaka
mmoja na nusuu na watu wengine wawili ambao alikuwa amewapa lifti.
Mtendaji huyo
ametoa wito kwa uongozi wa wilaya na polisi kuweka utaratibu wa askari
kusindikiza mabasi ya abiria hasa yale yaendayo mbeya kwani hali ya utekaji nyara
magari ya abiria na ya mizigo huenda ukarudia tena na kuongeza kuwa hali hiyo itasaidia kupunguza uharifu hasa
ikizingatiwa kuwa kata ya Kitunda kwa sasa kuna machimbo ya madini ya dhahabu
na kuna watu zaidi ya 3,000 kwa sasa hapo machimboni.
Aidha alisema
alifika mjini Sikonge majira ya saa 11:05 jioni na alifika kituo cha polisi na
kutoa taarifa hiyo na askari walianza safari kuelekea eneo la tukio.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Tabora amesema ametuma askari kupitia kituo cha polisi Sikonge
kwenda kufanya doria kwenye eneo la tukio na hata kwenye machimbo kama kuna
watu wanajihusisha na matukio ya utekaji na ujambazi.
No comments:
Post a Comment