RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete,jumapili, anaanza ziara ya siku 5 mkoani hapa,kukagua shughuli
mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongea na wananchi.
Akitangaza
ujio huo kwa waandishi wa habari, mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa,
alisema kuwa rais atawasili siku ya Jumapili mkoani Tabora, akitokea
mkoani Singida na ziara yake itaanzia wilayani Igunga, ambapo atapokea
taarifa ya mkoa na ya wilaya hiyo.
Mwassa
aliongeza kuwa mheshimiwa Rais akiwa wilayani humo ataweka jiwe la
msingi kwenye ujenzi wa daraja la Mbutu na kufungua ‘Chujio la
Maji-Bulenya’ na baadaye atafanya mkutano wa hadhara mjini Igunga kabla
ya kuelekea Nzega.
Akiwa
wilayani Nzega, Rais Kikwete ataongea na wananchi katika mkutano wa
hadhara na baadae jioni atapokea taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo, na
siku inayofuata ataelekea Puge kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa
barabara ya Nzega- Tabora kabla ya kuelekea wilayani Uyui.
Aidha Mwassa aliongeza kuwa akiwa wilayani Uyui, Rais Kikwete mbali na kupokea taarifa ya maendeleo pia ataweka
jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Tabora-Ndono na
Tabora-Manyoni kupitia Nyahua na kisha kuongea na wananchi katika
mkutano wa hadhara kabla ya kuondoka kuelekea Tabora mjini.
Katika
ziara hiyo, Rais Kikwete pia atazitembelea wilaya za Urambo, Kaliua na
Sikonge ambapo atapokea taarifa za maendeleo kwa kila wilaya sambamba na
kukagua shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo pamoja na kuongea na
wananchi..
Akiwa
wilayani Urambo na Kaliua, Rais Kikwete ataweka jiwe la msingi katika
ujenzi wa barabara ya Ndono – Urambo na kuzindua shule ya sekondari
Kaliua.
Mwassa
alibainisha kuwa miradi mingine itakayozinduliwa katika ziara hiyo ya
Rais ni pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa Uboreshaji
huduma za Maji-Igombe na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa uwanja
wa ndege wa Tabora ambao upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Aidha,
Mwassa amewataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais, kila
atakapopita, kuanzia mwanzo wa ziara yake mpaka hapo atakapoondoka, kwani hii ni bahati ya kipekee kutembelewa na mkuu wa nchi mwanzoni mwa mwaka mpya.
‘‘Naamini
ujio wake una baraka za kipekee kwa mkoa wetu wa Tabora’ kwa sababu ni
mtu anayesikiliza kilio cha wananchi wake’’, aliongeza Mwassa
No comments:
Post a Comment