Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi -Zanzibar
Maafisa wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa nchini pamoja na Mamkala
ya Bandari Zanzibar, wamefanya oparesheni maalum ya ukaguzi wa meli ya AZAM Sealink -1 iliyoingia nchini juzi kuangalia kama ina ubora na kukidhi vigezo vya usafirishaji wa abiria na mizigo majini yakiwemo magari.
Maafisa waliofanya ukaguzi huo ni kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Usalama wa taifa, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Mamlaka ya Usalama Bandarini na Huduma za Meli Zanzibar (ZMA) na Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Pamoja
na kuangalia ubora na vigezo vingine, Maafisa hao pia wamepata maelezo
toshelezi juu ya ubora wa meli hiyo kutoka kwa Kampuni ya RFI iliyopewa dhamana ya kuisafirisha Meli hiyo kutoka nchini Ugiriki hadi hapa nchini.
Akizungumza
na Ujumbe huo ndani ya Meli hiyo iliyoweka nanga nje kidogo ya Bandari
ya Zanzibar, Mkurugenzi wa RFI Bw. Stefan Nedkoff, alisema kuwa meli
hiyo imeweza kusafiri yenyewe kutoka nchini Ubeligiji hadi hapa nchini
pasipo msaada wowote wa kiufundi.
Amesema
kuwa katika maeneo waliyopitia walipambana na kila aina ya dharuba na
kuvuka vikwazo vya mikondo mikubwa ya bahari kwenye kina kirefu na Meli
hiyo iliweza kuhimili hali hiyo.
Alisema
Meli hiyo inayoongozwa kwa mifumo ya kompyuta, ina uwezo mkubwa wa
kuhimili misukosuko ya hali ya bahari na kusafiri umbali na kina kirefu
cha maji baharini pasipo shaka.
Bw.
Nedkoff amesema kuwa, mbali ya kuwa meli hiyo ilisafiri ikiwa tupu,
lakini itahimili vishindo zaidi vya baharini pale itakapokuwa na abiria
na mizigo ya kutosha.
Amesema
kuwa mbali ya uwezo wake wa kubeba abiria 1,500, lakini pia meli hiyo
inauwezo wa kuchukua mizigo yakiwemo magari 200 kutoka eneo moja kwenda
jingine vyote vikiwa na uzito wa tani 500 bila ya kuwa na tatizo lolote
la kiusalama.
Maafisa
walioitembelea meli hiyo, wameonyeshwa njia maalum za kujiokolea pamoja
na vifaa muhimu vya kiusalama vinavyoweza kutumika kwa uokozi wakati itokeapo ajali majini.
Meli hiyo pia ina vitanda vya kutosha kwa ajili ya wagonjwa na abiria watakaojisikia kupumzika wakati wanapokuwa safarini.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari mjini Zanzibar mara baada ya kuwasili kwa Meli
hiyo, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Azam Coastal Ferry inayomiliki Boti
ziendazo kasi za Kilimanjaro, Bw. Hussein Mohammed Saidi, alisema meli
hiyo itafanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba.
Amesema
Kampuni yake ambayo ipo kihuduma zaidi, pia itaangalia uwezekano wa
kuweka viwango vya nauli itakayomfanya kila mtu kusafiri yeye pamoja na
jamaa ama watoto wake bila ya kujinyima.
Bw.
Hussein alisema watoto wenye umri wa kuanzia saa moja hadi mika mitano
watasafirishwa bure na wanafunzi watatozwa nusu ya nauli ya mtu mzima
kwa kila safari.
No comments:
Post a Comment