Pages

KAPIPI TV

Friday, July 20, 2012

WANAUME KUSHIRIKI KATIKA AFYA YA UZAZI NA MTOTO

NA LUCAS RAPHAEL TABORA

Ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi na mtoto ni mojawapo ya njia thabiti katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na ni mbinu sahihi katika kuhakikisha tunatokomeza Virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa watoto nchini Tanzania.

                                          
Kutokana na sababu mbalimnbali ikiwemo mfumo dume katika jamii za kitanzania,  imepelekea watoto wengi kuzaliwa wakiwa na maambukizi ya VVU wakati huduma za kuwakinga zinapatikana kila mahali na bila malipo yoyote nchini.

Shirika la EGPAF ambalo  linakusudia kuondoa tatizo la VVU kwa watoto limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCT) kupitia hospitali, zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika baadhi ya mikoa hapa nchini

Lengo ni kuhakikisha watoto wanaozaliwa hawana maambukizi ya virusi vya UKIMWI hata kama wazazi wao wanaishi na virusi vya UKIMWI kwa maana “kuwa na kizazi kisicho na UKIMWI na VVU nchini Tanzania, inawezekana.”

Daktari Tresphory Rugaragu ni afisa wa EGPAF, anyeshughulika na  mpango wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma za matibabu na matunzo kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI mkoani Tabora, amesema kwamba asilimia 20 ya watu duniani ni watoto hivyo wanastahili kuzaliwa bila maambukizi ya VVU .

Amesema kwamba watoto hao wanaweza kuzaliwa bila ya maambukizi iwapo kina baba watashirikiana  kikamilifu na wenza wao katika huduma ya afya ya uzazi na kupima VVU pamoja wakati wa ujauzito wa mama.

Amesema kwamba  wanaweza kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto mfumo dume ukitupiliwa mbali ili jamii yote iweze kushiriki kwenda kliniki kwa ajili ya kumpeleka mama na wanaume kupima afya zao na kupata elimu ya uzazi.

Dkt Rugaruga amesema, taasisi hiyo isiyokuwa ya kiserikali na ambayo inashirikiana na wizara ya afya na ustawi wa jamii, imekuwa ikihamasisha wazazi wote mke na mume  wapime afya zao kwa ajili ya kubaini endapo wanamaambukizi ya VVU au hawana.

Amesema kwamba iwapo watakuwa hawana maambukizi ya VVU, mtoto atayezailwa atakuwa mwenye afya njema ,lakini ikitokea wazazi  wameambukizwa na virusi vya UKIMWI huelimishwa ili mtoto atakayezaliwa asiwe na maambukizi ya VVU.

Amesema EGPAF hushirikiana na hospitali, vituo vya afya, na  zahanati mbalimbali katika kutoa huduma zakuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).

Huduma zingine ambazo zimekuwa zinafadhiliwa na (EGPAF) kwenye vituo hivyo ni ugunduzi wa mapema wa VVU kwa watoto wachanga (EID),huduma za matibabu na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.

Huduma zingine ni huduma shirikishi ya tiba ya UKIMWI na kifua kikuu,usaidizi wa maabara na huduma kwa wagonjwa majumbani yenye lengo la kuhakikisha wale wasiojiweza kutoka na kwenda kituo cha kutolea tiba wanapatiwa tiba majumbani kwao.

Dkt Rugaruga amesema kwamba sasa kila Hospitali,Kituo cha afya na zahanati kuna watoa ushauri nasaha kwa ajili ya kutoa elimu ya uzazi kwa wanaume na kinamama wanaokwenda na wenzi wao wao kwa ajili ya kucheki afya zao .

Ameongeza kuwa, baadhi ya wanaume wamekuwa wazito kuambatana nawake zao katika huduma za kliniki ya afya ya uzazi na mtoto kutokana na dhana potofu kuwakuongozana na mke kwenda kituo cha afya inaashiria kuwa mke wako anakutawala”

Dkt Rugaragu amesisitiza kuwa dhana hiyo ni potofu na amesisitiza kuwa kila baba anayejali familia yake ni muhimu kupima afya zao wakiwa pamoja nanzi wao hususankatika kipindi kigumu cha ujauzito wa mama kwani hii itasaidia katika kumjali mama na mtoto na kuhakikisha mtoto anazaliwa salama.

Amesema kwamba wanaume wa mjini ndio wamekuwa kikwazo zaidi cha kushindwa kwenda na wake zao kwenye vituo vya afya kwani wengi wanasingizia majukumu ya kazi  .

Amesema kwamba wanaume wengi waliopo mijini wamekuwa na visingizio vingi ukilinganisha na wale walio pembezoni na mji hasa vijijini wamekuwa ni mfano mzuri sana, kwa kwenda na wake zao kwenye zahanati kuanzia hatua za awali mpaka kujifungua na kichachofanyika kwenye zahanati hizo ,pale anapoonekana mama na baba wanapata huduma haraka ili baba asione usumbufu kukaa kwa muda mrefu kumsubiri mkewe.

“hilo ndio linalofanyika karibu kila hospitali,zahanati na vituo vya afya ,inasaidia sana kumfanya mwanaume kwenda na mke wake mara kwa mara ili isionekane sehemu hizo ni sehemu za kuchelewesha watu bila sababu za msingi .


Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa mawasiliano na utetezi wa EGPAF,Mercy Nyanda Kingu, amesema kwamba EGPAF inakusudia kuondoa VVU kwa watoto

Amesema kwamba changamoto ambayo wameipata katika mkoa wa Tabora ni ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi na  mtoto ,hasa katika mpango wa kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

Amesema wanaume wengi kutokana na sababu mbalimbali ukiwemo mfumo dume ,mila potofu na unyanyapaa wamekuwa hawasindikizi wake zao katika kliniki za afya ya uzazi na mtoto.

Mercy amesisitiza kuwa ni muhimu sana kwa wanaume wote kuhakikisha kuwa wanawasindikiza wenza wao katika kliniki za uzazi na mtoto  ili mwisho wa siku waweze kupata ushauri kwa pamoja .

Mercy amesema kwamba mke na mume wakishapata ushauri na kupimwa wakiwa pamoja, endapo mmojawao ama wote watagundulika kuwa na maambukizi ya VVU, kwa pamoja watapatiwa ushauri utakao waelimisha jinsi ya kumlinda mtoto wao na maambukizi ya VVU.


“Kutokana na wababa kuto wasindikiza wenzi wao katika kliniki za afya ya uzazi na mtoto,wanawake wengi wamekuwa wakipewa dawa za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,wanatumia kwa kificho na mwisho wa siku wanapojifungua hushindwa kuwalinda watoto wao na maambukizi ya VVU kwani wenzi wao wanakuwa hawajui kuhusu suala zima la hali ya afya ya mama na mtoto na hivyo wamama hushindwa kufuatilia njia sahihi za kuwalisha watoto zinazoshauriwa na wataalamu wa afya kwa watu wanaoishi na VVU.

Hata hivyo amesema kwamba wataalamu wapo na dawa zipo ,zote zinatolewa bure ni vyema wanaume wote wahamasike na wahakikishe kila mama anapokwenda kliniki anaambatana na mwenza wake na pia kupata ushauri mzuri kwa watoa huduma wa afya ili waweze kuinusuru Tanzania na kizazi kijacho na maabukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI.



No comments: