Meneja biashara wa Mamlaka ya maji safi na maji taka Tuwasa Bw.Benald Biswalo wakati akiangalia moja ya pampu mpya ya maji ambayo kwasasa inatumika kusukumia maji mjini Tabora.
Na Lucas Raphael,Tabora.
Maji - Tabora.
Mamlaka
ya majisafi na majitaka mjini Tabora (TUWASA) imeleta mita 3000 za
maji kwa ajili ya kuzifunga kwa wateja wa mamlaka hiyo mjini Tabora.
Meneja
Biashara wa mamlaka hiyo Biswalo Benard, amesema kuwa mita hizo
zimegharimu kiasi cha shilingi milioni 36 na kwamba lengo lake ni
kuhakikisha kuwa kila mteja analipa kiwango cha maji alichotumia hivyo
kuondokana na mfumo wa kadilio la malipo ambao alisema hauna tija.
Alisema
Mamlaka hiyo imelazimika kutumia mita hizo za plastiki kutokana na
kuepa athari zinazoendelea za biashara ya vyuma chakavu inayoendelea
nchini ambayo alisema imeipa hasara kubwa mamlaka hiyo kutokana na
miundombinu yake ikiwemo mita kuibwa.
Akiongea
katika ziara maalum ya kuitembelea Mamlaka hiyo, mkuu wa wilaya ya
Tabora, Suleiman Kumchaya, aliipongeza kutokana na jitihada kubwa
inazoendelea kuzifanya kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya
majisafi na taka katika manispaa ya Tabora.
Hata
hivyo aliitaka mamlaka hiyo ichukue hatua madhubuti za kulinda vyanzo
vya maji kwa kutunga sheria ndogo ndogo za kulinda rasilimali hiyo
muhimu kwa ajili ya uhai wa watu.
Hii
ni ziara ya kwanza ya mkuu wa wilaya ya Tabora, kuifanya katika mamlaka
ya majisafi na majitaka mjini Tabora (TUWASA) toka alipoteuliwa rasmi
kushika madaraka hayo miezi miwili iliyopita ambapo alitembelea mabwawa
ya Igombe, Kazima na kukagua shughuli za utandazaji wa mabomba ya maji
katika mitaa mbali mbali ya mji wa Tabora yenye urefu wa kilomita 27.
No comments:
Post a Comment