Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Ali Abdulla Ali akiwa na Makatibu wake wakitoka nje ya Ukumbi wa Baraza hilo baada ya kuahirisha kwa siku moja kikao cha baraza la Wawaklilishi jana asubuhi. Hatua hiyo imekuja kufuatia msiba uliolikumba Taifa baada ya ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyozama karibu na kisiwa cha Chumbe
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wabunge wa Muungano waliofika Zanzibar Kutoa mkono wa pole hapo katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Wawakilishi Mbweni kufuatia Ajali ya Meli ya M.V. Skagit. Ujumbe huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh. Shamsi Vuai Nahodha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua baadhi ya majeruhi wa M.V Skagit waliolazwa katika Hospiotali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema akitoa Taafifa ya uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit hapo Ofiosini Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwafariji baadhi ya Watalii na wageni waliokuwa wakija Zanzibar kwa Meli ya M.V. Skagit iliyopata ajali juzi mchana karibu na Kisiwa cha Chumbe. Kulia ya Balozi ni Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Mh. Hamad Masoud Hamad.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema akitoa Taarifa ya uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit hapo Ofiosini Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na Saleh Masoud Mahmoud – OMPR-ZNZ.
Na Othman Khamis Ame
Serikali ya Muungano wa Tanzania Kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa litaendelea kutoa ushirikiano na msaada kwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyotokea
jana mchana karibu na Kisiwa cha Chumbe.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh. Shamsi Vuai Nahodha
alitoa kauli hiyo wakati akitoa mkono wa pole kwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Taifa ya Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mh. Nahodha akiuongoza Ujumbe wa Wabunge 20 wa Bunge la Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kutoa mkono huo wa pole alisema Vikosi vya
Ulinzi mbali ya kusaidia operesheni hiyo pia litaendelea kuto msaada
wowote utaohitajika katika kurejesha hali ya kawaida kwa wahanga hao wa
ajali ya Meli.
Mh. Nahodha alisema maafa yaliyotokea jana yameigusa Jamii yote ya
Watanzania hivyo Wananchi wote wanapaswa kuzidisha juhudi zao katika
harakati zote za kurejesha hali ya utulivu na Amani.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi aliushukuru ujumbe wa Wabunge hao kwa kuguswa kwao na msiba huo
uliopelekea vifo vya Watu 53 hadi sasa.
Balozi Seif alisema wazamiaji pamoja na Vikosi vya Ulinzi bado
wanaendelea na operesheni ya kuwatafuta Abiria waliopotea kwenye chombo
hicho.
Alisema Serikali imechukuwa gharama za mazishi kwa Mazishi ya wale wote
waliokufa katika ajali hiyo sambamba na kuhudumia usafiri wa maiti
ambazo Familia zao ziko Tanzania Bara.
“ Hatupendi Meli zetu zizame lakini zinazama. Hatupendi Ndege zetu
zianguke lakini zinaanguka. Hiyo ni kudra ya Mwenyezi Muungu”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Hata hivyo Balozi Seif alieleza kwamba bado ipo tabia ya baadhi ya
wamiliki wa vyombo vya usafiri wa Baharini kusaidia kufuata taratibu za
usafiri zilizowekwa na mamlaka husika badala ya kutawaliwa zaidi na
Tamaa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa za kutembelea majeruhi
wa ajali hiyo wanaoendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja.
Balozi Seif alielezwa kwamba jumla ya majeruhi 80 waliokuwa wamelazwa
hospitalini hapo wamesharuhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata tiba.
Mmoja wa Majeruhi hao ambae ni mfanyabiashara Kitwana Makame Ali
ameipongeza Serikali na Vikosi vya ulinzi kwa juhudi zao za uokozi
zilizopelekea wengi kati ya wahanga hao kuokolewa.
Hata hivyo Mfanyabiashara Kitwana ameishauri Serikali kuhakikisha sheria
na taratibu za usafiri wa Baharini zinazingatiwa kwa lengo la kuepusha
ajali.
Baadaye Balozi Seif aliwakagua Wageni na Watalii waliookolewa ambao
walikuwa wakisafiri na chombo hicho hapo katika Hoteli ya Serrena Inn
Shangani Mjini Zanzibar.
Wageni hao 14 ni Paul Smeulders kutoka, Eline Van Nistelrooy, Jaap Van
Der Heyden, Joa Maouche, Inge Van Herwynen kutoka Uholanzi, Lauren Dent
na Hilary Strasburg kutoka Marekani, Arne Sohns kutoka Ujerumani, Joas
Gielen na Elvira Feyen kutoka Ubelgiji.
Wengine ni Bastiar Var Rennings,Lena Roker kutoka Ujerumani Chen Dagan
na Nitzan Bodenheimer kutoka Nchini Israel.
Akiwa Ofisini kwake Vuga Balozi Seif alikutana na Mkuu wa Jeshi la
Polisi Tanzania Ispekta General Said Mwema kupokea Taarifa ya jeshi hilo
tokea mwanzo wa harakati za uokozi wa janga hilo.
IGP Said mwema alimueleza Balozi Seif kwamba Jeshi la Polisi tayari
limeanza uchunguzi wa awali na hitilafu kadhaa zimejichomoza kutokana na
idadi halisi ya abiria waliokuwemo kwenye Meli hiyo.
Alisema mahojiano ya watu mbali mbali wakiwemo baadhi ya abiria
waliokuwemo kwenye chombo hicho pamoja na wahusika wa chombo chenyewe
Mjini Dar es salaam yanaendelea vyema.
Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.
Mohd Gharib Bilal amefanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mazungumzo hayo yalikuwa katika jitihada za kutoa mkono wa pole pamoja
na kutafuta mbinu za namna gani Serikali zote mbili zitaendelea
kushirikiana katika kukabiliana na Maafa hayo.
Dr. Bilal ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kushirikiana vyema na vikosi vyote vya Ulinzi kwa jitihada zao za haraka
zilizopelekea kuokoa idadi kubwa ya abiria waliokuwemo kwenye vyombo
hivyo.
No comments:
Post a Comment