RISALA YA
RAMADHANI YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI
WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA
DK. ALI MOHAMED SHEIN, KWA MWAKA
1433 HIJRIYA, 2012 MILADIA.
Assalam
Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh
Alhamdu Lillahi Rabil Alamin. Shukurani
zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa Viumbe vyote. Sala na Salam
zimshukie Aliyetukuzwa na Muumba wetu, Mtukufu wa Daraja aliyeletwa kwa Rehema
kwa ajili ya kuwaongoza waja wapate nusra ya Allah (Subhana Wataala).
Ramadhani tukufu imetufikia. Tuna
wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Azawajalla, kwa kutujaaliya umri tukaupokea Mwezi huu
Mtukufu, Mwezi wa Ibada, Mwezi wa Furaha, Mwezi wa Neema. Kubwa zaidi ni kuwa
huu ni Mwezi ambao kwa hekima zake Mola wetu ametuteremshia Quran, ambayo ndio “Uongofu kwa Watu” na yenye “hoja zilizo wazi za uwongofu na
upambanuzi”. Aidha, ametutengezea
usiku wa cheo kitukufu” usiku huo wa “Laylatul
Qadri ni bora kuliko miezi elfu”.
Ndugu
Wananchi,
Kutokana na neema hizi, sote
tunawajibika Kwake kwa vitendo. Hivyo basi, madhumuni ya risala hii ni
kuukaribisha Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani na kukumbushana baadhi ya mambo
tunayostahiki kuyafanya katika Mwezi huu Mtukufu ili tufanikiwe hapa duniani na
akhera twendako.
Wakati tunaukaribisha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhan, Mwenyezi Mungu ametupa mtihani wa maafa kwa kuzama meli ya MV SKAGIT
iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar. Hadi jana usiku Watu wapatao 31 wamefariki,
123 hawajaonekana baada ya meli hiyo kuzama na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watu
136 wameokolewa. Kuanzia asubuhi ya leo
hadi mchana huu jumla ya maiti 22 zimepatikana. Katika kipindi hiki tumuombe
Mola wetu atupe rehema zake, atughufirie makosa yetu na atujaalie subira.
Ndugu
Wananchi,
Mwenyezi Mungu ametupa maelekezo kamili
ya Mwezi huu Mtukufu katika Quran tukufu, surat Al-Baqara aya 183 hadi 187, aya
ambazo Mashekhe na Maimamu wetu wamekuwa wakizielezea tangu Mwezi wa Shaaban na
wanaendelea kutufundisha katika kipindi hichi na kutoa mawaidha yao.
Ndugu
Wananchi,
Mafanikio ya wanadamu duniani yanakuwa
makubwa kutokana na kuwa na mipango mizuri na madhubuti. Serikali zote duniani
zinaendeshwa katika mtindo huo wa kujipanga na sisi hapa Zanzibar tunafanya
hivyo hivyo. Mipango mbali mbali kama vile Mpango wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUZA), Dira 2020 na mengineyo ni miongoni mwa utaratibu huo.
Lakini mipango tu haiwezi kutuletea mafanikio bila ya kuwepo mikakati ya utekelezaji, usimamizi
mzuri na juhudi za utekelezaji. Wahenga
walisema “Mipango
si matumizi”.
Jitihada mbali mbali zimekuwa
zikifanywa na Serikali katika kuimarisha ustawi wa wananchi mmoja mmoja, vikundi na wananchi
wote kwa jumla tukiwa na lengo kuu la kuwapunguzia wananchi wetu ukali wa
maisha. Kwa mfano, Serikali imeamua kuwapunguzia gharama za Kilimo wakulima
wetu na kuimarisha huduma hiyo ili kuwasaidia wananchi kuongeza kipato chao na
kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi. Kadhalika, hatua hii
imelenga kupunguza tatizo la mfumko wa bei hasa kwa bidhaa za chakula.
Aidha, napenda kuwashukuru wakulima
wetu kwa kujiandaa kuwapa huduma nzuri wananchi wetu hasa katika upatikanaji wa
chakula kwa ajili ya futari. Naamini kuwa hisani, ukarimu na kuhurumiana vitazingatiwa
katika biashara na utoaji wa huduma kwenye kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani. Serikali nayo itajitahidi kufanya kila linalowezekana ili kuwasaidia
wananchi katika kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo
yetu. Ni imani yangu kuwa kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake ili tuweze
kutekeleza ibada zetu kwa wepesi huku nafsi zetu zikiwa zimeridhika. Tumuombe
Mwenyezi Mungu atushushie baraka zote za Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Ndugu
Wananchi,
Tumebahatika kuwa na kitabu cha Quran
na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Pamoja na
kuendesha ibada za Saumu, Sala na utoaji Sadaka katika mwezi huu, tutakuwa
tumejipangia vyema ikiwa tutazidisha kusoma na Quran pamoja na Hadith za Mtume
Muhammad, S.A.W. katika mwezi huu.
Kuporomoka kwa maadili ni miongoni mwa
matatizo yanayoikabili jamii yetu siku hizi. Sote tunaelewa madhara yake,
yakiwemo maasi, uhalifu, kutotii sheria na hata kuanguka kwa kiwango cha elimu
kwetu na kwa watoto wetu.
Tukirejea kwenye Quran na Hadith za
Bwana Mtume S.A.W. tutajisaidia kupata ufumbuzi wa kuondosha madhara haya
niliyoyagusia. Kwanza tukumbuke kuwa Quran Tukufu inanufaisha kila pahala na
kila zama. Aya na sura za Quran zimejaa hekima (Ishara) ya elimu, sayansi,
historia, maadili na kila fani. Kwa mfano, Aya ya 53 ya Surat FUS SWILAT, Juzuu
ya 24, inatuambia “Tutawaonesha Ishara zetu katika upeo wa mbali katika nafsi
zao wenyewe mpaka inabainika kwamba haya ni kweli. Je haikutosha kwamba Mola
wako yeye ni Shahidi wa kila kitu?”
Kuhusu elimu katika mwezi kama huu
iliteremshwa sura ya amri ya kusoma, aya ya kwanza ya Qurani, iliyosema:
“Soma
kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba binaadam kutoka tone la damu. Soma!
Na Mola wako ni karimu kushinda wote. Ambaye, amefundisha kwa kalamu.
Kamfundisha mtu aliyekuwa hayajui!
Aya hizi zinatuhimiza wajibu wa elimu,
zinatufundisha sayansi ya maumbile na zinatupa maarifa ya manufaa ya elimu na
utamaduni, yakiwa ni funguo za maendeleo kwetu katika nyakati zote.
Ndugu
Wananchi,
Elimu hii haipatikani bila ya
kuitafuta. Tukumbuke kuwa Quran imeeleza katika Surat Ibrahim, Aya ya kwanza
kuwa:
“Hiki
ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu kwenye kiza uwapeleke kwenye
mwangaza kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye Nguvu na
Msifiwa”.
Ndugu
Wananchi,
Nawasihi muutumie muda mwingi kuisoma
na kupata maarifa ya Quran katika Mwezi huu, mafunzo ambayo yatadumu siku zote.
Tukumbuke usemi wa Sayyidna Muhammad, Alayhi Salam kwamba:
“Asiyekuwa
na chembe ya Quran moyoni mwake ni kama nyumba iliyobomoka”.
Imani zetu zitajengeka na maadili yetu
mema yatarejea tutakapoisoma na kujifunza Quran na kuwa wakweli katika maisha
yetu ya uongozi na ya kuongozwa. Uelewa wetu utayageuza maisha yetu katika njia
sahihi. Baadhi ya wanazuoni wanasema “Elimu
bila ya vitendo ni kama mti usiotoa matunda”. Hivyo tuazimie kuyatumia
mafunzo ya Ramadhani katika maisha yetu yote ya kawaida kama ni matunda ya
Saumu. Matunda ambayo ni muhimu kwetu.
Ndugu Wananchi,
Serikali
yetu imo katika juhudi za
kuwaandalia wananchi wake maisha bora, kwa kupitia mageuzi ya katiba na
pia kwa kuhesabiwa
watu, mambo yaliyomo katika sheria zetu. Quran na Hadithi za Bwana Mtume
S.A.W
zinatufundisha mshikamano, umoja na utiifu wa sheria. Ni vyema kufahamu
na kuzingatia usafi wa nia (IKHLAS) ili tuwe watu wema na
wenye kupenda amani na tusiokuwa na hasada au kupenda kutukuzwa.
Ndugu zangu nyote ni mashahidi ni
mashahidi kuwa nchi yetu inaendelea kupata mafanikio. Uchumi wetu umeendelea kukua licha ya kuwepo
kwa changamoto kadhaa. Wananchi na viongozi tumeshikamana kwa lengo moja la
kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi yetu. Nakunahini nyote tuendelee
kushikamana, tuendelee kutii sheria na kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjifu
wa amani.
Tujikumbushe Surat Al – Imran, Aya 103
inayosema:
“Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala
msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu; vile
mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema
yake mkawa ndugu”.
Ndugu
Wananchi,
Tuutukuze Mwezi huu wa Ramadhani kwa
kukumbuka mafundisho hayo ya Quran na tuendeleze shughuli zetu za kimaisha
katika hali ya amani, utulivu na mshikamano. Pamoja na hayo, tufanye biashara
kwa misingi ya kutodhulumiana katika
bei, viwango na vipimo.
Kuhusu hili la biashara, sote
tunakubaliana kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wa neema kibiashara. Lakini ni vyema kufanya neema hii iwe kwa
wauzaji na kwa wanunuzi. Muuzaji anauza
bidhaa zake nyingi zaidi, kwa hivyo anapaswa kuhakikisha zina ubora na anachuma
faida kwa kiasi ya anachouza. Mnunuzi naye
anahitaji kupewa bei iliyo nafuu, hasa kwa bidhaa ambayo Serikali imeipunguza
kodi, kwani Serikali yenu kama kawaida itapunguza ushuru kwa bidhaa muhimu za
chakula ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa bei.
Wakati huo huo, ni jambo la kusikitisha
kuona baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa wanasafirisha bidhaa kama vile
unga, sukari na mchele waliotozwa kodi ya chini na kuzisafirisha kwa njia ya
magendo nje ya Zanzibar ili wapate faida kubwa.
Kwa hakika jambo hili linasababisha upungufu wa baadhi ya vyakula na kuwasababishia
shida wananchi wakati huu wa mwezi wa Ramadhan.
Tunapaswa kuwa waadilifu katika hili na pia katika kuhakikisha vipimo
vya kuuzia ni vya halali. Serikali
imeweka mazingira mazuri ya biashara hasa katika Mwezi huu Mtukufu na ni wajibu
wetu kuyatumia vyema ili tunufaike sote.
Kama kawaida Serikali itakuwa macho kuona biashara inaendeshwa kwa
mujibu wa sheria na kujali maslahi ya wananchi.
Natoa wito tuwe watendaji wema na
ihsani baina yetu na hasa kwa masikini na wasiojiweza. Utoaji sadaka ni jambo la msingi na hatuna
budi kulizingatia zaidi katika Mwezi huu, ili wenzetu wenye kipato cha chini
nao mwezi huu wa Ramadhan uwe ni mwezi wa furaha kwao. Ramadhan Karim – basi tuwe na ukarimu kwa
wenzetu na wageni wetu.
Aya 29-30 ya Surat Faatir inasema: “Hakika
wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakashika sala, na wakatoa kwa siri
na kwa dhahiri katika tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyobwaga; ili
yeye amalize ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake.
Hakika yeye ni mwenye kusamehe, Mwenye shukurani”.
Nawasihi ndugu zetu wafanya biashara,
wakulima, wavuvi na wahusika wote kuzingatia mambo hayo ili sote tuwe tumepata
nafuu. Kutokana na hali nzuri ya hewa natumai tutakuwa na mwezi wa neema.
Ndugu
Wananchi,
Kwa kuwa Ramadhani mwaka huu imetujia
katika msimu wa Watalii na ziara za Wazanzibari wenzetu wanaoishi nchi za nje,
tunapaswa kwa umoja wetu kuwaonesha wema wetu na mambo mema kwao. Tudumishe
sifa yetu ya ustaarabu, uvumilivu na ustahamilivu, tushikamane nao na
tuwaelimishe kwa upole kwa yale wasiyoyajua ya mila zetu. Tudumishe amani na
tuhakikishe usalama kwa watu wote, hasa nyakati za usiku ambapo watu wengi
wanakwenda misikitini kufanya ibada za Mwezi wa Ramadhan.
Sote kwa pamoja tujitahidi kuweka mitaa
yetu katika hali ya usafi na Mamlaka zinazohusika na usafi ziongeze bidii
kusafisha maeneo ya makazi na matembezi ya watu.
Tujitahidi kuzingatia mafundisho ya
dini katika kupata ukamilifu wa saumu zetu. Wananchi wengine wasiowajibika na
saumu kama kawaida watoe ushirikiano na wawe wastahamilivu kwa wenzao
wanaofunga. Wale wasiowajibika kufunga kwa sababu mbali mbali wajitahidi
kutumia fursa hii vyema bila ya kuwakirihisha wengine. Kwa upande wa madereva
na watumiaji wote wa barabara tuzingatie usalama barabarani hasa wakati wa
jioni ambapo watu wengi huwa wanakimbilia kuftari.
Jeshi letu la Polisi litaendelea
kuimarisha ulinzi wa watu na mali zao kwa kushirikiana na vijana wa ulinzi
shirikishi ili wananchi wapate utulivu na watekeleze saumu kwa amani. Ni wajibu
tushirikiane na Jeshi letu la Polisi katika kulifanikisha suala hili.
Ndugu
Wananchi,
Kwa kumalizia, napenda kugusia mambo
mawili. Kwanza ni kwa wazazi na walezi kuzisimamia zaidi nyenendo za watoto wao
katika Mwezi huu na kuwahimiza zaidi katika ibada na darsa. Pili, kwa vile
tunakabiliwa na msimu wa Hijja, basi ni vyema kwa wanaofanya safari za Hijja
kuwa na ushirikiano wa karibu ambao utaleta manufaa kwa wenye kukusudia
kutekeleza ibada ya Hajji na Umra. Mwenyezi Mungu awape taufik wote na
awafikishe kutimiza azma zao na kuwarejesha nyumbani kwa salama.
Namuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe
kutekeleza ibada za Saumu na nyenginezo katika hali ya umoja, mshikamano, amani
na utulivu. Atuongezee mapenzi baina yetu ili
tuzidi kuhurumiana. Atufanyie wepesi
katika kupata riziki za halali na kumshukuru Mola wetu. Tunamuomba Mola wetu atuzidishie
imani zetu kwake na tuwe wenye kujali maslahi ya wenzetu na tuwe watu wa
kufanya ihsani ili tupate mavuno ya mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
R
A M A D H A N K A R I M
Assalam
Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh
Ahsanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment