Na Hastin Liumba,Tabora
NAANZA kwa kuwasalimu watanzania wenzangu, kwani si kwa bahati mbaya
Mungu kutuweka Tanzania nchi ambayo, Mungu ameipendelea sana katika
dunia hii.
Nawasalimu viongozi wa serikali, viongozi wa dini, madhehebu na wenye
mamlaka katika nchi hii.
Hayo ni maneno ya Mtumishi wa Mungu, Stanley Mteule Rweyemamu,
mwinjilisti wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania Tumbi, mkoani
Tabora, alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa makala hii katika kata ya
Tumbi iliyoko nje ya manispaa Tabora.
Rweyemamu anasema kuwa, anatumia nafasi yake, kuwakumbusha watumishi
wa Mungu wote hasa wenye uhakika na wito wao kwa Mungu wao bila kujali
madhehebu yao, huduma zao wala umaarufu wao, kwamba Tanzania
ilipofikia leo watumishi wa Mungu tumechangia kwa kiasi kikubwa.
Mwinjilisti alisema wachache kama si wengi wanaweza wasinielewe kwa
haraka kwamba ni kwa namna gani watumishi wa Mungu wamechangia
kuifikisha Tanzania mahali ilipo leo!.
Rweyemamu, alisema sasa hakuna heshima kabisa katika nchi yetu, hakuna
mkubwa wala mdogo, mwenye mamlaka na asiye na mamlaka.
Anaongeza watu wanauana kirahisi tu tena kama kuku kwa kukatana
mapanga na risasi na kila mtu anasema kwa jinsi anavyojisikia tu.
Mwinjilisti huyo anabainisha kuwa baba ni baba tu, hata kama ni mfupi
kiasi gani,mwembamba kiasi gani , maskini kiasi gani au uwezo wake wa
kufikiri ni mdogo kiasi gani bado ataitwa Baba.
Aidha anasema kuwa hakuna heshima kwenye matumizi ya zawadi tulizopewa
na Mungu hasa katika hizi zinazoonekana kama madini,makaa ya mawe, na
jana tu Mungu ametuongezea nyingine ya gesi.
Anaongeza kuwa,zipo nyingi na zingine Mungu ataendelea kuziweka wazi
siku hadi siku, je kuna heshima katika matumizi ya zawadi hizi? Na je
wanajua vyote hivi ni zawadi toka kwa Mungu?
‘‘Watumishi wa Mungu kumbukeni na kukubali kwamba kukosekana kwa
heshima katika nchi hii ni sehemu kubwa watumishi tumechangia.......
tulipoona dhambi, uchafu na makosa sehemu mbalimbali katika idara za
serikali na ndani ya jamii tulichukua hatua gani kama watumishi wa
Mungu?’’.alisisitiza.
Alisema nakumbuka katika karne ya 11 na 12 kanisa, ( watumishi Mungu)
lilikuwa na heshima kubwa mno ( utisho) kwani hata mwizi alipokimbilia
kanisani au mikononi mwa watumishi wa Mungu, maaskari waliogopa
kumfuata ndani ya kanisa na kwa namna hiyo alipona na kusamehewa!
Anaongeza zaidi kuwa jaribu kukimbilia huko kwa sasa uone maaskari
watakavyo kufuata watakavyo shukuru kwa kuwapunguzia kazi.
Aidha anabainisha zaidi kuwa, Kanisa lilikuwa na mazungumzo na
serikali na kusikilizana na kuwa pamoja na kwamba Serikali ilitegemea
sana moani na mashauri ya watumishi wa Mungu? Bila shaka ni wachache
sana na inabidi kujiuliza kwa nini hali hii imetokea sasa.
‘’Watumishi wa Mungu walikemea dhambi, uchafu na makosa yaliyokuwa
wazi na yaliyojificha Mungu wao aliwaonyesha’’.alisema mwinjilisti
huyo.
Alisisitiza kuwa watumishi wa Mungu, walikemea kwa ujasiri mkubwa mno
na walipokemea walisikilizwa na wengi wao waliacha dhambi, uchafu na
makosa yao kwa sababu waliamini kwamba Mungu amewakemea.
Hata hivyo anafafanua kuwa hali hiyo ilitokana na watumishi wa Mungu
kuwa kama kioo na mfano wa kuigwa siku kwa siku.
Alisema kuwa huwezi kudai haki wakati wewe uko nje ya haki, lakini pia
huwezi kuhitimu masomo pasipo kwenda shule na kufanya mtihani, dhambi
,uchafu na makosa yanayotajwa mara kwa mara kwa viongozi mbali mbali
wa serikali kama Ufisadi,Uuzaji wa madawa ya kulevya, kutumia madaraka
vibaya,uchawi na ushoga, na mengine yanayofanana na hayo yametajwa pia
kwa watumishi wa Mungu ( Kanisa) .Je, nani amkemee mwenzake au nani
amsikilize mwenzake na kuacha?.
Anasisitiza kuwa, hapa ndipo tatizo lilipo na lilianza polepole na
sasa limekuwa kubwa na matokeo yake ni kuendelea kutiana moyo tu ili
kuendelea katika upotevu na nani amkee mwenzake, Wote tumetenda dhambi
na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (Rumi 3: 23), ndio maana heshima na
adabu katika nchi yetu vimepotea kabisa.
‘‘Kupotea kwa heshima na maadili kumechangiwa na watumishi wa Mungu
kwani wao ndio wameanza kuipoteza na wengine wamefuata ndio maana
tuko hapa tulipo sasa..... enyi makuhani amri hii yawahusu ninyi ,kama
hamtaki kusikia na kama hamtaki kuitia moyoni ili kulitukuza jina
langu, asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami
nitazilaani Baraka zenu; naam nimekwisha kuzilaani kwa sababu hamyatii
haya moyoni ( Malaki 2:1-2).
Anaongeza zaidi kuwa, Yesu anasema uyaonapo haya ( kukosekana kwa
heshima na maadili katika Taifa lolote duniani), yanaanza kutokea,
Changamkeni kuukimbilia Wokovu.
Alisema watumishi wa Mungu changamkeni katika kutubu na kughairi
dhambi, uchafu na makosa , kisha tuwaongoze viongozi na wenye mamlaka
wote katika Tanzania na mwisho tuwaongoze watanzania wote kutubu na
kughairi dhambi,uchafu na makosa pasipo kunyosheana mikono (Luk 21:
28).
‘‘Maana yake tuanze kutubu watumishi wa Mungu kwanza , ndipo viongozi
mbalimbali na mwisho watanzania wote kwa ujumla .......watumishi wa
Mungu tukiwa safi nina uhakika tukikemea dhambi , uchafu na makosa kwa
wenzetu huku sisi tukiwa ni kioo na mfano wa kuigwa tutasikiwa na watu
wataacha dhambi, uchafu na makosa ambayo yamelifikisha Taifa la
Tanzania pabaya.
Alisema hii ni hatua kwa Taifa letu la Tanzania, tuache kunyoosheana
vidole na kutuhumiana kila kukicha bali sasa tuchukue hatua ya moyoni
kabisa kutubu na kughairi dhambi ,uchafu na makosa tuliyofanya ,
tunayofanya na tuliyokusudia kufanya.
Aliongeza kuwa tuondokane na watanzania wachache kufaidi nchi ya
Tanzania peke yao kana kwamba ni ya kwao peke yao, hatua hii inawataka
viongozi wa dini kwanza pasipo kujitetea kwamba mimi sijawahi kutajwa
katika dhambi ,uchafu na makosa yoyote.
Aidha anasema kuwa ,anawasihi kwa pamoja tuchukue maamuzi
wanaangamizwa kwa kukosa maarifa mtu wa kwanza wa Mungu ni mtumishi
wake na wakisha angamizwa wao, basi taifa limekwisha Hosea 4:6.
Kwa sababu ya kuzubaa na kukosekana kwa maarifa taifa la Tanzania
limefika hapa lilipo leo, sasa tuchangamke ili kulikomboa taifa letu
sasa.
‘‘Binadamu ayeumbwa na Mungu tena kwa mfano wa Mungu hamwogopi tena
Mungu muumba wake..... hofu ya Mungu imepungua sana kwa binadamu kiasi
kwamba wanafanya kwa jinsi wanavyojisikia tu.’’
Alifafanua kuwa hali hiyo ni kama achinjwavyo ngombe ndivyo sasa
mwanadamu anavyomchinja binadamu mwenzake tunakenda wapi ni nani aliye
na busara naye atayajua kwa maana njia za bwana zimenyoka nao wenye
haki watakwenda katika njia hizo bali wasiio wataanguka ndani yake,(
Hosea 14:9).
Je watumishi wa Mungu tumeasi? wakati uliokubalika ni sasa wa
kulikomboa taifa la Tanzania, Changamka! mtumishi wa Mungu Habakuki,
(Habakuki 3:12), anasali na katika sala yake anamsihi Mungu afufue
kazi yake ya kukomboa na katika ghadhabu yake akumbuke rehema.
‘‘Ee Mungu nakusihi fufua kazi yako ya ukombozi katika taifa la
Tanzania, ili tupate kufaidi wote zawadi ulizotupa katika Taifa letu
na ukumbuke kuendelea kurehemu siku kwa siku .
No comments:
Post a Comment