Pages

KAPIPI TV

Thursday, May 3, 2012

MAFUNZO YA UFUNDI MCHUNDO YAFANYIKA MWANZA

Katibu Tawala Msaidizi - Mkoa wa Mwanza Bw. Ndaro Kulwijila akifungua mafunzo kwa mafundi Mchundo kuhusu njia bora za kuhudumia majokofu na Viyoyozi na umuhimu wa kuhifadhi tabaka la Ozoni. Mafunzo hayo ya siku mbili yameratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na yanafanyika Jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Mafundi Mchundo wa Majokofu na Viyoyozi kutoka viwanda mbalimbali vya Jiji la Mwanza wakisikiliza kwa makini umuhimu wa kuhifadhi tabaka la Ozoni
Katibu Tawala Msaidizi - Mkoa wa Mwanza Bw. Ndaro Kulwijila wa pili kutoka kushoto (waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mafundi Mchundo wa Majokofu na viyoyozi kutoka katika viwanda mbalimbali vya jiji la Mwanza waliohudhuria mafunzo ya njia bora za hifadhi ya tabaka la Ozoni. Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka VETA Mwanza na VETA Kigoma.
Na Lulu Mussa 
Afisa Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais

Mwanza
Imeelezwa kuwa Tanzania imefanikiwa kuondoa matumizi ya kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka tani 254 mwaka 1999 hadi tani 35.76 mwaka 2009. Hayo yameelezwa leo Jijini Mwanza na Bw. Ndaro Lulwijila, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza katika hotuba ya ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya mafundi mchundo kuhusu teknolojia mbadala ya majokofu na viyoyozi.
Bw. Kulwijila ameainisha baadhi ya kemikali hizo kuwa ni methyl bromide, halons na chloroflorocarborns ambazo hutumika kama vipozi katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya  kuzima moto, usafishaji chuma, ufukizaji wa mazao katika maghala na utengenezaji wa magodoro ambazo huleta madhara kwa tabaka la ozoni na adhari zake hutokea kwa binadamu, mimea na viumbe hai.
Amezitaja athari za uharibifu wa tabaka la ozoni kuwa ni kuongezeka kwa magonjwa ya saratani ya ngozi,uharibifu wa macho maarufu kwa jina la mtoto wa jicho, na upungufu wa uwezo wa mwili kujikinga na maradhi.  Athari hizi kwa kiasi kikubwa zinatokana na shughuli za kibinadamu kama vile matumizi ya kemikali haribifu na zisizo rafiki kwa mazingira.
Bw. Kulwijila amewataka wanahabari kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya athari hizi ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali kudhibiti uingizaji wa majokofu yaliyotumika. Jitihada za Uhifadhi wa tabaka la ozoni umetokana na utekelezaji wa Mkataba wa Montreal na Vienna ambayo Tanzania iliridhia mwaka 1993.
Warsha hiyo imeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais imehusisha washiriki kutoka, Chuo cha ufundi VETA - Mwanza na Kigoma, wanahabari, Maafisa mazingira wa Mkoa wa Mwanza na mafundi mchundo kutoka viwanda mbalimbali vya Jiji la Mwanza.

No comments: