ACP ANTHONY RUTHA:Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora akiwa ofisi kuu ya Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora. |
MAUAJI
Watu ambao hawajaweza kufahamika mara moja wamemuua kwa kumpiga risasi Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Bw.Mashaka Kaliyuwa majira ya saa saba usiku akiwa nyumbani kwake Ipuli manispaa ya Tabora.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha,amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo amedai kuwa uchunguzi wa awali umeonesha kuwa ni tukio linalohusishwa na masuala ya kisasi ingawa bado jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.
Alisema kutokana na maelezo waliyoyapata toka eneo la tukio,wauaji hao walivamia nyumbani kwa mwenyekiti huyo wakiwa na bunduki ambapo kabla ya kuingia ndani walifyatua risasi hewani na baadaye kuingia ndani ambako walitekeleza mauaji hayo kwa kumpiga risasi tumboni Mwenyekiti huyo ambaye kwa sasa ni marehemu.
Akifafanua zaidi wakati akiongea na waandishi wa habari wanaofuatilia tukio hilo la kuhuzunisha,Kamanda Rutha alisema mbali na kumpiga risasi Mwenyekiti huyo wauaji hao pia walimjeruhi kwa kumkata panga kichwani walipokuwa wakimwamuru kutoa fedha walizodai kuwa ni mali yao.
"Kwakweli tukio hili hatuwezi kusema kuwa ni majambazi kwani hapo nyumbani kwake marehemu kuna vitu vingi vya thamani lakini hawakuvichua na kisha walipokuwa wakidai hizo fedha zao pia walimwambia marehemu kuwa ni lazima wamuue"alisema kamanda Rutha.
Hata hivyo mauaji hayo pia yameendelea kuzua minong'ono ya hapa na pale yakihusisha wadhifa aliokuwa akiutumikia ingawa hakuna anayethibitisha ukweli hadi sasa.
No comments:
Post a Comment