Pages

KAPIPI TV

Monday, February 27, 2012

SAKAYA,MTATIRO WAWATIA MACHUNGU TABORA..."Ni kuhusu uchumi na umasikini unaowakabili"

JULIUS MTATIRO:Naibu katibu mkuu Tanzania bara wa Chama cha Wananchi CUF alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tabora mjini katika viwanja vya Salama Guest.
Mh.MAGDALENA SAKAYA:Mbunge wa vitimaalum mkoa wa Tabora akizungumza na wananchi wa Tabora mjini.


Baadhi ya wananchi wa mjini Tabora wakiwa wameshika vichwa baada ya kuzungumziwa masuala ya uchumi na umasikini unaowakabili hali ambayo iliwatia simanzi.


Baadhi ya wakazi wa mjini Tabora wamejikuta wakitokwa na machozi wakati walipokuwa wakiwasikiliza viongozi wa  juu wa Chama cha Wananchi Cuf,mbunge wa vitimaalum mkoa wa Tabora Mh.Magdalena  Sakaya na Naibu katibu mkuu bara wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara ambapo kwa sehemu kubwa ya hotuba zao zililenga masuala ya uchumi na umasikini unaowakabili watanzania.

Hali  hiyo  ilitokana  na  viongozi  hao kudai kubainisha  kuhusu  hali  ya  uchumi  na  umasikini unaowakabili wananchi  wakiwa  ndani  ya  nchi  yao  yenye rasilimali  za  kutosha  ikiwemo madini,misitu na mengineyo  ambapo  fursa  na  rasilimali  hizo zimekuwa  zikitumiwa  na  wajanja  wachache kwa manufaa yao binafsi.     

Katika  kulifafanua  hilo  Mh.Sakaya   aliweka  bayana  na  kuitaka  serikali  kuwasaidia  wananchi  katika  nyanja  mbalimbali  huku  akiiangazia  zaidi  sekta  ya  kilimo  ambayo kimsingi  ndiyo  mkombozi  kwa  mwananchi  wa  kawaida.

Alisema  bado  anashangazwa  na  serikali  kuona  kuwa  haiwajali  wakulima  licha  ya  kuanzisha  programu  ya  Kilimo  kwanza  ambayo  inadaiwa  kuwa  ndio  ingekuwa  na  uwezo  wa  kumuinua  mkulima  mwenye  kipato  cha  chini  lakini  badala  yake  imekuwa ni  kinyume  na  hivyo  huku  akipigia  mfano  kwa wakulima  wa  zao  la  Tumbaku  ambao  kwasasa  bado  wataendelea  kuwa  masikini  wakutupa.

 ''Pale Dodoma serikali imeweka matrekta ambayo inadai kuwa itawakopesha wakulima lakini chakushangaza hadi  sasa hakuna  mkulima  anayekopeshwa  na sasa yanazidi kuchakaa  na mengine mpaka yanaibiwa vipuri"alisema  Mh.Sakaya

Aidha  ameitaka  serikali kuwa  na  dhamira  ya  dhati  katika  kumsaidia  mkulima  na  hasa  kwa  kuangalia  upya  mifumo  na  sera  zinazosimamia  kilimo  pamoja  na  utekelezaji  wake na si  kukalia  mipango  iliyoko kwenye  makaratasi  wakati  utekelezaji  ukiwa umekumbwa  na  wimbi  la  ufisadi ambao  unanufaisha  wajanja  wachache.

Sambamba na hilo  Mh.Sakaya  aliwaeleza  wananchi  kuwa  serikali  inayoongozwa  na  Chama  cha  Mapinduzi  imeshindwa  kuwajali  wananchi  kwa  kile  alichodai  kuwa  kutotimiza  ahadi  zake  katika  kuwahudumia  wananchi huduma  mbalimbali zikiwemo  za  afya  na  nyinginezo licha  ya  kuwa  inaendelea  kukusanya  kodi  kwa  wananchi  hao.

Kwa  upande  wake  Naibu  katibu  mkuu  bara  wa  Cuf  Bw.Julias Mtatiro  pamoja  na  kuzungumzia  masuala  kadhaa  yanayohusu  uchumi  na  namna  baadhi  ya  viongozi  wa  Serikali  kupitia  Chama  cha  Mapinduzi  walivyoshiriki  kudidimiza  uchumi  wa  Taifa  kwa  kuingia  mikataba  mibovu  ya  madini  na  mingineyo  aliwataka  wananchi  kuepuka  dhana  ya  kuwa  umasikini  wa  watanzania  ni  mipango  ya  Mwenyezi Mungu.

Alisema  umasikini  wa  watanzania  unatokana  na  mipango au  sera  mbovu  ambazo  kwa  sehemu  kubwa  pia  zimekuwa  zikilenga  kuwanufaisha  wawekezaji  na  sio  wazawa  jambo  ambalo  bado  litaendelea  kuwa  ni  tatizo  hapa  nchini huku  akilielezea  kuwa  suluhisho  lake  ni  kupatikana  kwa katiba  mpya.

Aidha  amewataka  wananchi  kujitokeza  kwa  wingi  kutoa  maoni  yao  wakati  wa  mchakato  wa  kutafuta  kuundwa  kwa  katiba  mpya  jambo  ambalo  litasaidia  kuwezesha  matatizo  waliyonayo  kuwasilishwa  kwenye  katiba  hiyo ili  yaweze  kupatiwa  ufumbuzi.







No comments: