Pages

KAPIPI TV

Monday, February 8, 2016

HALMASHAURI KALIUA YASHINDA KESI DHIDI YA MKANDARASI

Na Allan Ntana, Kaliua 
 MAHAKAMA ya wilaya ya Urambo Mkoani Tabora imetupilia mbali shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na Mkandarasi (Kampuni ya SARAM ya jijini Dar es salaam) ikipinga kusimamishwa na halmashauri ya wilaya ya Kaliua kuendelea na mkataba wake wa ujenzi wa miradi 4 ya halmashauri hiyo. 

 Akitoa taarifa kwa madiwani katika kikao kilichoketi jana katika ukumbi wa Milenia mjini Kaliua Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Athuman Kihamia alisema mahakama imesikiliza shauri hilo na kujiridhisha pasipo shaka kuwa Mkandarasi huyo alikiuka makubaliano ya mkataba wake na hivyo kutupilia mbali pingamizi lake. 

 Alisema baada ya Mkandarasi huyo kusimamishwa na halmashauri kuendelea na mkataba wake katika miradi 4 alifungua shauri katika mahakama hiyo akipinga maamuzi hayo ikiwemo kuweka zuio kwa halmashauri hiyo kutofanya shughuli yoyote ile katika miradi iliyokuwa inatekelezwa kwa mujibu wa mkataba. 

 ‘Waheshimiwa madiwani napenda kuwataarifu kuwa Januari 20 mwaka huu mahakama imetengua pingamizi lililowekwa na Mkandarasi SARAM na ilituagiza Mkurugenzi (mwajiri) na Mkandarasi (mwajiriwa) tukae pamoja na kufanya tathmini ili kujiridhisha kama ana madai yoyote kwetu na tutoe taarifa ndani ya siku 14’, alisema Kihamia. 

 Alifafanua kuwa licha ya Mahakama kutoa maelekezo hayo ya kukutana pande zote mbili, Mkandarasi huyo hajaonekana hadi sasa na siku 14 zimeshaisha hivyo akabainisha kuwa watakachofanya sasa ni kufanya tathmini wao wenyewe na kupeleka taarifa mahakamani ili mchakato wa kutafuta mkandarasi mwingine uanze mara moja. ‘Ukweli mahakama imetenda haki kwani kuzuia miradi ya maendeleo isiendelee kisa tu mkandarasi katimuliwa ni kuchelewesha maendeleo ya wananchi, nimepokea uamuzi wa mahakama kwa furaha kubwa’, aliongeza. 

 Miradi iliyokuwa inatekelezwa na mkandarasi huyo ni ujenzi wa ofisi ya 
Mkurugenzi wa halmashauri, jengo la wagonjwa wan je (OPD), nyumba 4 za watumishi na jengo la maonyesho ya nane nane eneo la Ipuli katika manispaa ya Tabora. Akizungumzia hukumu hiyo Mwanasheria wa Mkoa wa Tabora Richard Lugomela aliyesimamia kesi hiyo alisema mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa pingamizi la mkandarasi huyo halina tija kwa maendeleo ya halmashauri kwani alishindwa kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika mkataba wake wa awali. ‘Mkandarasi yeyote anayepewa mkataba wa kutekeleza mradi fulani anapaswa kuwajibika ipasavyo kama mkataba unavyotaka, katika miradi ya maendeleo tunahitaji mkandarasi mwenye uwezo na kasi na amalize kwa wakati si vinginevyo’, alibainisha.

No comments: