Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Hamisi Seleman |
Na Allan
Ntana, Tabora
JESHI la
Polisi mkoani Tabora limetoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo
wachungaji, mapadre, mashekhe, viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na
wengineo kusaidia kuelimisha jamii umuhimu wa kudumisha amani katika maeneo yao
ili kutokomeza vitendo vya mauaji ya raia.
Rai hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi
mkoani hapa ACP Hamis Selemani alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari
juu ya mauaji ya watu 17 yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo mbalimbali
mkoani humo.
Alisema
vitendo vya mauaji vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku katika maeneo tofauti
tofauti chanzo kikubwa kikiwa ni imani za kishirikina, wivu wa kimapenzi, tamaa
ya mali na uhasama baina ya familia na familia.
Alieleza
kuwa katika kipindi cha siku 15 tu kuanzia tarehe 10 hadi 24 Agosti mwaka huu
wananchi wapatao 17 wameuawa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za
miili yao matukio ambayo ni ya kusikitisha na yanahatarisha amani ya wananchi
kwa kiasi kikubwa.
‘Naomba watumishi
wa Mungu wa dini na madhehebu mbalimbali watusaidie kueneza neno la Mungu kwa
waumini wao ili wawe na hofu itakayosaidia kukomesha vitendo hivyo vya mauaji
ya raia wasio na hatia, naomba sana tushirikiane kurejesha amani katika jamii’,
aliasa.
Aidha
aliwataka viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo watendaji wa vijiji na kata
kusaidia kuelimisha jamii ili kukomesha vitendo hivyo vya kujichukulia sheria
mkononi kwani vinachochea uvunjifu wa amani kwa wanajamii.
‘Watu hawana
huruma kabisa, hata imani kwa Mungu hawana, wamekuwa kama wanyama, naomba sana
ndugu zangu watumishi wa Mungu tushirikiane kuielimisha jamii ili waachane na
chuki zisizokuwa na maana, tunataka kukomesha mauaji ya aina zote’, aliongeza.
Aidha
Kamanda Selemeni alizitaka taasisi zote za kifedha zilizopo hapa nchini
kuhamasisha jamii umuhimu wa kutunza fedha zao benki kwa usalama zaidi kuliko
hali ilivyo sasa ambapo wananchi wengi hususani wale wa vijjini wamekuwa na
tabia ya kutunza fedha zao majumbani hali inayochochea vitendo vya wizi.
Akizungumzia
mauaji yaliyotokea mwishobi mwa wiki Kamanda alisema, mnamo tarehe 23 Agosti
mwaka huu katika kitongoji cha Mtakuja kijiji cha Mwanzugi kata ya Nsenda
tarafa P wilayani Urambo aliuawa Kashindye Majebele (45) msukuma kwa kukatwa
shingo na kisu chenye ncha kali kwa imani za kishirikina.
Katika
mauaji hayo msako wa jeshi la polisi ulifanikiwa kumtia nguvuni Hamis Lwangamko
(55) msukuma ambaye ni mkulima wa Kamgembya na yupo mahabusu.
Aidha wauaji
hao pia inadaiwa waliwaua kwa kuwachoma moto Shija Madobo (80) mkazi wa kijiji
cha Kamgembya tarafa ya Urambo wilayani Urambo ambaye ni mume wa Kashinje Majebele,
Charles Shija (30) msukuma mkazi wa kijiji cha Msumbiji na Hamis Kingamkono
(55) mnyamwezi mkazi wa Kamgembya.
Alitaja
watuhumiwa wengine waliokamatwa kwa mahojiano zaidi na jeshi hilo kwa
kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wenzao kuwa ni William Seni (68) msukuma mkazi wa kijiji cha
Azimio, Paul Maduka (38) msukuma mkazi wa kijiji cha Mtakuja na Zungu Ng’wandu
(65) msukuma mkazi wa kijiji cha Kasisi.
No comments:
Post a Comment