Pages

KAPIPI TV

Monday, July 6, 2015

WATANO CHADEMA WAJITOKEZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA TABORA MJINI

Na Mwandishi wetu, Tabora

WANACHAMA watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wametia nia
rasmi ya kuingia katika kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa katika
UKAWA ili kuwania ubunge katika jimbo la Tabora mjini linaloshikiriwa
na Ismail Aden Rage wa CCM.

Watia nia hao wametambulishwa jana katika mwendelezo wa mikutano ya
hadhara iliyoandaliwa na uongozi wa chama hicho mkoa ambao jana
ulifanyika katika kata ya Mpera katika Manispaa ya Tabora.

Wanachama wanaowania kuteuliwa na chama hicho ni Profesa Hamba
Makambi, Raymond William Maganga, Said Mwakasekela, Furaha Kisanji na
Peter Stewart Mkufya huku dada Rehema Raphael akijitosa kuwania nafasi
ya kuteuliwa kupitia nafasi za viti maalumu wanawake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo watia nia hao
ambao wako kwenye ziara maalumu ya kutembelea wanachama wa chama hicho
katika kata zote za Manispaa hiyo walisema wananchi wanachohitaji sasa
ni mabadiliko chanya ya kiutendaji yatakayoleta tija ya maendeleo.

Walisema mkoa wa Tabora unazo rasilimali nyingi sana na fursa lukuki
ambazo kama zingeweza kutumiwa vizuri na viongozi walioko madarakani
maisha ya wananchi walio wengi yasingekuwa kama yalivyo sasa.

‘Umaskini tulio nao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na viongozi
tuliowaweka madarakani kwani wametumia muda wao mwingi kujilimbikizia
mali badala ya kutatua kero za wananchi, naomba mtuunge mkono ili
kumaliza ukilitimba huo wa viongozi wa chama tawala kwani hawana nia
ya dhati ya kuwaletea maendeleo’, walibainisha.

Mratibu wa Kanda wa chama hicho Christopher Nyamwanji alisema viongozi
wasiokuwa na dhamira ya kuwakomboa watanzania ndio wameifikisha Nchi
mahali ilipo sasa na hawana mbinu nyingine yoyote ya kubadilisha hali
ya maisha ya wananchi.

Alieleza kuwa pamoja na mkoa kuwa na misitu katika maeneo mengi tena
kwa asilimia kubwa cha kushangaza wanafunzi bado wanakaa chini kwa
baadhi ya shule jambo ambalo ni aibu kwa vile hawakustahili kukaa
chini kutokana na kuwepo misitu mingi.

“Wananchi wengi wamekata tamaa hawajui wafanye nini, wamekosa mtetezi
licha ya kuwa na fursa nyingi za maendeleo, kama CHADEMA tuna hasira
kubwa dhidi ya CCM na dhamira ya UKAWA ni kukiondoa madarakani ifikapo
Oktoba 25 mwaka huu,tunaomba mtuunge mkono,”alisema.

Alibainisha kwamba wamejipanaga vizuri na hawana mzaha katika suala
zima zla kuwatumikia wananachi kwa kuhakikisha rasilimali zilizopo
katika Mkoa huu zinatumika vizuri wa manufaa ya wananchi wote na Taifa
kwa ujumla.

Kada na Mhamasishaji Mkuu wa chama hicho mkoani hapa Elisha Daudi
alieleza wazi kuwa Watanzania wengi wanahangaika kwa kukosa mtetezi wa
kweli na jambo hilo limewakosesha fursa nyingi za kimaendeleo, hivyo
akawataka kuunga mkono jitihada za CHADEMA na UKAWA kwa kuchagua
viongozi wenye dhamira ya maendeleo.

Wagombea hao wa chama hicho watachujwa ifikapo tarehe 25 mwezi huu na
kubaki mmoja atakayepambanishwa na mmoja kutoka kila chama kinachounda
ukawa na kasha kupatikana mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya
ukawa Jimbo la Tabora Mjini.

No comments: