Pages

KAPIPI TV

Friday, July 24, 2015

"NITASHUGHULIKIA IPASAVYO KERO NA MATATIZO YA WANANCHI WA JIMBO LA TABORA MJINI"-BANDORA MIRAMBO

NA LUCAS RAPHAEL,TABORA

Kazi ya uwakilishi wa wananchi kwenye vyombo vya maamuzi sio kukaa ofisini na kutembelea  gari lenye  kiyoyozi bali ni kuyajua  matatizo na changamoto zinazowakabili na kisha kuzipatia ufumbuzi.


Imekuwa mazoea mara baada ya uchaguzi wabunge na madiwani wa vyama vyote kusahau  wajibu wao kwa wananchi jambo linalowafanya kuhaha unapokaribia wakati wa uchaguzi.



Hebu jaribu kukumbuka nyakati za mwisho wa Bunge hili lililopita la mwisho lililokuwa na bajeti,lilikuwa halina wawakilishi wa kutosha  kwa kuwa wengi wao walijaribu kujirudisha majimboni kwao ili kuanza kujenga upya  imani ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka minne na nusu.



Tabia ya kutowajali wananchi imegharimu kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo kuwa ndogo, Miradi kutokukamilika kwa wakati, Miradi kutekelezwa kwa viwango duni na matumizi mabaya ya fedha za umma na madaraka.



Mmoja kati ya vijana mahili anayeteka kuwani nafasi ya ubunge jimbo la Tabora mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi, Bandora Salum Mirambo (40) ambaye ni mkurungezi wa kampuni ya Salu Security Services Ltd ya Tabora imemkera sana hali hiyo na hata kufikia hatua ya kutoa kauli hiyo.



Anasema wabunge wengi kwa makusudi wamekuwa hawawatumikii wananchi waliowachagua ipasavyo jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya maeneo husika.



Anasema, “Mimi  nikipewa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo la Tabora mjini nitahakikisha navitumia vizuri vyombo vya maamuzi kwa maana ya baraza la madiwani na bunge la Jamhuri ya Muungano kutatua matatizo na kero mbalimbali  za wananchi.”



Anasema vyombo hivyo vya maamuzi vikitumiwa vizuri vinaweza kuleta matokeo chanya na kuharakisha maendeleo ya wananchi kwa kuwa ndipo maamuzi ya kibajeti ufanyika.



Anasema wabunge wengi wanaomaliza muda wao wameshindwa kuwatetea wananchi wao bungeni na wala hawakuonekana kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani na hivyo kushindwa kujua kinachoendelea kwenye ngazi ya halmashauri.





Anasema ubunge au udiwani unahitaji kiongozi ambaye ni mbunifu, mwenye maono na dira ya kuwavusha watu wake kutoka kwenye umasikini kwa kuzibadili changamoto kuwa fursa.





Bandora anasema suala hilo limekuwa gumu kwa wabunge wengi ambao wamekuwa wakisubiri fedha za kibajeti au za mfuko wa jimbo ambazo zinaukomo na hivyo kushindwa kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi.



Kazi ya uwakilishi inahitaji mtu mwenye upeo wa kupambanua na kuchambua mambo mbalimbali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi ngazi ya vikao vya kamati za maendeleo za mitaa, vijiji na kata.



Aidha anasema mtu huyo anapaswa kuutumia upeo wake kuchambua mambo kwenye vikao vya ushauri vya wilaya DCC na mkoa RCC ili kushawishi mwelekeo wa kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi wa jimbo lake.



Vikao hivyo muhimu vimekuwa vikipuuzwa na wabunge wengi na hata wanapohudhuria wamekuwa hawatoi mchango chanya au kutoongea kabisa.



Anabainisha kuwa kwa muda mrefu wabunge wengi wameshindwa kuonekana majimboni sio kwa sababu ya vikao vya bunge au vya kamati za kudumu za bunge bali wanaogopa kuombwa misaada na wapiga kura wao.



Jambo hili la kihekima linapaswa kutatuliwa na mbunge kwa kuwaonesha wapiga kura wake fursa zinazowazunguka ili waanzishe shughuli za uzalishaji mali badala ya kuwakimbia kwa hofu ya kuombwa.



Anasema, “Nikifanyikiwa kuwa mbunge nitasimamia upatikanaji wa mikopo ya fedha ,zana za kazi pamoja na maarifa ambayo yatawafanya wananchi kuziona fursa za uzalishaji mali na kuzitumia.”





Anasema kwa kuwashirikisha wananchi wa kada zote tutaimarisha shughuli za VICOBA uanzishwaji wa SACCOS zenye nguvu ambazo zitapambana na masharti ya dhamana yanayotolewa na taasisi za kifedha.



Bandora anasema jambo lingine atakalo lifanya ni kuibana halmashauri ya Manispaa ya Tabora kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana na wanawake.



Anasema endapo halmashauri hiyo ingekuwa ikitenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa mujibu wa sheria ingesaidia kubadili maisha ya wananchi wake kwa kiwango kikubwa.



Anabainisha jambo lingine atakalolipa kipaumbele ni uwazi katika kutekeleza majukumu yake ya kibunge kwa maana ya wapiga kura kujua utaratibu na ratiba ya mikutano ya kibunge, na vikao vya kamati za bunge ili kuondoa visingizio vya kutowajibika kwao.



Jambo lingine atafanya mikutano ya hadhara na wananchi na makundi mbalimbali ya kisekta ili kujua matatizo na changamoto zinazowakabili kabla ya kwenda bungeni tofauti na ilivyosasa ambapo mbunge anakwenda Bungeni kuwasilisha mambo anayoyawaza kutoka kichwani kwake.



Anasema wananchi wa Manispaa ya Tabora wamekabiliwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu ambayo imedhoofisha shughuli zao za uzalishaji mali na uwekezaji wa makazi na mambo mengine.



Anasema, “Jambo hili nitalisimamia kwa kuwakosoa na kuwakemea waziwazi watu wanaotumia madaraka yao ya utumishi wa umma au ya kisiasa kutengeneza migogoro ya ardhi kwa manufaa yao.”



Kwa kuwa njia nyingine bora ya kukabiliana na vitendo vya dhuluma kwenye ardhi ni kuwawezesha wananchi kuzijua sheria za ardhi za mwaka 1999 na sheria ya mipango miji ya mwaka 2007.



”nitahakikisha wakazi wa mji wa Tabora wanarasimisha shughuli zao pamoja na makazi kwa kupata hati zitakazowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.”



Anabainisha kuwa atahakikisha vyombo vya kisheria vinavyoshughulikia migogoro ya ardhi vinawezeshwa kwa kupatiwa wataalamu,vitendea kazi na kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na haki.



Anavitaja vyombo hivyo  kwa mujibu wa sheria kuwa ni mabaraza ya Ardhi ya kijiji, kata, mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya , mahakama kuu kitengo cha Ardhi na mahakama ya Rufaa.



Bandora anaweka wazi kuwa akiwa mbunge ataweka daraja la wazi kati yake na asasi za kiraia, makundi maalumu ya watu wenye ulemavu ambayo yamesahauliwa na wabunge na madiwani.



Aidha anaeleza kuwa ataimarisha misingi ya utawala bora kwa kujenga ofisi za wenyeviti wa mitaa kila kata kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.



 Anasema kwa kufanya hivyo kutapunguza malalamiko ya rushwa na kwamba atawawezesha kupata posho na vitendea kazi kila mwezi.



Anasema atasimamia kikamilifu sekta za maji, elimu na afya ambazo zinagusa na kuchochea ustawi wa sekta nyingine.

Bandora anasema atahakikisha zahanati zinakuwa na watumishi wa afya, dawa, vifaa tiba ili kupunguza msongamano kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete.


Aidha atahakikisha mpango wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Tabora unaanza mara moja kwa fedha kutengwa na pia kutafuta misaada kwa wadau wa sekta ya afya.


Mkakati huo anasema ni wa makusudi utasaidia kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na akinamama wajawazito.


Atahimiza uimarishwaji wa mpango wa damu salama ambao umepuuzwa na wabunge na madiwani wengi huku wahitaji wakubwa ni watoto na akinamama wajawazito.



Bandora anasema kama wanawake ni jeshi kubwa linalotumika kwenye uchaguzi kwanini limekuwa likisahaulika mara baada ya uchaguzi kwa kuruhusu vifo vyao wakiwa wajawazito?.



Anasema atasimamia mipango ya uboreshaji wa huduma ya maji kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira TUWASA pamoja na kuhimiza serikali kulipa madeni ya taasisi zake ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni moja.

Atahimiza pia utekelezaji wa mradi wa maji ya ziwa Victoria kutokea kijiji cha Solwa Shinyanga kupitia Nzega kuja Tabora na wilaya nyingine za mkoa wa Tabora.


Aidha kwenye elimu atahakikisha hakuna mtoto anayekaa chini katika shule za msingi za manispaa ya Tabora ambako kuna miti ya mbao na mbao za kutosha.



Akizungumzia michezo anasema kwamba atashirikiana na vyama vyote vya michezo kuinua michezo kuanzia ngazi za mitaa, vijiji na kata tofauti na ilivyosasa nguvu  zisizo na utaratibu zimewekwa kwenye soka la wanaume pekee.



Anasema ameamua kufanya hivyo ili kurudisha hadhi ya michezo ya mkoa wa Tabora iliyokuwepo miaka ya nyuma.



“Kukosekana kwa mikakati madhubuti katika michezo kumefanya vipaji vingi vya vijana wa Tabora  kupotea  jambo ambalo limesababisha kupoteza ajira kupitia michezo.”anasema Bandora.



Anasisitiza kukitumikia Chama Cha Mapinduzi na kukifanya kuwakomboa wananchi na wanachama wake kwa kuwaletea maendeleo halisi.

No comments: