Pages

KAPIPI TV

Friday, July 10, 2015

NHIF YAKABIDHI MSAADA WA MASHUKA 200 KWA HOSPITALI YA MKOA MJINI SINGIDA

DSC00136
Meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Agnes Chaki (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Singida, Alli Amanzi msaada wa mashuka 200 kwa ajili ya hospital ya mkoa mjini hapa.(Picha na Nathaniel Limu).
DSC00132
Mkuu wa wilaya ya Singida,Alli Amanzi (kulia) akibadilishana mawazo na Meneja Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoa wa Singida, Agnes Chaki (katikati) muda mfupi kabla Meneja NHIF hajakabidhi mashuka 200 kwa hospitali ya mkoa mjini hapa.Kushoto ni Afisa uthibiti ubora wa huduma NHIF mkoani hapa, Dk.Edwin Mwangajilo.
Na Nathaniel Limu, Singida
HOSPTALI ya mkoa wa Singida iliyopo mjini hapa,inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mashuka kitendo kinachochangia wagonjwa kutumia mashuka yao binafsi wakati wote wanapokuwa wamelazwa hospitalini hapo.
Hayo yamesemwa na Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Henry Mgetta, wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa mashuka 200 yaliyotolewa msaada kwa hospitali ya mkoa na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) mkoani Singida.
Alisema hospitali hiyo yenye vitanda 300 vya kulaza wagonjwa,inakabiliwa na uhaba wa mashuka 2,400 na magodoro 230.
“Hali ni mbaya mno,shuka 100 tulizonazo,ni chakavu na kwa ujumla nazo hazifai kwa matumizi ya binadamu.Wagonjwa wanaolazwa inawalazimu kutumia shuka zao binafsi jambo ambalo halikubaliki”,alisema Dk.Mgetta.
Alisema mbali na uhaba wa shuka na magodoro,hosptali hiyopia ina uhaba wa vitanda na hasa kwenye wodi ya wazazi, kitendo kinachochangia wajawazito wanne watumie kitanda kimoja.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali,waangalie uwezekano wa kuisaidia kwa hali na mali hospitali yetu hii na vituo mbalimbali,ili viweze kutoa huduma bora inayokidhi mahitaji ya wananchi”’alisema Dk.Mgetta.
Kwa upande wake Meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Agnes Chaki,alisema kuwa wametoa msaada huo wa mashuka hayo baada ya kuombwa na serikali ya wilaya ya Singida.
Alisema majukumu ya NHIF,ni pamoja na kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya zinajitosheleza kwa kuwa na mahitaji yote muhimu kwa kutoa misaada na vile vile mikopo ya kununulia dawa,vifaa tiba na uboreshaji wa majengo.
“Nina imani kituo cho chote cha afya,zahanati na hospitali,kinapokuwa na vitanda,mashuka na mambo mengine muhimu kwa wagonjwa wanaolazwa,kitendo hicho kitakuwa kinawajengea mazingira mazuri ya kuendelea na matibabu bila usumbufu wo wote”,alifafanua meneja huyo.
Chaki alisema NHIF itaendelea kutoa misaada mbalimbali kadri uwezo utakavyoruhusu kwa lengo la kusaidiana na serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za afya.

No comments: