Pages

KAPIPI TV

Monday, February 9, 2015

WAMASAI WATAKA UWEKEZAJI KUSITISHWA NGORONGORO

DSC_0200Kiongozi wa mila tarafa ya Ngorongoro, Augustino Pakai Olonyokei akizungumza na Meneja uendeshaji wa mtandao wa habari wa modewjiblog, Zainul Mzige aliyefika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia miradi mbalimbali inayoendeshwa kusaidia jamii ya wafugaji wa kimasai hivi karibuni.

Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
KIONGOZI wa mila tarafa ya Ngorongoro Augustino Pakai Olonyokei ameitaka serikali kusimamisha uwekezaji katika Mamlaka ya Ngorongoro ili kupunguza shinikizo la raslimali katika eneo hilo.

Alisema kuendelea kuwekeza katika mahoteli,makambi ya watalii, miundombinu katika hali ilivyo sasa ni kuzidisha migogoro iliyopo kati ya wakazi wa eneo hilo na mamlaka ambayo tayari ipo.

Olonyokei alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ambaye alifika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia miradi mbalimbali inayoendeshwa kusaidia jamii ya wafugaji wa kimasai.

Alisema hali ya sasa ni ngumu na inayosikitisha hasa kutokana na sheria iliyoanzisha mamlaka ya Ngorongoro kuwanyang’anya umiliki wa eneo ambalo wao wamelilinda miaka yote ndiyo maana wanyama wanapatikana na utalii unakuwepo.

Aidha alisema mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya mazingira yao kuwa magumu , wanakuwa na njaa huku wakiwa wamekatazwa kulima hata eneo dogo.

“Tuna changamoto nyingi…hatuna ajira, ushiriki wetu katika bodi ni mdogo na baraza la wafugaji linapewa hela kidogo katika mazingira ya kuwa na miradi mingi,” alisema Olonyokei.

Alisema Baraza hilo kupewa sh bilioni moja tu haitoshi wakati utalii ukiingiza mabilioni ya fedha.

Pamoja na kuelezea changamoto hizo na kuitaka serikali kuzuia kuongezeka kwa shughuli zaidi katika eneo hilo, aliwataka watanzania kujua mazingira ya jamii ya wafugaji na adha wanazokutana nazo.

Hata hivyo Mhifadhi wa mamlaka ya Ngorongoro Dk. Freddy Manongi amesema kwamba pamoja na malalamiko hayo, mamlaka hiyo iliyoanzishwa mwaka 1959 kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii, utalii na kuhifadhi mazingira mwaka jana pekee ilitumia sh bilioni 60.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza jamii na utalii.

Alisema msaada mkubwa wanaoufanya ni katika sekta ya elimu ambapo imejenga shule 21 na kila mwanafunzi anayekwenda sekondari kutoka katika eneo hilo hupatiwa udhamini wa masomo.

Aidha alisema kutokana na wananchi kuzuiwa kulima, huwapatia mahindi kwa ajili ya chakula na ingawa kunatakiwa kuangaliwa namna bora zaidi endelevu ya wananchi kupata chakula lakini kwa sasa hilo ndilo wanalofanya.
DSC_0041
Mhifadhi wa mamlaka ya Ngorongoro, Dk. Freddy Manongi katika mahojiano maalum na Meneja uendeshaji wa mtandao wa habari wa modewjiblog. Zainul Mzige (hayupo pichani).

“Mahindi ya bure yanapokosekana anagalau yawepo ya kununua kwa bei ya chini, na tunauza kwa shilingi 5000 kwa debe” alisema.

Dk. Manongi alisema pia kwamba fedha nyingine zinatumika katika sekta ya afya na pia kuboresha hali ya mifugo kwa kuwezesha uharamishaji mifugo na kujenga majosho.

Alisema ongezeko kubwa la watu katika eneo ambalo haliongezeki ni dhahiri linaleta migongano lakini mamlaka hiyo inafanya shughuli zake kwa kushirikiana na Baraza la wafugaji ili kupunguza migongano.

Wakati mamlaka inaanzishwa 1959 eneo hilo lilikuwa na wakazi 8,000 baada ya wengine 4000 kuhamishiwa hapo kutoka Serengeti. Kwa sasa eneo hilo lina watu takaribani 90,000 katika eneo lilelile la kilomita za mraba 8,262.

Alisema baraza hupewa sh bilioni 2 kwa mwaka wakati shughuli nyingine za maendeleo zinazofanywa na Mamlaka hugharimu sh bilioni 11.

Kuhusu changamoto za elimu amesema kwa mwaka jana hali haikuwa njema kwa ufaulu lakini sasa wametafuta sababu na kuanza kuhakikisha kwamba walimu wanapewa motisha na pia wanafunzi wanapata mlo wa mchana ili kuwafanya wasitoroke.

Kuhusu suala la ajira Dk. Manongi amesema ni tatizo la tafsiri tu lakini kila nafasi zinazpopatikana hujitahidi kuajiri watu kutoka katika eneo hilo.

Alisema kuna mambo mengi yanayofanywa kuimarisha eneo hilo kuendeleza jamii na kuendeleza hifadhi ili kuwezesha utalii ambao ndio unatoa fedha kwa ajili ya mambo yote.

No comments: