Mbunge wa Jimbo la Urambo Magharibi wilayani Kaliua Profesa Juma Athumani Kapuya akifurahia na wana CCM katika kilele cha sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa CCM. |
Na Allan Ntana, Kaliua
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kutoogopa
matusi na kashfa zinazotolewa kwenye majukwa ya kisiasa na viongozi wa vyama
vya upinzani kwa kuwa matusi hayo ni kichocheo cha kuifagilia CCM na hamasa ya
kuongeza jitihada zaidi za kuwatumikia wananchi.
Hayo yalibainishwa juzi na Mbunge wa jimbo la Urambo
Magharibi ambayo ni wilaya mpya ya Kaliua mkoani Tabora Profesa Juma Athumani
Kapuya katika kilele cha sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika
katika kata ya Usinge na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Kapuya aliwataka wana CCM na viongozi wote wa chama
hicho kutoogopa misukosuko ya aina yoyote ile na maneno ya kashfa na matusi
yanayosemwa majukwani dhidi yao na wapinzani kwani wanawafagilia tu na
kuwajenga zaidi kisiasa ili waendelee kuwatumika wananchi kwa ari mpya, kasi
mpya na nguvu mpya.
Alisema CCM iliyoasisiwa na Baba wa taifa hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imejijengea misingi mizuri ya kuwatumikia
wananchi wake ndio maana imekuwa na mikakati mingi ya kuhakikisha huduma za
kijamii zinaboreshwa sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya maadui wa
maendeleo ikiwemo ujinga, maradhi na umaskini vita aliyoanza Baba wa Taifa
akawaachia waiendeleze.
‘Ndugu zangu CCM imefanya kazi kubwa sana ya
kuwaletea maendeleo wananchi, msishabikie tu maneno ya hao ndugu zetu
wasiopenda amani na wasioitakia mema nchi yetu angalieni shule za msingi na
sekondari zilivyoongezeka, angalieni wingi wa vyuo vikuu, zahanati, vituo vya
afya, barabara za lami na kasi kubwa ya kusambaza umeme hadi vijijini
inayoendelea sasa’, alisema.
Alieleza kuwa CCM na serikali yake hawapaswi kuanza
kulumbana na hao wapinzani wala kuwaona kwamba hawafai kwani hao ni wenzetu
tulikuwa nao na tukiendelea kuwaletea maendeleo watarudi tu sie hatuna ugomvi
nao, chama chetu kinaamini kuwa binadamu wote ni sawa, tutajenga barabara,
shule, vituo vya afya, zahanati na vyuo vikuu, kwa ajili ya Watanzania wote na
wao wakiwemo.
Aidha alieleza kuwa kitendo cha serikali ya CCM
kuendelea kukaa madarakani kwa mda mrefu tofauti na vyama vingine vya ukombozi
Barani Afrika kinatokana na misingi mizuri na mshikamano uliopo baina ya
viongozi na wanachama wake, jambo ambalo ni tofauti kwa vyama vilivyo vingi
ikiwemo hivi vilivyoko hapa nchini.
Akizungumzia hali ya kisiasa ndani ya wilaya hiyo
Profesa Kapuya alisema wananchi wengi bado wanaipenda CCM kwani ushindi wa viti
44 kati ya 71 waliopata wagombea wa CCM ambao ni sawa na asilimia 78 dhidi ya
viti 27 sawa na asilimia 23 walivyopata wapinzani ni ishara tosha ya
kukubalika.
Aidha alisema chama chake kuendelea kukubalika
wilayani humo ni kwa sababu kina dira ya maendeleo na mshikamano mzuri wa
wanachama na viongozi na ni mkombozi wa kweli kwa wananchi wa wilaya hiyo
kinachotakiwa ni kushikamana vizuri na wananchi ili wazidi kuwaunga mkono.
Akitoa maoni yake juu ya suala la wizi wa pesa za escrow,
Profesa aliwataka viongozi wa serikali na mashirika kuacha tamaa ya mali na
utajiri wa haraka haraka kwani itawamaliza kisiasa au kuharibu mtiririko mzima
wa maisha yao ikiwemo kufilisiwa.
Aidha alisema vitendo vya wizi wa mali ya umma na
ufisadi vinavyofanywa na viongozi wa serikali vinachochewa na tamaa ya mali na
utajiri na kwa kiasi kikubwa vina changiwa na kuporomoka kwa maadili ya
viongozi sambamba na matumizi mabaya ya teknolojia ambapo alishauri kuwepo na
udhibiti wa teknolojia inayotumika katika mitandao ya kifedha.
Na kwa biashara haramu ya madawa ya kulevya inayofanywa
na wananchi wa rika tofauti wakiwemo viongozi wakubwa alisema kuwa inachangiwa
na malezi mabaya ya wazazi na kuporomoka kwa maadili ya viongozi.
Ili kukomesha tabia za wizi wa mali ya umma kwa
viongozi wa serikali Profesa Kapuya alishauri Chama Cha Mapinduzi ambacho
ndicho kimeshika dola kusimamia ipasavyo suala la uadilifu kwa watendaji wake sambamba
na kuwachukuliwa hatua kali wale wote wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Akizungumzia katiba inayopendekezwa Profesa Kapuya aliitaka jamii kuiunga mkono kwa
sababu imeelezea mambo yote ya msingi yanayogusa na kutetea maslahi ya makundi
yote ya kijamii na imezingatia hali ya kila Mtanzania huku akiwataka wote
wanaoshawishi wananchi waikatae kuacha tabia hiyo kwani haina maslahi kwa
taifa.
No comments:
Post a Comment