Wafanyakazi wa Shirika la Posta, wanafunzi wa shule ya sekondari Chabutwa na uongozi wa shule wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu. (Picha na Allan Ntana) |
Na Allan Ntana, Sikonge
WAKATI halmashauri zote hapa nchini zikiwa katika pilika pilika za kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la ujenzi wa vyumba 3 vya maabara kwa kila shule ya sekondari, Shirika la Posta Tawi la Tabora limetoa msaada wa mabati na simenti kwa shule ya sekondari Chabutwa iliyoko wilayani Sikonge mkoani Tabora ili kuharakisha utekelezaji zoezi hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa serikali ya kijiji na uongozi wa shule hiyo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu, Meneja wa Shirika hilo mkoani Tabora Aggrey Mhecha alisema wameguswa kutoa msaada huo katika shule ya Chabutwa ili kuunga mkono jitihada za
serikali na wananchi katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati.
Vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo ili kumalizia ujenzi wa vyumba 3 vya maabarani katika shule hiyo ni mabati 5 yenye thamani ya sh 75,000/-, mifuko 5 ya saruji (simenti) yenye thamani y ash 95,000/- na fedha taslimu kiasi cha sh 136,200/- zilizochangwa papo hapo kwa hamasa ya Meneja msaidizi wa shirika hilo Bi. Mwatum Tambwe.
Meneja Mhecha alisema halmashauri nyingi bado zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha katika harakati za kukamilisha majengo yote 3 ya maabara ndio maana Mkuu wa wilaya ameendelea kuhamasisha wadau mbalimbali, taasisi, mashirika ya umma, makampuni binafsi na wananchi kwa ujumla kuchangia zoezi hilo kwa faida ya watoto wetu.
‘ Tumeguswa sana na jitihada zinazofanywa na wananchi wa kijiji hiki, uongozi wa kijiji, uongozi wa shule na mkuu wa wilaya, tumekuja kutoa mchango wetu japo kidogo, ili mweze kukamilisha zoezi hili muhimu katika nchi yetu, na hii ni kwa kutambua umuhimu wenu katika huduma zinazotolewa na Shirika la Posta’, alieleza.
Mhecha alibainisha kuwa shirika hilo limeendelea kuboresha huduma zake kwa kiwango kikubwa ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na sanduku la barua, kuhamasisha wananchi kutumia mtandao makini wa mawasiliano ya komputa wa Postal Global NetSmart unaotolewa la shirika hilo sambamba na kuhamasisha ushiriki wa wanafunzi wa sekondari na msingi katika shindano la uandishi wa barua kwa mwaka huu.
Afisa Masoko wa Shirika hilo wilayani Sikonge Peter Mbadagu alisema msaada waliotoa kwa shule hiyo ni chachu kubwa ya kujenga mahusiano mazuri na wateja wilayani humo na kuhamasisha utumiaji wa huduma mbalimbali zitolewazo na shirika hilo.
Aidha alibainisha mikakati ya shirika hilo katika wilaya hiyo kuwa ni pamoja kutembelea wateja na kuhamasisha huduma mbalimbali zitolewazo na posta, kukumbusha huduma ya utumiaji mtandao kwa wanafunzi wa sekondari wanaojiandikisha kufanya mitihani na wale waliomaliza kidato
4 kuchukua vyeti vyao katika ofisi za shirika hilo.
No comments:
Post a Comment