CHAMA cha wafanyakazi wa asasi za fedha,viwanda,Benki,Uzalishaji wa nishati,Biashara na Kilimo FIBUCA tawi la Tabora kimelalamikia hatua za vitisho wanavyopatiwa wanachama wa chama hicho tawi la kampuni ya tumbaku ya ATTT kutoka kwa mwajiri wao na kusababisha baadhi ya wanachama kutaka kujitoa kwa kuhofia kupoteza ajira zao.
Akisoma taarifa fupi mbele ya kaimu mkuu wa mkoa wa Tabora Suleiman Kumchaya wakati wa semina ya viongozi wa tawi la chama hicho katika kampuni ya ATTT,Katibu wa FIBUCA mkoani hapa Ramadhani Wakulichombe alisema moja kati ya changamoto kubwa inayowakabili ni pamoja na vitisho dhidi ya wanachama na viongozi wa tawi hilo.
Wakulichombe amebainisha kuwa licha ya FIBUCA kuendelea kujitangaza sehemu mbalimbali za waajiri na kufanikiwa kuingiza wanachama wengi ikiwemo wafanyakazi wa kampuni ya Association of Tanzania Tobacco Traders ATTT,lakini jambo la kushangaza ni kuona uongozi wa kampuni ya ATTT ikihoji kwanini wafanyakazi hao wamejiunga na chama hicho jambo ambalo limekuwa likiwatishia na hata kufikia hatua ya kuanza kujitoa wakihofia kupoteza ajira.
Alisema hatua ya kampuni ya uongozi wa kampuni ya ATTT kutishia wanachama ni kinyume na sheria ya ajira na mahusiano kazini sehemu ndogo 'd' inayozungumzia uhuru wa kujumuika(Employees right to freedom of association)kifungu namba tisa(9) kwamba kila mwajiriwa anayo haki na kujiunga na chama cha wafanyakazi anachokiona kinamfaa.
Hata hivyo Katibu huyo wa FIBUCA ameiomba Serikali ya mkoa wa Tabora kuingilia kati na kulifanyia kazi suala hilo ambalo linawafanya wafanyakazi au wanachama wa chama hicho tawi la ATTT kutokuwa na uhuru wa kisheria katika maeneo yao ya kazi.
Akifungua semina hiyo kaimu mkuu wa mkoa wa Tabora Suleiman Kumchaya aliwataka vingozi wa FIBUCA kusimama imara wakati wanapotetea haki za wanachama wao pasipo kuvunja sheria.
Kumchaya alisema vitisho imekuwa ni jambo ambalo linalotumiwa sana na baadhi ya waajiri ikiwa ni moja ya hatua ya kuwanyonya wafanyakazi mahala pa kazi ili wao waweze kunufaika zaidi.
Aidha katika hatua nyingine baadhi ya wafanyakazi wa ATTT ambao hawakutaka kutaja majina yao wameeleza kuwa mwajiri wao amekuwa akilazimisha wafanyakazi wake wajiunge na chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo TPAWU ambacho wamedai kuwa kimekuwa kikilinda zaidi maslahi ya mwajiri kuliko mfanyakazi.
Walisema TPAWU ni chama ambacho kilikuwepo tangu awali kabla ya FIBUCA na hivyo wamedai kuwa kimeshindwa kutetea maslahi ya wafanyakazi ndio maana wakaamua kujiunga na FIBUCA ambacho mwajiri hakubaliani nacho na ndio sababu ya kuwepo kwa vitisho kwakuwa chama hicho kimekuwa kikiweka wazi na kutoa elimu ya haki za wafanyakazi na namna ya kuzidai.
Chama cha wafanyakazi FIBUCA ni chama huru kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini namba sita(6)ya mwaka 2004 na kupata usajiri wa kudumu mnamo tarehe 24 Julai 2009 kwa kupewa cheti namba 24 ambapo kilianzishwa na wafanyakazi wapatao 20 kutoka Benki ya NMB,NBC,NSSF na DAWASCO.
No comments:
Post a Comment