Pages

KAPIPI TV

Friday, December 12, 2014

UZAZI WA MPANGO WAPUNGUZA UTOAJI MIMBA HOLELA

Na Magreth Magosso,Kigoma.

WANAWAKE waishio Mkoa  wa Kigoma wameshauri watumie njia za kisasa (Uzazi wa Mpango) ili kupunguza wimbi la utoaji mimba usio salama pamoja na ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi.

Hayo yalibainika Kigoma Ujiji  katika warsha ya  siku moja kwa wandishi wa habari wa hapo ukilenga kuwaongezea   uelewa  mpana  namna  ya kuandika kwa umahiri habari za afya ya uzazi wa mpango ili walengwa wachukue hatua za kutumia njia salama ya uzazi wa mpango(nyota ya kijani)itakayochangia kuimarisha afya na kumudu  huhudumia familia walizonazo.

Akifafanua hilo Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la (UNFPA) Mehjabeen Alarakha pia Family Planning Programmer Analyst alisema  9% ya wanawake wanatoa mimba kwa njia isiyo salama kwa nia ya kuepuka majukumu ambayo hawakutarajia kwa muda huo.

Aliongeza kwa kusema kuwa,changamoto hiyo itatoweka ikiwa watathubutu kutumia njia za salama za uzazi wa mpango kama Kitanzi,lupu,vidonge vya majira,sindano , kipandikizi na kufunga kizazi ambapo mwanamke akianza kutumia anaweza kupata maudhi madogomadogo ama asikutane nayo .

Kwa upande wa  Program Manager Advocacy James Mlali alisema kwa mikoa ya Kigoma na tabora ina 30% ya watoto kubeba mimba ambapo kitakwimu inaonyesha ndio mikoa yenye idadi kubwa ya watoto kuzaa watoto wakati mkakati wa taifa  unahitaji kufikia  mwaka 2015  kuwe na 60%  ya wanawake watumie njia za kisasa.

Athari kubwa kwa watoto kubeba mimba kabla ya wakati ni vifo wakati wa kujifungua kutokana na viungo vya uzazi bado havijakomaa kushika mimba,kupoteza ndoto za maisha yake ya kesho kutokana na kuanza majukumu ya ulezi kabla ya wakati ,kuwa tegemezi katika familia hatimaye huishi katika mazingira magumu ya umaskini.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Fadhili Kibaya alisema  wandishi wa habari wanajukumu kubwa la kuelimisha umma  madhara ya mimba za utotoni,ambapo serikali inashindwa kutoa huduma kwa haki na usawa kwa wananchi kutokana na ongezeko la watu kuwa kubwa kuliko rasilimali husika.

Mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Ramadhan Maneno alisema watoto wa kike waache tamaa na wasitumie kigezo cha umaskini kujiingiza kwenye mapenzi kabla ya umri ambapo inachangia serikali ishindwe kuboresha huduma  ya  afya  na elimu kwa umma na kushauri wazazi  wasikwepe jukumu la kulea watoto kimaadili.

Aidha  inaelezwa kuwa,ifikapo 2035  taifa litakuwa na idadi ya watu wapatao milioni 100 endapo wanawake watashindwa kutumia njia za kisasa ambazo ni chachu kwa maendeleo ya taifa lolote duniani.

No comments: