Pages

KAPIPI TV

Friday, November 28, 2014

WATOTO WENYE MAZINGIRA MAGUMU WAPATIWA VYANDARUA ...KIGOMA

Na Magreth Magosso,Kigoma

WAKAZI wa Mkoa wa Kigoma, wametakiwa waache tabia ya kutumia chandarua katika matumizi ya kuvua samaki na kuzungushia uzio wa bustani za mboga ,badala yake watumie  kutega  katika kitanda  kwa nia ya kuwakinga watoto na  mbu aina ya anofelesi anayeambukiza ugonjwa wa Malaria.

Mbali na hilo, watoto 3,000 waishio katika mazingira magumu wamepatiwa msaada wa vyandarua 6,000 vyenye viatilifu vya dawa maalum ya kuua mbu jike aitwae anofelesi  ambao hutafuna chembechembe nyekundu za damu hatimaye hupelekea homa kali na kuishiwa damu mwilini,  ambapo wahanga wakubwa ni watoto na wanawake wajawazito.

Hayo yalisemwa na mtaalamu wa afya kutoka  asasi isiyokuwa ya kiserikali (Compassion InternationalTanzania)  Elias Mwinuka katika tukio la siku ya malaria iliyoazimishwa mkoani humo  ikilenga kutoa msaada wa  vyandarua kwa lengo la kuwakomboa watoto husika katika janga la maradhi,umaskini na ujinga.

Alisema lengo la asasi ni kuwalea watoto walio katika mazingira magumu bila kujali itikadi za kidini wala dhehebu kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiakili, kiroho na elimu ya awali hadi chuo kikuu na kuwasihi wananchi wazingatie matumizi bora ya vyanandarua hivyo ambapo kila mtoto alipatiwa vyandarua viwili.

Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa  wachungaji wa madhehebu husika (Clasta ya kigoma) Wilson Gwimo alifafanua kuwa, asasi hiyo ya kimataifa ya Compassion inafadhili  mungano wa madhehebu 15 ya dini ya kikristo nchini hapa ikilenga kulea watoto wenye maisha duni na wenye mazingira hatarishi .

Kwa upande wa mgeni rasmi pia Mkuu wa mkoa Lt.mstaafu Issa Machibya alisema walezi wakumbuke wajibu wa kuwapa malezi mema watoto ni pamoja na kuimarisha afya zao, ambapo kigoma inaongoza  matumizi mabaya ya chandarua ambapo wengi  hutumia kwenye uvuvi na uzio wa bustani.

Naye Mganga Mkuu wa kigoma Leonard Subi alisema kigoma ina 26% ya wakazi wake kuugua ugonjwa wa malaria,nakuipongeza asasi hiyo kwa jitihada za makusudi za kuokoa watoto waishio katika mazingira magumu na kuwasihi walezi waboreshe lishe za walengwa.

Baadhi ya watoto waliopokea vyandarua hivyo Rahman Hamis na Jefrina Emanuel kwa nyakati tofauti walisema,watatumia vyema vyandarua hivyo,ili kujikinga na mbu aenezae ugonjwa hatari wa malaria na kusihi watu binafsi na asasi zingine zisaidie watoto waishio katika mazingira magumu.

No comments: