Na Anna Nkinda – Beijing, China
Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan ameahidi kutoa vifaa vya
shule vikiwemo vya maabara pamoja na vitabu kwa ajili ya shule ya
Sekondari ya WAMA-Nakayama ili wanafunzi hao waweze kusoma vizuri
masomo ya sayansi.
Mama Liyuan aliitoa ahadi hiyo jana wakati akiongea na mke wa
Rais Mama Salma Kikwete katika ukumbi maarufu wa watu (Great hall of
the People) uliopo mjini Beijing.
“Nina mapenzi na Taasisi ya
WAMA, nakupongeza kwa kazi unayoifanya ukiwa Mke wa Rais ya kuwainua
wanawake kiuchumi na kuwasaidia watoto wa kike ambao ni yatima na
wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao nao wanapata elimu sawa na
watoto wengine”.
Najua kitaaluma wewe ni mwalimu
na unapenda shule mwaka huu nitakuunga mkono zaidi katika masuala ya
shule, hii itawasaidia wanafunzi kusoma vizuri. Pia nitakuwa na
ushirikiano endelevu na Taasisi ya WAMA”, alisema Mama Liyuan.
Kwa upande wake Mama Kikwete
alishukuru kwa msaada huo na kusema kila kwenye maendeleo changamoto
hazikosekani alizitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambazo
ni upungufu wa maabara, kutokuwepo kwa wataalamu wa maabara na walimu
wa masomo ya sayansi wa kutosha.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema katika
upande wa elimu Serikali kwa kushirikiana na wananchi wamejitahidi
kujenga shule nyingi za Sekondari lakini bado kuna upungufu wa walimu
wa masomo ya sayansi , kutokuwa na maabara za kutosha, kutokuwa na
vifaa vya maabara na upungufu wa wataalamu wa maabara .
“Ninaomba kuwe na ubadilishanaji
wa ujuzi wa kazi (Exchange Program) kwa walimu wetu wa nchi hizi mbili
hii itawasaidia kupata utaalamu zaidi katika fani zao na kutoa mfano wa
wataalamu wa maabara ambao wakija nchini watasaidia kwa kiasi kikubwa
kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa njia ya vitendo”, alisema
Mama Kikwete.
Shule hiyo ambayo inamilikiwa na
Taasisi ya WAMA wanafunzi wake ni watoto wa kike ambao ni yatima na
wanaotoka katika mazingira hatarishi kutoka mikoa yote ya Tanzania
Bara na Visiwani iko kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani
Pwani.
Hii ni mara ya pili kwa Mama
Liyuan kuiunga mkono Taasisi ya WAMA ambapo mwaka 2013 alipotembelea
nchini alitoa Yuan milioni moja sawasawa na shilingi milioni 250 za
kitanzania na mabegi ya shule 100 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya
Sekondari ya WAMA-Nakayama na vyerehani 20 kwa ajili ya Umoja wa Vikundi
vya WAMA (UVIMA).
Mama Kikwete ameambatana na mumewe Rais Prof. Jakaya Mrisho Kikwete nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku sita.
No comments:
Post a Comment