Na Mwandishi wetu, Tabora
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Jakaya
Mrisho Kikwete ameahidi kuchangia kiasi cha sh milioni 10 na trekta moja kwa
Kituo chaVijana cha Pathfinder Green City kilichoko wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Aliitoa ahadi hiyo alipotembelea kituo hicho chenye
vijana wapatao 100 ambao wanajifundishwa utaalamu wa aina mbalimbali ikiwemo
ufundi, ujenzi, ufyatuaji matofali ya kisasa (aina ya interlock), kilimo,
ufugaji nyuki, ufugaji wa kuku na ng’ombe na ujasiriamali.
Rais alionyeshwa dhahiri kufurahishwa na shughuli za
uzalishaji mali zinazofanywa na vijana hao sambamba na kujishughulisha na kilimo
cha mazao mbalimbali kama vile tumbaku, mahindi, mpunga na mbogamboga ambapo
tayari wameshaanza kujipatia kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mauzo ya mazao
hayo.
‘Kazi niliyokuta kwenye kijiji cha mfano pale
Sikonge imenifurahisha sana, wanafanya mambo makubwa, wanalima tumbaku,
mahindi, wanafuga nyuki, kuku, ng’ombe, wanashona viatu, nguo, wanafyatua
tofali na kujenga nyumba za kisasa wao wenyewe, hawa vijana ni mfano wa kuigwa,
wanastahili pongezi’, alisema.
Nimeahidi kuwasaidia shilingi milioni 10 na trekta
ili wafanye kilimo kilicho bora zaidi kitakachowafanikisha kiuchumi wao
wenyewe, familia zao, jamii inayowazunguka, wananchi wa wilaya ya Sikonge, mkoa
mzima wa Tabora na taifa kwa ujumla, aliongeza.
JK alibainisha kuwa vijana walioko katika kituo
hicho kilichoko katikati ya vijiji vya Lufwisi na Tumbili wilayani humo
watakuwa mfano wa kuigwa na waalimu wazuri kwa wenzao na jamii nzima kwani
mafunzo wanayopata yanawapa ujuzi mkubwa sana katika kilimo na fani nyinginezo.
Aidha JK alipongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya
hiyo chini ya Mkuu wa wilaya Hanifa Selengu na Mkurugenzi Mtendaji Shadrack
Mhagama na serikali ya mkoa huo kwa kufanikisha uanzishwaji kituo hicho cha
mfano katika mkoa huo huku akiwataka waendelee kukisimamia vizuri zaidi.
Aidha akiwa katika ziara hiyo aliziagiza halmashauri
zote hapa nchini kujiwekea utaratibu wa kutoa taarifa za maendeleo mara kwa
mara angalau kila baada ya miezi nne ili kubaini mafanikio yako wapi na
changamoto ni zipi ili waweze kuweka utaratibu wa namna ya kukabiliana nazo,
kwa kuanzia aliwataka kutoa taarifa za maendeleo mwezi desemba na nyingine baada
ya miezi 4.
No comments:
Post a Comment