Mkurugenzi
wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke
(katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukuaji wa Pato la
Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam. Wengine ni Bw. Oswald
Ruboha (kulia) Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara
ya Kilimo na Dkt. Stephen Kirama (kushoto), Mhadhiri wa Uchumi, Chuo
Kikuu cha Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Sekta ya Kilimo,Uvuvi, Viwanda ,
Nishati na Madini zimeelezwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu
zinazoongoza zaidi katika kuchangia kukua kwa pato la Taifa hadi
asilimia 7.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji nchini na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kutumia kanuni za kimataifa
kukokotoa pato la Taifa zinaonyesha kuwa sekta hizo zimetoa mchango
mkubwa wa kukua kwa pato la Taifa kwa asilimia 7.4 kuanzia mwezi
Januari hadi Machi, 2014 ikilinganishwa na asilimia 7.1 za mwaka 2013.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke akizungumzia ukuaji wa
Pato la Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam amesema kuwa Pato
la Taifa katika robo ya mwaka 2014 kuanzia Januari hadi Machi limekua
kwa asilimia 7.4 kutokana na kukua kwa sekta za Kilimo, Uvuvi, Viwanda,
Ujenzi, Umeme na utoaji wa huduma.
Amesema sekta zilizofanya vizuri
katika ukuaji huo ni pamoja na sekta ya uchimbaji wa Madini, mawe na
kokoto ambayo imekua kwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 1.7 za
mwaka uliopita kutokana na kukua kwa masoko ya uuzaji ya nje ya nchi.
Ameongeza kuwa sekta uzalishaji
wa bidhaa za viwandani imekua kwa asilimia 8.5 kutoka 8.3 huku shughuli
za utoaji wa huduma na uchumi zikiwemo za ukarabati wa magari, pikipiki
na vifaa vingine vya majumbani zikikua kwa asilimia 8.0 kwa robo ya
mwaka 2014.
Bw. Oyuke ameeleza kuwa shughuli
za uchukuzi na mawasiliano zimefikia kasi ya ukuaji wa asilimia 16.5
katika kipindi hicho na kuongeza kuwa huduma za hoteli na migahawa
zimefikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.0, huku shughuli za uendeshaji wa
Serikali zikifikia asilimia 5.1, Elimu asilimia 5.2, huduma za Sfya
na shughuli nyingine zikikua kwa asilimia 4.5.
Aidha, amefafanua kuwa sekta ya
umeme katika robo ya mwaka 2014 imekua kwa asilimia 12.6 ikilinganishwa
na asilimia 6 ya mwaka uliopita kutokana na kupatikana kwa vyanzo
mbadala vya kuzalisha umeme hususan ugunduzi wa gesi nchini ambao
umeondoa tatizo la utegemezi wa umeme wa maji katika kuzalisha umeme.
“Kwa kipindi kirefu sekta ya
umeme imekuwa na mawimbi kwa kiasi kikubwa , umeme wetu umekuwa wa
kutegemea maji ya mvua, baada ya juhudi za Serikali na kugundulika kwa
nishati ya Gesi nchini na kupatikana chanzo mbadala cha nishati tatizo
hili limeshghulikiwa sasa sekta hii imeimarika” Amesisitiza.
Amesema Tanzania sasa inafanya
vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuwa ya pili
ikifuatiwa na Uganda, Rwanda na Burundi na kuongeza kuwa hali ya amani
na utulivu iliyopo nchini inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kukua
zaidi kiuchumi.
Kwa upande wake mtaalam wa wa
Uchumi kutoka Benki Kuu ya Taifa (BOT) Bw. Davidi Kwimbere akifafanua
kuhusu hali iliyopo ya ukuaji wa uchumi amesema kuwa imechangiwa na
kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji .
Amesema sekta ya
Kilimo na uzalishaji wa mazao imekua kutokana na matumizi ya mbolea,
zana bora za kilimo, mbegu bora, madawa na kufafanua kuwa endapo juhudi
zaidi zitaendelea kufanywa na wananchi kwa kuingia katika shughuli
mbalimbali za uzalishaji uchumi utaendendelea kuonekana kwa mtu mmoja
mmoja.
Amefafanua kuwa
maendeleo katika nchi yoyote yanachukua muda na kutoa wito kwa nchi za
Afrika kuendelea kujifunza na kufafanua kuwa nchi zote zilizopiga hatua
kimaendeleo mpaka kufikia asilimia 15 ikiwemo China iliwachukua miaka
20 kuondoa umasikini.
Amesema Tanzania
inayo nafasi nzuri kukua kiuchumi kutokana na kuendelea kuimarika kwa
miundombinu na ukuaji wa sekta za ujenzi, Nishati, madini, Viwanda,
umeme , kilimo na uvuvi hali inayochangia kuongezeka kwa uwekezaji.
No comments:
Post a Comment