Pages

KAPIPI TV

Monday, September 1, 2014

CHADEMA TABORA WAPATA MWENYEKITI MPYA

Na Allan Ntana, Tabora

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Tabora kimepata safu mpya ya uongozi baada ya kufanya uchaguzi wake mkuu katika ngazi ya mkoa hapo jana katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Tabora.

Katika mkutano huo wa uchaguzi nafasi zilizokuwa zinagombewa ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa na Katibu wa Mkoa na Mwenyekiti na Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Baraza la Wanawake (BAWACHA) na Baraza la Wazee.

Aliyeibuka kidedea katika nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora ni Bw. Francis William Msyuka aliyepata kura 46 na kumshinda mgombea mwenzake Bw.Hassan Said aliyepata kura 17 kati ya kura zote 66 zilizopigwa huku kura 3 zikiharibika.

Na aliyeibuka kidedea katika nafasi ya Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tabora ni Bw.Alinanuswe Mwakilima ambaye alipigiwa kura za ndio 57 na hapana 2 kati ya kura zote 61 baada ya kukosa mpinzani katika wajumbe wote waliohudhuria mkutano huo.

Waliochaguliwa kuongoza mabaraza ya chama hicho katika ngazi ya mkoa ni, BAVICHA, Mwenyekiti ni Lazaro Damson na Katibu wake ni Daud Ndelwa, BAWACHA Mwenyekiti ni Sada Kabezi na Katibu wake ni Anna Nyawacha na Baraza la WAZEE Mwenyekiti ni Joseph Tanganyika na Katibu wake ni Vicent Ndeuka.

 Msimamizi wa Uchaguzi huo Christopher Nyamwanji ambaye ni Mratibu wa chama hicho Kanda ya Magharibi aliwapongeza wajumbe wote waliohudhuria mkutano huo kwa kufanikisha zoezi hilo la kikatiba ndani ya chama kwa utulivu na amani huku akiwataka kukitumika chama hicho kwa moyo mmoja pasipo kuruhusu roho za usaliti kama walivyofanya viongozi waliokuwepo.

Naye diwani wa kata ya Bukene wilaya ya Nzega Omar Shehe kupitia chama hicho ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo wa Uchaguzi aliwataka viongozi hao kudumisha amani, mshikamano na uzalendo ndani ya chama hicho na kujiepusha na makundi ili kuwaunganisha vizuri wanachama katika mkoa huo hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu hauko mbali sana huku akiwaasa kutogopa changamoto za hapa na pale.

Akitoa shukrani zake Mwenyekiti mpya wa chama hicho Mkoa wa Tabora Francis William Msyuka alisema kazi kubwa iliyoko mbele yake ni kutengeneza mshikamano mzuri kwa viongozi wote na wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina, wilaya, jimbo na mkoa na kuhamasisha maendeleo katika kila eneo husika sambamba na kukutana na wananchi ili kusikiliza kero zao.

No comments: