Pages

KAPIPI TV

Saturday, August 2, 2014

WATENDAJI HALMASHAURI SIKONGE WAPONGEZWA

Mkuu wa wilaya ya Sikonge Bi.Hanifa Selengu akizungumza katika baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge.
Na Allan Ntana, Sikonge

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Sikonge mkoani Tabora
Shadrack Mhagama na watendaji wake wamepongezwa kwa jitihada zao nzuri
kiutendaji ambazo zimefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo kwa kiwango kikubwa.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani
Sikonge Abisai Mbogo katika kikao cha baraza la madiwani wa
halmashauri ya wilaya hiyo kilichoketi jana katika ukumbi wa mikutano
wa Ndawkilo mjini hapa.

Mbogo alisema mikakati mizuri na mafanikio makubwa yanayoanza
kuonekana sasa katika halmashauri ya wilaya hiyo yanachangiwa na
ushirikiano mzuri uliopo baina ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri,
watendaji wakuu wa idara, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, madiwani, DC
na mbunge wa jimbo hilo.

Alieleza kuwa karibu kila mwaka halmashauri hiyo ilikuwa inapata hati
yenye mashaka katika taarifa zake za ukaguzi jambo lililokuwa
linachangiwa na ushirikiano mbovu baina ya watendaji hao.

‘Nimefurahi sana tumepata hati safi katika msimu uliopita , hili ni
jambo la kujivunia na la kupongezwa kwa kuwa tulikuwa tunapata hati za
mashaka tu, na hii ilimaanisha kuwa watendaji hawakuwa na ushirikiano
wowote katika utekelezaji wa majukumu yao, kulikuwa na uzembe mwingi’,
alisema.

Aliongeza kuwa jitihada zote zinazofanywa na Mkuu wa wilaya hiyo
Hanifa Selengu katika kuhamasisha uanzishaji miradi ya ufugaji nyuki
kwa kila kaya na suala zima la ulinzi na usalama wilayani humo zinafaa
kuungwa mkono.

Aidha alisema jitihada za Mbunge wa jimbo hilo Said Nkumba katika
kutetea na kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia kilimo cha
tumbaku ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi wilayani humo.

Mbogo aliwataka watendaji wote wa halmashauri hiyo kutobweteka na sifa
za hati safi bali waendelee kurekebisha kasoro ndogo ndogo za
kiutendaji na mapungufu kadha wa kadha waliyo nayo kwa kufanya kile
kinachotakiwa kwa faida ya wananchi.

Aidha Mbogo alitoa wito kwa madiwani wote kufanya kila linalotakiwa
kwa wananchi wao hasa katika kipindi hiki cha lala salama kabla ya
vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwakani halijaanza vinginevyo
watahukumiwa na wananchi.

Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Richard Lugomela
ambaye pia ni Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa aliipongeza
halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuwa miongoni mwa halmashauri 20
zilizofanya vizuri sana katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Pia alimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kusimamia na kuhamasisha
suala zima la uchangiaji mfuko wa afya ya jamii (NHF) sambamba na
kusimamia uanzishwaji wa mfuko wa elimu na sheria ndogo ndogo
zitakazosaidia kukusanya mapato ya ndani kutokana na uchimbaji madini
unaoendelea wilayani humo.

No comments: