Mashine ya kusaga makaa yam awe
katika viwango mbalimbali kulingana na mahitaji ya wateja ikiendelea na
kazi ya kusaga mawe katika Mgodi wa Mkaa ya Mawe wa Ngaka unaomilikiwa
kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na kampuni ya Australia.
Gari la kubeba makaa ya Mawe
katika mgodi wa Ngaka likimwaga makaa sehemu maalum kutoka mgodini kabla
ya kusagwa katika viwango mbalimbali kulingana na mahitaji y wateja.
Meneja wa Kampuni ya TANCOAL
(wanne kulia) Tan Brereton na Mkuu wa Masoko wa kampuni hiyo Emmanuel
Constantinides (wa tatu kulia) wakimwonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini Eliakim Maswi na ujumbe wake namna shughuli za himbaji
Makaa ya Mawe zinavyofanyika.
…………………………………………………………………………
*Aeleza TMAA wapo kuhakiki mwenendo wa uzalishaji,uuzaji
* Mwekezaji asisitiza Makaa ya Ngaka yana ubora wa juu
Na Asteria Muhozya, Mbinga
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
amewataka watanzania kuondoa dhana kuwa madini yanayochimbwa katika
migodi mbalimbali nchini yanaibwa na wawekezaji wakubwa na kusisitiza
kuwa, Wizara kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), wapo
katika migodi yote nchini kuhakikisha kwamba madini hayo hayatoroshwi .
Maswi ameyasema hayo alipotembelea Mgodi wa kuchimba Makaa ya
Mawe wa kampuni ya Tancoal eneo la Ngaka wilayani Mbinga inayomilikiwa
kwa ubia kati ya Kampuni ya Australia na Shirika la Maendeleo ya Taifa
(NDC) na kuongeza kuwa, TMAA wapo katika kila mgodi kujua kiasi cha
madini kinachochimbwa, kinachouzwa na kwa ajili ya kuhakiki vyeti vya
mauzo ya madini hayo kuhakikisha kuwa vinakwenda sambamba na kiasi cha
mrahaba kinachotolewa na wawekezaji.
Kwa upande wake Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul
Masanja alisisitiza hoja ya Katibu Mkuu Maswi na kuongeza kuwa, Wizara
kupitia maafisa wa TMAA wamekuwa wakifanya ukaguzi kuhakikisha kwamba
serikali inapata mrahaba stahili kupitia madini yanayouzwa na kutoa
mfano kwa madini ya Makaa ya Mawe ya Ngaka kwamba serikali inapata
asilimia 100 ya mrahaba.
“Nawapongeza sana TanCoal ni wasikivu, maafisa wa TMAA huwa
wanafanya ukaguzi kila baada ya miezi mitatu kujua kiasi kinachozalishwa
na kinachouzwa hivyo, tunakwenda nao vizuri,” alisisitiza Masanja.
Naye Mkurugenzi wa Tancoal Tan Brereton ameeleza kuwa, mgodi wa
wa Ngaka ni mradi mkubwa kwa Tanzania na kuongeza kuwa, uwepo wa mgodi
wa makaa ya mawe wa Tancoal ni mafanikio na maendeleo makubwa kwa
Tanzania kutokana na kuwezesha ajira kwa wataalamu mbalimbali nchini
ikiwemo serikali kupata kodi na mirahaba kupitia mgodi huo jambo ambalo
litawezesha kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, amezitaja faida za nyingine za mgodi huo kuwa, uwepo wa
Mgodi huo utawezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha nishati ya
umeme kutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha makaa hayo katika mgodi wa
Ngaka na kueleza kuwa, makaa ya mawe kutoka katika mgodi huo yana ubora
wa kiwango cha juu tofauti na madini yanayochimbwa nchini Afrika Kusini.
“Makaa ya Ngaka yana ubora wa hali ya juu sana tofauti na makaa
ya nayochimbwa Afrika Kusini kwasasabu madini haya hayahitaji kusafishwa
kabla ya matumizi tofauti na mengine ambayo husafishwa kabla ya
kutumiwa ,alisisitiza Tan.
Aidha ameongeza kuwa, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha kiasi
cha tani 480,000 za makaa ya mawe kwa mwaka na kuongeza kuwa, tayari
kampuni hiyo imesaidia huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo ya
afya,shule ,maji na kuwaendeleza vijana na kutumia zaidi ya shilingi
milioni mia sita na kuongeza kuwa, kampuni hiyo imekwisha toa kiasi za
bilioni 2 kama kodi na mrahaba kwa serikali.
Kwa mujibu wa Tan, ameeleza kuwa, makaa yanayozalishwa na
kampuni hiyo yanatumika katika viwanda vya saruji vya Mbeya Tanga Lake,
kampuni ya METL na viwanda vya karatasi viwanda vya nguo.
No comments:
Post a Comment