Mtoto Pendo Sengerema(14)mkazi wa Kijiji cha Usinge wilayani Kaliuwa ambaye kwasasa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo akipatiwa matibabu kufuatia kujeruhiwa kwa kukatwa mkono na watu wasiojulikana na kisha kutoweka nao.
Pendo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Usinge hali yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibau katika hospitali ya wilaya ya Urambo.
Akizungumzia tukio hilo kwa kutumia lugha ya kabila la Wasukuma,Pendo ambaye kwasasa yupo katika uangalizi mkali wa Jeshi la Polisi katika Wodi maalumu alisema watu watatu ambaye mmoja tayari amemfahamu walifika nyumbani kwao majira ya saa tatu usiku na kubisha hodi ambapo waliingia ndani na kumuangusha chini kisha kumkata mkono na kuondoka nao mbio.
"Sisi tulikuwa ndani tunakula chakula na mama,walipoingia tu mmoja akaniangusha chini mwingine akanikata na upanga huku akinikataza kupiga kelele,...alinikata mara mbili tu akauchukua mkono wangu akakimbia,mimi nilikuwa nimekaa chini ninawaangali tu bila kupiga kelele"alisema Pendo
Kwamujibu wa Pendo watu hao baada ya kutekeleza unyama huo walikimbia ndipo wakaanza kupiga mayowe kwa lengo la kuomba msaada.
"Mama yangu ni kipofu hakuona walivyonikata isipokuwa alikuwa akisikia wakati wananiambia nisipige kelele ingawa nilikuwa nasikia maumivu makali sana"aliendelea kueleza huku akiweka wazi kuwa katika watu aliowaona mmoja alimtambua kabisa.
Maafisa wawili kutoka Kituo cha Sheria na haki za binadamu LHRC Bw.Mkuta Masoli anayehudumu dawati linaloshughulikia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na Wakili wa Kituo hicho Mwanasheria Reginald Martin walifika katika hospitali ya wilaya ya Urambo kumjulia hali mtoto huyo Pendo na kupata maelezo yake kuhusu mkasa huo.
Katika tamko la LHRC lililotolewa na Bw.Masoli alieleza kuwa LHRC imelaani vikali unyama huo na kuviomba vyombo vya dola kushirikiana katika kukabiliana na wimbi la mauaji ya Walemavu wa ngozi albino ambayo yameanza kujitokeza tena kwa siku za hivi karibuni.
"Kitendo hiki ni cha kinyama ni vema tushirikiane katika kukomesha ukatili wa aina hii ni wazi kwamba Walemavu wa ngozi ni binadamu wa kawaida na wanahaki kama walivyowengine,taifa linaingia katika kashfa ya ukiukwaji wa haki za binadamu"alisema Masoli huku akiitaka jamii kuvisaidia vyombo vya dola katika kuwafichua wanaofanya uharamia huo kwa imani za kishirikina
Hata hivyo bado jamii mkoani Tabora inahitaji elimu kuhusu haki za binadamu kutokana na ukweli kwamba matukio ya mauaji yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara yakiwemo ya watu wenye ulemavu wa ngozi albino huku jamii ya vikongwe nayo ikiendelea kuwa katika mazingira hatarishi ya kuuawa kwa imani hizo za kishirikina.
No comments:
Post a Comment