Waziri wa maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu katika picha ya pamoja na Wahitimu wa mahafali ya tatu Chuo cha Nyuki Tabora |
SERIKALI imeahidi kupandisha hadhi ya Chuo cha
Mafunzo ya Nyuki kilichoko mkoani Tabora ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi
kutoka ndani na nje ya nchi kujiunga na chuo hicho.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii
Razaro Nyarandu aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 3 ya Chuo hicho
yaliyofanyika juzi chuoni hapo.
Alisema kutokana na umuhimu wa Chuo hicho
atahakikisha kinaboreshwa zaidi ili kiwe kitovu cha ubora katika taaluma ya
sayansi ya misitu na nyuki na hifadhi zake na kwa kuanzia ameahidi kuwasiliana
na wataalamu wa wizara hiyo ili wahuishe mitaala yake ili kukiongezea hadhi.
‘Tunataka chuo hiki kiwe kimbilio la wanafunzi
kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi, tutakiboresha zaidi
ili kiwe kitovu cha ubora katika sayansi ya misitu na nyuki’, alisema Waziri
Nyarandu.
Aliongeza kuwa Wizara yake itajitahidi
kuzishughulikia changamoto zote zinazokikabili ikiwemo suala la upungufu wa
watumishi ili kuhakikisha chuo hicho na sekta zingine zilizoko ndani ya Wizara
hiyo zinakuwa na watumishi wa kutosha sambamba na kutoa fursa za ajira kwa askari
wa wanyama pori na wataalamu wengineo.
Lengo ni kuhakikisha ulinzi wa kutosha unakuwepo
katika maeneo yote ya hifadhi za misitu sambamba na kuwezesha shughuli zingine
zote ziendelee vizuri katika maeneo hayo ikiwemo ufugaji nyuki.
Awali akisoma risala ya Chuo mbele ya Waziri, Mkuu
wa Chuo hicho Semu L. Daud alisema tangu Mafunzo ya Chuo hicho yarudishwe rasmi
mkoani Tabora chuo hicho kimeanza kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza
udahili wa wanafunzi kutoka 34 kwa mwaka
2010/2011 hadi 115 kwa mwaka 2014/15, huku akibainisha kuwa wanafunzi 58 wa
kike na kiume kwa mwaka 2013/14 wamehitimu mafunzo hayo katika ngazi ya
Astashahada na Stashahada ya Ufugaji Nyuki .
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na Chuo
kupata utambulisho maalumu toka Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) wa Ithibati
ya muda (Partial Accreditation), ili kuthibitisha umuhimu wa taaluma inayofundishwa
na Chuo hicho wamepewa fursa ya kushiriki katika Maonyesho ya Biashara na
Kilimo (Sabasaba na NaneNane) kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa ili kuelimisha
wananchi.
Aidha Mkuu wa Chuo alitaja changamoto mbalimbali
zinazokikabili chuo hicho kuwa pamoja na
upungufu wa watumishi wasio wakufunzi hususani Afisa Utumishi, Wakutubi,
Wapishi, Madereva, Afisa Ugavi, walinzi na mwangalizi wa masijala.
Changamoto nyingine ni tatizo la uhaba wa vifaa vya
kisasa vya kufundishia ikiwemo vitabu na chombo cha usafiri hasa kwa shughuli
za utawala na shughuli za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
Aidha alibainisha kuwa hadhi ya Chuo hicho
itaongezeka pale tu mikakati yote ya kukipanua na kukiboresha itakapotekelezwa
ipasavyo hivyo akaiomba serikali kupitia Waziri mwenye dhamana kuangalia
uwezekano wa kuongeza fungu la bajeti ya Chuo hicho ili jitihada za kuboresha
miundombinu hiyo zianze mra moja.
No comments:
Post a Comment