Pages

KAPIPI TV

Monday, July 28, 2014

MUME ADAIWA KUMUUA MKEWE - TABORA

Mwanamke aliyejeruhiwa baada ya kupigwa na mumewe.
Na  Mwandishi wetu maalumu.
Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Ntarikwa manispaa ya Tabora aliyefahamika kwa jina la Rehema Hassan(28) anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na mumewe baada ya ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi majira usiku wakiwa nyumbani kwao.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea  mwishoni mwa wiki  majira ya saa saba usiku wakati wanandoa hao walipokuwa wameingia ndani kwa lengo la kutaka kulala.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntarikwa Bw. Ali  Hamisi Mdaki amemtaja mwanaume aliyemuua  mkewe ni Hamad Mohammed Kasanzu(25)ambaye alidai alifanya mauaji hayo baada ya kumkuta na barua iliyokuwa ikihisiwa ya mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.

Mdaki alisema ugomvi huo wa wivu wa kimapenzi kati ya Hamad na mkewe ambaye kwasasa ni marehemu ulisababisha mwanaume huyo kumpiga na kumjeruhi vibaya mkewe na baada ya kutekeleza unyama huo alikimbia kusikojulikana na kumuacha mkewe chumbani akiwa amepoteza maisha huku chumba cha pili mke mwingine ambaye ni bimkubwa akimuonya kutoeleza ukweli wa tukio hilo la kinyama.

Aidha alipoulizwa kuhusu tukio hilo kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora kamishna msaidizi Suzan Kaganda alithibitisha kuwepo kwa mauaji hayo huku akieleza Jeshi la Polisi bado linamsaka mtuhumiwa wa mauaji hayo ya kikatili.

Hata hivyo duru kutoka maeneo ya Ntarikwa zinaeleza kuwa mwaume huyo ambaye ni dereva wa Bodaboda Hamad Kasanzu amefichwa na ndugu zake wa karibu akijaribu kukwepa mkono wa sheria kuhusiana na tukio la kinyama alilolitenda.

Aidha kwa upande mwingine inakadiriwa kuwa wastani wa asilimia 65 ya wanawake walio ndani ya ndoa na nje ya ndoa wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia na wanaume na hivyo mbali ya kusababisha vifo visivyo na hatia lakini wanawake wamekuwa na unyonge wa kupindukia. 

No comments: