Na Anna Nkinda – Maelezo, Nachingwea
Wanafunzi wa kike wa vyuo
vya ualimu nchini wametakiwa kuvaa mavazi nadhifu yanayoendana na
maadili ya kazi yao ili wanafunzi na jamii inayowazunguka ijifunze
kutoka kwao kwani wao ni kioo cha jamii.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na baadhi ya wanafunzi
wa kike wa chuo cha Ualimu Nachingwea mara baada ya kumalizika kwa
futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi wa wilaya iliyofanyika chuoni
hapo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe
wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema siyo
jambo jema kwa mwalimu kuvaa mavazi yanayoonyesha sehemu za miili yao
ikiwemo kata mikono, nguo zinazobana na sketi fupi kwa kufanya hivyo ni
kwenda kinyume na haiba ya ualimu.
Alisema, “Sikuhizi kuna baadhi ya
watu wanavaa mavazi yasiyoendana na utamaduni wa mtanzania, nyinyi kama
walimu ambao ni kioo cha jamii na mnawafundisha wanafunzi madarasani
msifanye hivyo kwa kufanya hivyo watoto wataiga na kufikiria kuwa kuvaa
mavazi hayo ni sawa”.
Mama Kikwete pia aliwataka
wanafunzi hao kutokuchagua maeneo ya kwenda kufanya kazi pindi
wamalizapo masomo yao na kupangiwa vituo vipya vya kazi kwani kazi ya
ualimu ni wito na kama mtu hakuipenda kazi hiyo basi angechagua fani
nyingine za kusoma.
“Baadhi ya walimu wamekuwa
wakikataa kwenda kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na wengine
wakipangiwa vituo vya mbali na mjini wanaogopa na kudiriki hata kuacha
kazi, kama ni hivyo kwa nini ulipoteza fedha na muda wako kusomea
ualimu?” , aliuliza Mama Kikwete.
MNEC huyo alimalizia kwa kuwataka
wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi
wawapo masomoni kitendo ambacho kitawasaidia kumaliza masomo yao salama
na kurudi nyumbani bila ya kufukuzwa chuo kwa ajili ya kupata ujauzito.
Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni
mwalimu miaka ya nyuma alisoma chuo cha ualimu Nachingwea na juzi akiwa
chuoni hapo alitembelea Bweni la wasichana la Kawawa ambalo ndilo
alilokuwa analala wakati akiwa mwanafunzi wa chuo hicho.
No comments:
Post a Comment