Pages

KAPIPI TV

Sunday, July 20, 2014

ACT YAZOA VIONGOZI WA CHADEMA TABORA


Na Mwandishi wetu maalumu.
 
CHAMA kipya cha siasa hapa nchini Alliance for Change and Transparency
(ACT) kimedhamiria kukiondoa madarakani chama tawala (CCM) kwa kuwa
viongozi wake hawana uchungu na dhamira ya kweli ya kumaliza kero za
wananchi zilizokithiri katika
nyanja mbalimbali hapa nchini jambo ambalo limechangia wananchi wengi
kuwa na maisha duni.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Kadawi Lucas
Limbu katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika uwanja wa
stendi ya zamani mjini Tabora ambapo alieleza kuwa CCM imeshika dola
kwa mda mrefu sana lakini viongozi wake hawajali wananchi na hawana
uzalendo kwa Taifa.

Limbu alisema inasikitisha sana kuona Watanzania walio wengi
wakiendelea kuishi katika hali ya sintofahamu wakati nchi yao
imejaliwa kuwa na utajiri mwingi sana, badala yake utajiri huo ambao
ni rasilimali za Taifa ukiendelea kuibiwa na watu wachache badala ya
kuwanufaisha wazawa wote.

Alisema tokea nchi hii inapata uhuru baba wa Taifa hayati Mwalimu
Nyerere alisimama imara kupinga aina zote za unyonyaji, alikemea
vikali mtu au kiongozi yeyote yule kujinufaisha kupitia mgongo wa
wanyonga sambamba na kufukuza viongozi wazembe na wasio waadilifu
wasiotetea maslahi ya mwananchi.

Alibainisha kuwa CCM haina viongozi wenye uchungu wa kutetea wanyonge
na kusimamia rasilimali za nchi yao kama alivyokuwa Mwl Nyerere ndio
maana watu wachache wanazidi kunemeeka wakati kero za wananchi
zikizidi kuongezeka kila kona ya nchi, kero za ardhi, madini, elimu
n.k hazikustahili kuwepo mpaka sasa, enzi za Nyerere elimu ilikuwa
bure, yeye aliwezaje, CCM wameshindwaje?

Akizungumzia msimamo wa ACT katika mchakato wa katiba mpya unaoendelea
sasa Limbu alisema wanataka serikali 3 zilizoboreshwa zitakazokuwa na
Rais mmoja tu wa Jamhuri ya Muungano, kama Rais atatoka upande fulani
wa Muungano upande uliobaki utoe Makamu wa Rais na kila upande uwe na
mtendaji mkuu wa serikali na bunge lake.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Samson Mwigamba alisema ACT ndicho chama
pekee chenye uwezo wa kuing’oa CCM madarakani kwa kuwa kimedhamiria
kusimamia fursa zote zilizoko hapa nchini zimnufaishe mwananchi na
nguvu yake kubwa ni kujali uzalendo, usawa, uwazi, demokrasia n.k
wakati vyama vingine vimejaa ubinafsi tu na vimeshindwa kulisimamia
hilo.

Kaimu Katibu wa Mawasiliano na Uenezi  wa chama hicho Mohamed Masaga
alisema ACT haina mpango wa kuua chama chochote cha Siasa bali ACT
imekuja kuleta demokrasia ya kweli na kusimamia rasilimali za Taifa
ili zisomeshe watoto wetu, ziondoe umaskini na kuleta uzalendo.

Katika mkutano huo wanachama zaidi ya 90 kutoka vyama mbalimbali vya
siasa walijiunga na chama hicho wakiwemo Katibu wa CHADEMA mkoa wa
Tabora Bw.Athman Alfan balozi, aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani
Tabora Hussein Juma Wakundecha, aliyekuwa mjumbe wa NEC CHADEMA Maulid
Bwiru ambaye sasa ndiye Kaimu Mwenyekiti wa ACT mkoa wa Tabora.

Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kata ya Chemchem katika manispaa ya
Tabora kupitia CHADEMA Idd Omar  na aliyekuwa mgombea udiwani kupitia
CHADEMA katika uchaguzi uliopita katika kata ya Kitongoni mjini Kigoma
Kacheche Maulid Kacheche.

No comments: